Mar 06, 2017 07:03 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Machi 6, 2017

Ufuatao ni mkusanyiko wa matukio kadhaa muhimu ya michezi yaliyojiri katika muda wa siku saba zilizopita, ndani na nje ya nchi.......

Rais Rouhani awaenzi wanariadha wa Iran waliong'ara Rio

Rais Hassan Rouhani wa Iran ameshiriki hafla za kuwaenzi wanariadha wa Jamhuri ya Kiislamu walioshiriki katika michezo ya Olimpiki ya Rio mwaka jana 2016. Akiongea katika sherehe hizo siku ya Jumamosi, Dakta Rouhani amesema timu ya taifa ya Iran katika michezo ya Olimpiki na Paralimpiki huko Brazil ilibeba ujumbe wa maadili, amani na urafiki katika medani ya michezo ya kimataifa sambamba na ujumbe wa matumaini na nishati kwa taifa la Iran ndani ya nchi. Rais wa Iran amesema mafanikio yoyote yale ya Wairani huwapa fahari wananchi na kuzidisha fahari ya taifa lakini fahari hiyo hufikia kileleni wakati Jamhuri ya Kiislamu inapopata ushindi mkabala wa adui yake. Dakta Rouhani amesema michezo ni chimbuko la matumaini na huimarisha umoja, usalama na utangamano wa jamii. Katika hafla hiyo, Morteza Mehrzad alipokea Tuzo ya Heshima ya Rais kwa kufanya vyema timu ya walemavu ya voliboli katika mashindano hayo ya Rio. Timu ya Olimpiki ya Iran ilijinyakulia medali 3 za dhahabu, moja ya fedha na nne za shaba na kuambulia nafasi ya 25 kimataifa. Timu ya Paralimpiki (wanariadha walemavu) ya Iran ilishinda medali 8 za dhahabu, nne za fedha na saba za shaba, katika mashindano ya Olimpiki ya Rio De Janairo nchini Brazil mwaka jana 2016. 

Wanamieleka wa Iran wazoa medali 8 Ukraine

Wanamieleka wa Iran mtindo wa Greco-Roman imezoa medali kochokocho katika duru ya 21 ya mashindano ya mchezo huo nchini Ukraine. Katika mashindano hayo ya Kuwaenzi Wanamieleka na Makocha Bora wa Ukraine yaliyofanyika katika mji mkuu Kiev, wanamieleka Farshad Belfakkeh na Reza Afazli walishinda medali 2 za dhahabu katika kategoria ya kilo 74 na 71.

Mieleka Ukraine

Shirzad Beheshti aliipa Iran medali ya fedha kategoria ya kilo 59, huku Reza Atari na Hossein Shahbazi wakitia kibindoni medali ya shaba kila mmoja. Siku ya Jumamosi Wanariadha wa Kiirani wa mindo wa Freestyle Payman Biabani naSaeed Qiyasi waliiongezea Iran shaba moja kila mmoja huku Hamed Rashidi akijinyakulia fedha katika safu ya wanamieleka wenye kilo 70. Mashindano hayo ya kimataifa yanayojulikana kama Outstanding Ukrainian Wrestlers and Coaches Memorial yalianza Machi 2 na kufunga pazia lake Machi 4, kwa kuwaleta pamoja wanamieleka kutoka nchi mbali mbali kama vile Iran, Japan, Brazil, Ufaransa, Tunisia na Marekani.

Guinea yatinga Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya soka ya Guinea imefuzu kushiriki Kombe la Dunia la soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 baada ya kuishinda Mali. Katika mchuano huo uliopigwa Jumamosi, vijana wa Conackry waliichabanga Mali mabao 3-2 katika mchuano wa kufuzu Kombe la Afrika uwanjani Levy Mwanawasa mjini Ndola nchini Zambia. Guinea inajiunga na Zambia, ambayo iliibandua Misri nje ya mbio za kuingia Kombe la Dunia kwa kuilima mabao 3-1 jijini Lusaka. Zambia ilishinda Kundi A kwa pointi tisa baada ya kulemea Guinea 1-0 na Mali 6-1 katika mechi zake mbili za ufunguzi. Timu mbili bora kutoka kundi B linalijumuisha Afrika Kusini, Senegal, Cameroon na Sudan pia zitajikatia tiketi ya kuelekea nchini Korea Kusini kwa Kombe la Dunia litakalofanyika mnamo Mei 20 hadi Julai 11. Jumla ya mataifa 22 tayari yamefuzu kuwania ubingwa wa dunia. Mataifa hayo ni Korea Kusini (wenyeji), Iran, Japan, Saudi Arabia, Vietnam (Asia), Guinea, Zambia (Afrika), Costa Rica, Honduras, Mexico, Marekani (CONCACAF), Argentina, Ecuador, Uruguay, Venezuela (Amerika Kusini) na Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Ureno (Ulaya). Timu zitakazocheza nusu fainali ya AFCON 2017 U20 zitawakilisha Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia kwa timu za taifa za vijana wasiozidi miaka 20 iliyopangwa kuchezwa mwezi Mei na Juni 2017 nchini Korea ya Kusini. Michuano hii ya AFCON 2017 U20 itamalizika Machi 12.

Riadha, Kenya yaibuka kidedea Marathon Japan

Mwanariadha nguli wa Kenya Ezekiel Chebii ameibuka mshindi katika mbio za Lake Biwa Mainichi Marathon nchini Japan siku ya Jumapili. Chebii mwenye umri wa miaka 26, alifuata nyayo za washindi wa mwaka 2015, Samuel Ndung’u na mwaka 2016 Lucas Rotich kwa kukamilisha umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:09:06. Mkenya mwingine Vincent Kipruto, ambaye alishinda makala ya mwaka 2013, alimfuata unyounyo na kumaliza katika nafasi ya pili kwa kutumia saa 2:09:15.  Raia wa Uganda, Solomon Mutai aliridhika na nafasi ya tatu (2:09:59). Wakati huohuo, Michael Githae ameshinda makala ya tatu ya mbio za Shizuoka Marathon nchini Japan kwa kutumia saa 2:11:40, siku hiyo hiyo ya Jumapili.

Ligi ya Premier

Tunafunga kipindi kwa kutupia jicho baadhi ya mechi za Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza na msimamo wa jedwalila ligi hiyo. Klabu ya Manchester United ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Bornemouth kwenye mchezo wa aina yake wa Ligi ya Premier uliofanyika Jumamosi. Kwenye mechi hiyo mfumania nyavu mahiri wa timu hiyo, Zlatan Ibrahimovic alikosa penalti wakati Bornemouth wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake, Andrew Surman kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumsukuma Ibrahimovic katika kipindi cha kwanza. Man U ndio waliokuwa wa kwanza kucheka na nyavu kwenye dakika ya 23 kupitia kwa beki wa kimataifa wa Argentina, Marcos Rojo akimalizia krosi ya beki wa pembeni Antonio Valencia. Bournemouth walisawazisha bao hilo dakika tano kabla ya mapumziko kupitia mkwaju wa penalti kupitia kwa Joshua King baada ya beki wa Manchester United, Phil Jones kumuangusha Marc Pugh kwenye eneo la hatari. Kutokana na matokeo hayo, Manchester United imeendelea kubaki kwenye nafasi yake ya sita ikiwa na pointi 49 baada ya kucheza mechi 26. Aidha Jumamosi ilishuhudia mchezo kati ya Majogoo wa jiji la Liverpool dhidi ya Wabeba Bunduki wa London. Arsenal ambao wapo katika harakati ya kumuaga mkufunzi wa muda mrefu Arsene Wenger, walikubali kichapo cha magoli 3-1 kutoka Liverpool ambao walikuwa wanaupiga nyumbani Anfield. Magoli ya Liverpool yalifungwa na Roberto Firmino dakika ya 9, Sadio Mane dakika ya 40 na Georginio Wijnaldum dakika ya 90. Goli la kufutia machozi la Gunners lilitiwa kimyani kunako dakika ya 57 kupitia kiungo Danny Welbeck.Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kushuka hadi nafasi ya 5 wakiwa na point 50, huku Liverpool wakipanda hadi nafasi ya tatu kwa point 52. Tottenham wakiwa nyumbani wameiadhibu Everton mabao 3-2 wakati ambapo Sunderland walikuwa wakipkea kichapo cha mbwa cha mabao 2-0 kutoka Machesetr City.

…………………………………TAMATI…………………………

 

Tags