Mar 27, 2017 11:06 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Machi 27

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, ndani na nje ya nchi...........

Iran yaichachafya Qatar, yajisogeza Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeitandika Qatar bao moja la uchungu katika mchuano wa kutafuta tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2018. Katika kipute hicho cha Alkhamisi, Qatar licha ya kuchezea nyumbani uwanja wa Jassim Bin Hamad mjini Doha, ilishindwa kufurukuta mbele ya vijana wa Iran na kukubali kichapo cha bao 1-0. Bao la Iran lilipachikwa kimyani na Mehdi Taremi kunako dakika ya 52.

Ushindi huo umeifanya Iran ijikite kileleni mwa Kundi A ikiwa na alama 14 katika mechi 6 ilizocheza hadi sasa. Qatar inavuta mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi 4. Vijana wa mkufunzi Carlos Queiroz wanatazamiwa kuvaana na China Jumanne hii katika mchuano mwingine wa kusaka nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia mwakani. Timu nyingine ambazo ziko katika Kundi A ni South Korea, Uzbekistan na Syria.

Iran yapeta mashindano ya kupiga mshale (Archery)

Mchezo wa kupiga mshale (Archery)

Mabingwa wa mchezo wa kulenga shabaha kwa mshale (Archery) wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameshinda medali mbili za dhahabu katika Kombe la Asia la mashindano hayo nchini Thailand. Siku ya Ijumaa, Esmaeil Ebadi aliipa Iran ya Kiislamu medali ya dhahabu katika kategoria ya wapiga mshale wa kiume katika uwanja wa Archery Range of the Sports Authority of Thailand, mjini Bangkok baada ya kusanya jumla ya alama 147. Alifuatiwa kwa karibu na Mohammad Juwaidi Mazuki wa Malaysia aliyepata pointi 146 na kutwaa fedha. Mchezaji Parisa Baratchi wa Iran alimlemea hasimu wake Mfilipino Amaya Amparo Cojuangco katika safu ya wanawake na kuipa Iran dhahabu ya pili, baada ya kuzoa alama 146 dhidi ya 141 za mshindani wake. Mashindano hayo ya dunia ambayo ayanafahamika kwa kimombo kama The 2017 Asia Cup-World Ranking Tournament, Stage II and World Games 2017 Wroclaw Archery Qualification yalianza Machi 19 na kufunga pazia lake Jumapili ya Machi 26 katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok.

Mbio za Nyika: Kenya yatamalaki mashindano ya dunia Kampala, Uganda

Wanariadha wa Kenya wametamalaki katika duru ya 42 ya mashindano ya kimataifa ya mbio za Nyika yaliyofunga pazia lake Jumapili jioni katika uwanja wa Kololo katika mji mkuu wa Uganada, Kampala. Mwanaridha Geoffrey Kamworor wa Kenya alitetea taji aliloshinda mwaka 2015 nchini China, baada ya kumaliza mbio za Kilomita 10 kwa upande wa wanaume kwa muda wa dakika 28 na sekunde 24.

Nafasi ya pili ilimwendea Mkenya mwingine Leonard Kiplimo Barsoton huku Abadi Hadis raia wa Ethiopia akifunga orodha ya tatu bora. Rais wa Uganda mwenye asili ya Kenya Joshua Kiprui Cheptegei alionekana katika nafasi nzuri ya kumaliza wa kwanza lakini akabanwa na misuli ambapo wanariadha wengine walipata fursa ya kumpiku. Onesphore Nzikwinkunda kutoka Burundi alimaliza katika nafasi ya 14, huku Mtanzania Gabriel Gerald Geay akimaliza katika nafasi ya 22. Kenya pia ilifanya vizuri kwa upande wa wanawake baada ya wanariadha wake kumaliza katika nafasi ya kwanza hadi ya sita. Irene Chepet Cheptai alishinda mbio hizo za Kilomita 10 kwa muda wa dakika 31 na sekunde 57 na kunyakua medali ya dhahabu.

Nafasi ya pili ilimwendea Alice Aprot Nawowuna huku Lilian Kasait Rengeruk akimaliza katika nafasi ya tatu.

Riadha; Kenya na Ethiopia zang'aa Korea Kusini

Kenya ilitikisa katika mbio za Seoul Marathon nchini Korea Kusini kupitia wakimbiaji Amos Kipruto na Margaret Agai, Jumapili. Kipruto aliongoza wanaume kutoka Kenya katika kunyakua nafasi 10 za kwanza. Kipruto alikimbia umbali wa kilomita 42 kwa kutumia saa 2:05:54 na kuibuka kidedea akifuatwa na Wakenya wengine Felix Kipchirchir (2:06:03) na Mark Korir (2:06:05). Agai alishinda kitengo cha wanawake kwa kutumia saa 2:25:52 akifuatwa na Muethiopia Ashete Bekere (2:25:57) na Mkenya Mercy Kibarus (2:26:52).

Shein apongeza uanachama wa Zanzibar CAF

RAIS wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amekipongeza Chama cha Soka Zanzibar ZFA kupata uanachama wa Shirikisho la Soka Afrika CAF na kuwataka mashabiki wa soka na viongozi waq mchezo huo kuacha tabia ya kupelekana mahakamani. Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari pamoja na wadau wa soka katika Ikulu ambao walifika kuadhimisha mwaka mmoja kuwepo madarakani baada ya kushinda uchaguzi wa marudio wa Machi 20 mwaka juzi, Shein alisema kitendo cha ZFA kupata uanachama kamili wa Caf ni fursa nyingine kuitangaza Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo utalii. Aidha, alisema hiyo ni fursa kwa vijana wanaochipukia katika soka kuimarisha vipaji vyao na kuweza kununuliwa katika timu mbalimbali, ikiwemo za nje na kwenda na dhana ya soka ni ajira. Zanzibar ilipata uanachama kamili wa Caf katika mkutano uliofanyika hivi karibuni mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo Ahmad Ahmad aliutwaa urais wa shirikisho hilo kwa kumshinda Issa Hayatou aliyekalia kiti hicho kwa miaka 29. Baada ya tangazo hilo, Mkurugenzi wa Shirikisho la Soka Tanzania TFF, Yusuf Sigo alisema kwa sasa wanalenga kuhakikisha kuwa Zanzibar inapewa uanachama wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA.

Rais Shein wa Zanzibar

Mwanzoni mwa mwaka 2000, Zanzibar ilipata uanachama wa muda wa Caf, ambapo iliruhusiwa kushirikisha klabu zake katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi ya Mabingwa.

……………………………………TAMATI……….………………

 

Tags