Apr 26, 2017 07:10 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (159)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutagazieni kutoka mjini Tehran. Hiki ni kipindi kipya katika mfululizo wa vipindi hivi vya itikadi ya Kiislamu, vya Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain hii ikiwa ni sehemu ya 159 katika mfululizo huo. Katika kipindi hiki tutaendelea kujibu swali lililoulizwa na msikilizaji wetu Bwana Said Ahmad wa mjini Tanga Tanzania ambalo tumekuwa tukilizungumzia tokea vipindi viwili vilivyopita.

Swali hilo linasema, je, ni nini kitakachotofautisha elimu ya Ahlul Beit wa Mtume Muhammad (saw) na elimu ya wanazuoni wengine waliojifunza au kunukuu sunna za Mtume (saw)? Tulipata kujua kutokana na maandiko ambayo yamenukuliwa na madhehebu zote mbili za Kiislamu yaani Shia na Suni na kadhalika ushahidi wa wanazuoni wa Ahlu Suna wal Jamaa kwamba tofauti ya kwanza iliyopo kati ya Maimamu wa Nyumba ya Mtume (as) na wanazuoni wengine wa kawaida ni kwamba Maimamu wanajua elimu yote ya Quráni Tukufu pamoja na siri na vilevile hakika zote zilizofichwa na kuhifadhiwa humo. Tofauti ya pili ni kuwa elimu yao imekingwa na makosa, dhana katika kufahamu uhalisi wa mambo, mghafala au makosa mengine yoyote yanayofanywa na binadamu wa kawaida.

Tofauti ya tatu ni kwamba kila mlango wa elimu ya Maimamu (as) hufunguliwa milango mingine elfu moja ya maarifa ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu aliwapa uwezo huo ili Uislamu uwe ni dini yake ya mwisho kwa jamii ya mwanadamu ambayo ina uwezo wa kujibu na kukidhi mahitaji yake yote katika kila zama na sehemu kutokana na elimu hii adhimu ambayo huwafungulia waja wake hao wema (as) kupitia milango ya maarifa ya yakini.

 

Wapenzi wasikilizaji, ama tofauti ya nne ya elimu ya Maimamu wa Nyumba ya Mtume (as) na elimu ya wanazuoni wengine wa kawaida ni kuwa elimu ya watukufu hao ndiyo iliyokamilika zaidi katika elimu ya Ladunni ambayo Mwenyezi Mungu huwapa waja wake wema kwa njia ya ilhamu. Jambo hili ni miongoni mwa mambo ya dharura kabisa kwao (as) kutokana na ukweli kwamba wao ndio makhalifa wa Mwenyezi Mungu kwenye ardhi yake na hoja Yake kwa waja Wake. Kwa msingi huo ni wazi kwamba ni lazima awape siri za elimu yake ya ghaiba katika kile wanachokihitaji katika kuwangoza waja wake kwenye njia nyoofu na ya saada ya humu duniani na ya huko Akhera kama tulivyoona katika vipindi vilivyopita na kama tutakavyoona katika maandiko mengine hivi punde.

Imam wetu Ja’ffar as-Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi akisema: ‘’Mwenyezi Mungu ni mkarimu, mrehemevu na mpole zaidi kwa waja wake kiasi kwamba hawezi kufaradhisha utiifu wa waja kwa mja wake na kisha kumnyima habari za mbinguni asubuhi na jioni.’’

Na katika kitabu hichohicho Imam Baqir (as) amenukuliwa akilalamikia watu wanaopinga upana wa elimu ya Imam kwa kusema: ‘’Je, mnaona kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alifaradhisha utiifu wa waja wake kwa mawalii wake na kisha kuwafichia (kutowapa) habari za mbinguni na ardhini na vilevile kutowapa misingi ya elimu anayowateremshia, misingi ambayo ndiyo inayobeba nguzo za dini yao?!’’

Na katika hadithi ya tatu Imam Swadiq (as) ananukuliwa akisema: ‘’Mwenyezi Mungu Mtukufu hatatolea hoja kwa viumbe wake jambo ambalo halitakuwa linajumuisha kila wanalolihitajia.’’

 

Na kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, kila jambo waliloneemeka nalo Maimamu watukufu (saw) katika elimu ya Ladunni kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa hakika ni mfano wa wazi wa rehema, upole na baraka zake kwa waja wake ambapo huwaandalia kupitia mawalii na makhalifa wake maasumu kila jambo wanalolihitajia katika elimu inayohusiana na hukumu na sheria zake kuhusu mambo mapya yanayojitokeza katika zama zao.

Na hadithi tukufu zinasema waziwazi kwamba jambo hilo hutimia kwa Maimamu kupewa ilhamu na kupuliziwa elimu kwenye vifua na nyoyo zao. Jambo hilo bila shaka halipingani na ukweli kwamba Mtume Muhammad (saw) ndiye Mtume wa Mwisho. Hii ni kwa sababu ilhamu ya Mwenyezi Mungu kwa Maimamu (as) na kupuliza elimu kwenye nyoyo zao ni katika daraja za juu za wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake kama inavyoashiria Quiráni Tukufu kuhusiana na wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa nyuki katika kiwango cha chini zaidi na vilevile kwa mama yake Nabii Musa (as) aliyezungumza na Mwenyezi Mungu.

Imam Musa Kadhim (as) anaashiria maana hii katika hadithi iliyopokelewa katika kitabu cha Al-Kafi na vitabu vinginevyo vya kuaminika kwa kusema: ‘’Upeo wa elimu yetu ni wa aina tatu: Kuhusu yaliyopita, yaliyopo hivi sasa na yanayokuja.’ Kisha Imam (as) alibainisha aina hizi tatu za elimu ya Maimamu (as) kwa kusema: ‘’Ama elimu ya yaliyopita imefasiriwa.’’ Katika hilo kuna ishara ya kutekelezwa milango ya elimu ambayo waliirithi Maimamu (as) kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) katika zama zao maalumu, kama inavyoashiria hilo hadithi mashuhuri ya Imam Ali (as) inayosema: ‘’Mtume wa Mwenyezi Mungu alinifundisha milango elfu moja ya elimu ambapo katika kila mlango ilifunguliwa milango mingine elfu moja ya elimu.’’

Kisha Imam Kadhim (as) akasema: ‘’Ama elimu ya hivi sasa imeandikwa.’’ Suala hili linaashiria sahifa ambayo Mtume Mtukufu (saw) alikuwa akitamka mameneo fulani naye huku Imam Ali (as) akiyaandika kwenye sahifa hiyo kwa mkono wake. Sahifa hiyo ilikuwa ikirithiwa kati ya Maimamu na inavyoonekana katika hadithi nyingine ni kuwa sahila hiyo ilikuwa na mambo ambayo Maimamu hao 12 walitakiwa kuyatekeleza katika zama zao tofauti za uongozi, yaani majukumu yao maalumu kwa ajili ya kulinda dini ya haki.

Kisha Imam Kadhim (as) alisema: ‘’Ama elimu mpya inayohusiana na mambo yatakayotokea ni ile inayopulizwa kwenye nyoyo na kwenye masikio, nayo ndiyo elimu yetu bora zaidi na hakuna Nabii mwingine baada ya Nabii wetu.’’

Na aina hii ya elimu ndiyo elimu ya Ladunni inayotolewa na Mwenyezi Mungu kwa waja wake wema kwa njia ya ilhamu na ambayo huwakidhia waja mahitaji yao yote wanayotaka kuyajua kutoka mbinguni na ardhini, katika yale mambo ambayo hayapatikani kwa njia ya elimu ya kurithiwa au kuandikwa.

 

Na kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni kama kawaida kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo pamanapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.