May 15, 2017 07:54 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Mei 15

Huu ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Iran yatwaa taji la Mieleka barani Asia 2017

Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya Asian Senior Wrestling Championships nchini India. Wanamieleka hao wa Kiirani wameibuka kidedea baada ya kutwaa jumla ya medali 7 zikiwemo 4 za dhahabu katika mashindano hayo ya kieneo na kunyakua pointi 71 katika mtinfo wa Free Style.

Mwanamieleka wa Iran akipambana na hasimu huku New Delhi

Katika pambano la mwisho siku ya Alkhamisi, Muirani Hossein Ahmad Nouri aliimpeleka mchakamchaka Mjapani Atsushi Matsumoto katika kategoria ya kilo 85 na kutwaa medali ya dhahabu. Dhabu zingine za Iran zilitwaliwa na Ramin Soltanmorad kitengo cha kilo 80, Mostafa Seyyedghanbar Salehizadeh safu ya kilo 98 na Behnam Aliakbar Mehdizadeh katika kitengo cha kilo 130. Timu ya Iran ya mieleka mtindo wa Greco-Roman ya wanaume ilitawazwa mabingwa baada ya kuzoa alama 69, ikifuatiwa na Kazakhstan na Korea Kusini ambazo kwa pamoja zilivuna alama 59 katika mashindano hayo yaliyofanyika katika mji wa New Delhi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei ameongoza maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini kutuma salamu za pongeza kwa mabingwa hao wa Kiirani kwa kung'ara katika mashindano hayo ya kieneo ya India, yaliyoanza Me1 10 na kufunga pazia lake Mei 14.

Iran yazoa medali kochokocho Michezo ya Mshikamano wa Uislamu

Wanamichezo wa Iran wamezoa medali kochokocho katika duru ya 4 ya mashindano ya Michezo ya Mshikamano wa Uislamu inayofanyika Azerbaijan. Hadi kufikia sasa Wairani wamezoa jumla ya medali 8 katika mashindano hayo yanayofanyika katika mji mkuu wa Azerbaijan, Baku. Siku ya Jumamosi, walengaji shabaha wa Iran, Narjes Emamgholinejad na Elaheh Ahmadi walishinda medali mbili kwa mpigo ikiwemo ya dhahabu katika kitengo cha wanawake kupiga shabaha mita 10.

Aidha makarateka wa Kiirani wa kike na kiume wamejishindia medali nne hadi sasa huku Nasrin Dousti akiipa Iran ya Kiislamu dhahabu nyingine katika mchezo wa kunyanyua vitu vizito safu ya wanawake kategoria ya kilo zisizozidi 50. Katika siku ya kwanza ya mashindano hayo, timu ya voliboli ya wanaume ya Iran iliidhaliisha Saudi Arabia kwa seti ya moja kwa moja ya 25-18, 25-23 and 25-18 katika mchezo wa Kundi B katika ukumbi wa Crystal mjini Baku. Wanariadha na wanamichezo kutoka nchi 54 za Kiislamu kutoka kila pembe ya dunia wanashiriki mashindano hayo yaliyoanza Mei 12 na yanatazamiwa kumalizika Mei 22, chini ya kaulimbiu "Mshikamano Wetu, Umoja wa Wetu".

Majudoka wa Iran wazoa medali 3 mashindano ya IJF, Uzbekistan

Mabingwa wa mchezo wa judo wa Iran wametia kibindoni medali 3 zikiwemo 2 za dhahabu katika Mashindano ya Dunia ya Vijana ya mchezo huo huko Uzbekistan. Katika siku ya kwanza ya mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Judo Duninai IJF Alkhamisi, mjini Chirchik, yapata kilomita 32 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Tashkent, mwanajudo Hamidreza Malekzadeh aliipa Iran medali ya dhahabu katika safu ya kilo 100, baada ya kuwaelemea majudoka wa Marekani na Uzbekistan. Ali Parhizkar aliipa Iran medali ya fedha katika kitengo cha kilo 100 baada ya kumuadhibu mwenyeji. Awali Soheil Jamalabadi aliipa Iran medali nyingine ya dhahabu katika safu ya kilo 55. Zaidi ya majudoka 156 kutoka nchi 10 duniani walishiriki mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama International Judo Federation (IJF) Junior World Tour yaliyoanza Mei 11 na kufunga pazia lake siku ya pili. 

Mashindano ya Kikanda Tanzania, wenyeji na Kenya wang'ara

Wanariadha wa Tanzania wamefanya vyema katika mashindano ya kimataifa ya riadha kanda ya tano ya wanariadaha wenye chini ya miaka 18 yaliyofanyika nchini katika mji mkuu Dar es Salaam. Mwanariadha Rose Seif ameweka rekodi mpya katika mashindano ya Afrika ya Kanda ya Tano kwa vijana baada ya kuibuka na medali mbili za dhahabu. Rose ameshinda medali hizo katika mbio za mita 400 na mchezo wa mruko wa chini (long jump) juzi na jana kwenye fainali zilizofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sehemu ya mashindano ya Kanda ya Tano, Dar, Tz

Matokeo hayo ya Rose yanafanya Tanzania kufikisha medali sita za dhahabu za mbio hizo zilizofungwa jana jioni na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Muhammed Kiganja. Mzanzibar Daud Dahasheghe aliibuka kinara katika mchezo wa kurusha mkuki, akirusha umbali wa mita 49 na sentimita 68. Tanzania imetwaa medali zaidi ya 10, dhahabu zikiwa sita, fedha nne na shaba mbili huku Kenya ikiwa imetwaa medali saba, dhahabu zikiwa tano, fedha moja na shaba moja. Wnariadha hao chipukizi wa Tanzania kutamalaki mashindano hayo kumewapa moyo wa taifa hilo kuipuka Kenya katika mashindano ya kimataifa ya riadha katika siku za usoni. Kauli zinazotiliwa pondo na Wilherm Gidabudal, Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania.

Mbali na Kenya na Tanzania, mashindano hayo ya kikanda yameshirikisha wanariadha kutoka Eritrea, Sudan na Sudan Kusini.

Sitaki mshahara wa CAF kwa sasa, asema Ahmed Ahmed

Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika CAF, Ahmed Ahmed ametangaza kutokubali kupokea mshahara kutoka shirikisho hilo hadi pale mambo yote yatakapokuwa yamewekwa wazi. Raia huyo wa Madagascar mwenye umri wa miaka 57 alisimamia mkutano wake mkuu katika shirikisho hilo siku ya Jumatatu kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani Fifa siku ya Alhamisi.

Ahmed Ahmed, Mkuu wa CAF

Ahmed amesema kama tunavyomnukuu: "Mabadiliko kuhusu usimamizi ni swala muhimu sana. Kila mtu anapaswa kujua kinachotendeka.''  Uchaguzi wa Ahmed katika uongozi wa CAF mnamo mwezi Machi ulimaliza uongozi wa miaka 29 wa aliyekuwa rais wa shirikisho hilo kutoka Cameroon Issa Hayatou.

Chelsea yatwaa Ligi ya EPL

Klabu ya Chelsea imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Uingereza almarufu EPL baada ya kuichachafya West Brom bao 1-0 licha ya vijana wa Albion kuupigia nyumbani katika uwanja wa The Hawthorns siku ya Ijumaa. Bao hilo la pekee na la ushinda lilipachiwa kimyani na mtoka benchi Michy Batshuayi kunako dakika ya 82.

Chelsea walipotwaa ubingwa huko nyuma

Kwa kutwaa ushindi huo, Chelsea chini Antonio Conte imeweka rekodi ya kuwa klabu ya pili kutwaa ubingwa wa EPL mara nyingi ambapo imetwaa mata tano nyuma ya Manchester United iliyotwaa mara 13. Chelsea yenye alama 87 imeweka pia rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa wa EPL siku ya Ijumaa tangu Arsenal ilipofanya hivyo katika uwanja wa Anfield 1989 huku Antonio Conte akiwa meneja wa nne kutoka Italia kushinda taji hilo baada ya Ancelotti, Roberto Mancini na Claudio Ranieri. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameonekana kukerwa na ushindi huo wa The Blues licha ya kuwa katika nafasi ya sita kwenye viwango vya soka barani Ulaya. Ifahamike kuwa, kwa takribani misimu miwili, timu ambazo hazina kiwango cha ubora ndizo zinazotwaa mataji ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Premier.

Na nikudokeza kwamba, mabingwa mara 11 wa taji la klabu bingwa barani Ulaya UEFA, Real Madrid ya Uhispania, itamenyana na mabingwa mara mbili Juventus ya Italia kuwania taji la msimu huu. Mechi hiyo ya fainali inayotazamiwa kuwa kukata na shoka itachezwa tarehe 3 mwezi Juni katika uwanja wa Millennium mjini Cardiff nchini Uingereza.

……………………….TAMATI………………….

 

Tags