May 24, 2017 18:19 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (162)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Kuanzia kipindi cha juma hili tutakuwa tukijibu maswali yanayohusiana na Ufufuo au kwa jina jingine Maad ambayo ni maudhui nyingine katika misingi ya imani ya Kiislamu.

Swali ambalo tutaliwasilisha kwa Vitu Viwili Vizito ambavyo tuliachiwa na Bwana Mtume (saw) ili vipate kutuongoza kwenye njia nyoofu na hivyo kutopotea njia sahihi tunayotakiwa kuifuata na Mwenyezi Mungu ni hili kuwa, je, imani ya Maad au Ufufuo ina umuhimu gani katika maisha ya mwanadamu?

Hili bila shaka ni swali muhimu sana ambalo ufafanuzi wake utamchochea mtu anayejua jibu lake kufanya juhudi za kufuatilia undani wake ili apate kunufaika na matunda yake. Hivyo basi kuweni makini ili tutafute kwa pamoja jibu la swali hili muhimu la kiitikadi?

********

Kwanza kabisa mpenzi msikilizaji tunarejea kwenye Kizito cha Kwanza yaani Quráni Tukufu ambapo tunashangazwa  na wingi wa aya za kitabu hicho kitakatifu zinazozungumzia imani ya Ufufuo, masuala yanayohusiana na maisha ya Akhera, ufafanuzi wa Kiama, hesabu, malipo na maisha ya milele ima katika Pepo au motoni na mfano wa hayo. Sheikh Abdul Jawad al-Ibrahimi anasema katika kitabu chake alichokipa jina la Nadharutun Haula Durusin Fi al-Aqidatil Islamiyya kwamba kuna aya elfu mbili katika kitabu hicho cha mbinguni zinazozungumzia suala zima la Maad. Hii ina maana kwamba karibu thuluthi moja ya aya za kitabu hicho kitakatifu inazungumzia suala hilo. Bila shaka jambo hilo lina maana kuwa Mwenyezi Mungu ametenga sehemu kubwa ya Quráni Tukufu kuwabainishia waja wake suala zima la imani ya Maad na Siku ya Mwisho ambapo sote, wasikilizaji wapendwa, tunajua kwamba Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima na kuwa maneno yake ni muhimu mno ambayo wanadamu wanayahitaji kwa ajili ya kufikia saada yao ya humu duniani na huko Akhera. Na lengo la hekima hiyo ni kulipa kila jambo umuhimu linaoustahiki. Kwa msingi huo ni wazi kuwa upana na ukubwa uliopewa jambo hilo na Mwenyezi Mungu katika ufafanuzi wake wa imani ya Maad bila shaka unaashiria umuhimu wa kufahamika maudhui hiyo mbele ya waja wake ili wapate kujidhaminia maslahi yao. Jambo ambalo limebainika kiitika ni kuwa Mwenyezi Mungu hawahitajii waja wake katika jambo lolote lile na kwamba kila analowabainishia na kuwawekea wazi ni kwa maslahi na manufaa yao wenyewe. Kwa msingi huo, kila mara kitabu chake kitakatifu kinaposisitiza na kuzingatia zaidi jambo fulani bila shaka hilo hutokana na umuhimu mkubwa wa jambo hilo katika kuthibitisha lile analolitaka Mwenyezi Mungu katika kuwafikishia waja wake manufaa na kuwakinga na shari.

Ukweli huu unatosha kutufanya tudiriki kwa ujumla umuhimu wa kujifunza na kujua undani wa itikadi au imani ya Maad Na Siku ya Mwisho kutokana na umuhimu wake katika kutufikisha kwenye heri ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake. Kuna nukta nyingine muhimu ambayo tunaipata katika Quráni Tukufu ambayo inatusaidia kujibu swali la kipindi hiki, ambapo tutaijadili kwa urefu kidogo hivi punde, hivyo endeleeni kuwa pamoja nasi.

Image Caption

 

Ndugu wasikilizaji, kama tunavyoona katika kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, utajo wa imani ya Mwenyezi Mungu umefungamanishwa katika aya nyingi za Quráni na imani ya Maad, jambo ambalo bila shaka linaenedelea kusisitiza umuhimu wa maudhui hii. Kwa mfano, Quráni Tukufu imetumia ibara ya ‘’imani ya Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiama’’ katika zaidi ya aya ishirini. Katika hilo kuna ishara muhimu kwamba itikadi ya Maad inafungamana moja kwa moja na itikadi ya Tauhidi au inakamilisha imani juu ya Mwenyezi Mungu.

Hii ina maana kwamba umuhimu wa imani juu ya Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kunatokana na imani juu ya Maad na maisha ya Akhera. Imani mbili hizi ndizo zinazobuni nguzo mbili za Tauhidi, nguzo ambazo kwa pamoja zinamdhaminia mumini matunda yanayohitajika na kutarajiwa kutokana na kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba baadhi ya aya tukufu zimetumia neno ‘kutarajia’ kuhusiana na Mwenyezi Mungu na vilevile na Siku ya Mwisho. Kwa mfano, Mwenyezi Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 21 ya Surat al-Ahzab:

  لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّهَ وَالْيَوْمَ الآخِرَ وَذَكَرَ اللَّهَ كَثِيرًا

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi.

Kama mnavyoshuhudia wapenzi wasikilizaji, ibara iliyotumika hapa sio imani juu ya Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho bali ni kuzitarajia zote mbili yaani ni matunda yanayotokana na imani juu ya Mwenyezi Mungu na Maad kwa pamoja. Yaani matunda hayo yanatarajiwa kutoka kwa imani juu ya nguzo hizo mbili.

**********

Wapenzi wasikilizaji, natija hii tuliyoipata katika Kizito cha Kwanza imeakisiwa kwa mapana na uwazi mkubwa katika Kizito cha Pili. Inatosha kuashiria hapa kwamba baadhi ya hadithi zinazozungumzia imani ya Maad zimekusanywa na Allama al-Majlisi katika juzuu nne za kitabu chake cha al-Bihar. Pamoja na hayo kuna hadithi nyingine ambazo zinazungumzia suala hili ambazo hazijaandikwa na Allama katika kitabu chake hicho. Kwa vyovyote vile suala hili linaashiria umuhimu mkubwa ambao Mtume Mtukufu (saw) na kizazi chake kitoharifu (as) walilipa jambo hilo katika kuimarisha imani juu ya Maad na Siku ya Mwisho katika nyoyo za watu. Ni watukufu hao hao (as) ndio wanaochelea na kushughulishwa zaidi na maslahi ya waja na heri yao. Hivyo, sisitizo lao la kujuza na kuwafundisha watu hakika juu ya itikadi ya Maad na ufafanuzi wake bila shaka linatokana na hamu yao kubwa ya kutaka kuwasaidia waja hao kufikia mambo ambayo yana maslahi kwao kama tulivyoona kuhusiana na aya za Quráni.

 

Kutokana na yale tuliyojifunza kwenye kipindi cha juma hili, muhtasari ni kuwa umuhimu wa imani juu ya Maad unerejea kwenye muhimili wa imani hii kama njia ya kuwafikishia watu heri. Hivyo basi je, baraka muhimu zaidi inayotokana na imani juu ya imani hii ni gani?

Hili ndilo swali tutakalolijadili kwa pamoja katika kipindi chetu kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain Inshallah. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi. Basi hadi wakati huo, kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, hatuna la ziada ila kukuageni nyote wapenzi wasikilizaji tukikutakieni kila la heri katika kila jema mnalolifanya. Kwaherini.