Sep 04, 2017 06:20 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Sep 4

Huu ni mkusayiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita.....

Soka: Iran yailazimisha Korea Kusini 0-0

Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeilazimisha Korea Kusini sare tasa katika mchezo wa kusaka tiketi ya Kombe la Dunia mwaka ujao 2018 nchini Russia. Katika mchuano huo wa aina yake uliopigwa katika Uwanja wa Kombe la Dunia wa Seoul, wenyeji Korea walishindwa kutuliza mpira licha ya kuchezea nyumbani mbele ya mashabiki zaidi ya 60 elfu, na hivyo, wamejikosesha tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani. Msemo usemao mcheza kwao hutuzwa ulikosa maana kabisa ikizingatiwa kura sehemu kubwa ya kipindi cha pili, Iran ilicheza ikiwa na wachezaji 10 baada ya kiungo wake Saeid Ezatolahi kupigwa kadi nyekundu baada ya kumchezea visivyo Kim Min-Jae. Timu hizo zilishindwa kuona lango la mwingine katika kipindi cha kwanza licha ya majaribio kadhaa ya hapa na pale. Iran inatazamiwa kuvaana na Syria Jumanne hii katika mchuano wa Kundi A na kwa kuwa tayari ishajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia, mchuano huu utatoa mwangaza wa kubaini iwapo Syria itaanza kujindaa kuelekea Russia kwa Kombe la Dunia mwakani au la.

Kombe la Dunia mwakani nchini Russia

Katika mechi nyingine za kusaka tiketi ya Kombe la Dunia, Wales iliitandika Austria bao 1-0, Uingereza ikaigeuza Malta kichwa cha mwendawazimu kwa kuisaga mabao 4-0; Ujerumani ikiichabanga Jamhuri ya Czech mabao 2-1 wakati ambapo Syria ilikuwa ikiisasambua Qatar mabao 3-1 huku Uhispania ikiifunza soka Italia kwa kuifunga mabao 3-0. Ureno iliiadhibu Hungary bao 1-0 wakati ambapo Uholanzi ilikuwa ikinyolewa kwa kuchupa kwa kulimwa mabao 4-0 na Ufaransa. Mbali na Iran na mwenyeji Russia, timu nyingine zilizofuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia mwakani na Brazil, Japan, Mexico na Ubelgiji na kwa masikitiko hamna hata timu moja ya Afrika yenye tiketi mfukoni ya kushiriki mashindano hayo. Hata hivyo Uganda, Algeria, Ghana, Nigeria na Afrika Kusini ni miongoni mwa timu za bara hilo ambazo zipo mbioni kusaka tiketi na wengi wana matumaini nazo.

Iran yaweka rekodi mpya katika mechi za kimataifa za soka

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeandika ujumbe katika mtandao wake rasmi wa kijamii wa Twitter likieleza kustaajabishwa na matokeo ya mechi za timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Iran katika mechi za mchujo za kuwania nafasi ya kucheza kwenye Kombe la Dunia mwakani nchini Russia. Ujumbe wa FIFA umesema kuwa: Timu ya Taifa ya soka ya Iran imecheza dakika 1063 katika mashindano hayo bila ya kufungwa hata goli moja.  Katika mechi tisa zilizotangulia timu ya taifa ya soka ya Iran ilifunga mechi 6 na kutoka sare mechi tatu ambapo imefunga magoli 8 na kupata pointi 21. Kombe la Dunia litaanza kuroroma Juni 14 hadi Julai 15 mwaka ujao wa 2018 nchini Russia. 

Soka: Uganda yang'ara

Tukiwa bado katika pumzi hiyo ya Kombe la Dunia, timu ya taifa ya soka ya Uganda yumkini ikawa timu ya kwanza kutoka kanda ya Afrika ya Mashariki kushiriki mashindano hayo ya kimataifa ya mpira wa miguu, tangu yaasisiwe mwaka 1930. Hii ni baada ya kuizaba Misri bao 1-0 jijini Kampala siku ya Alhamisi na kukwea kileleni mwa Kundi E. Hii ni mara ya kwanza kabisa Uganda imepata ushindi dhidi ya Mafarao wa Misri tangu walipochuana mara ya kwanza mwaka 1962. Uganda ilikuwa imepoteza mechi tisa mfululizo dhidi ya Misri kabla ya bao la Emmanuel Okwi la dakika ya 51 kuipa Uganda Cranes ushindi huo wa kihistoria. Uganda imejiweka katika mazingira mazuri ya kutinga Kombe la Dunia hususan iwapo itapata ushindi katika mchuano wa marudiano mjini Alexandria. Ieleweke kuwa, Uganda ipo katika nafasi 73 kwenye orodha ya FIFA huku Misri ikiwa nambari 25.

Kenya yashikilia taji la EAC, soka ya wanajeshi

Klabu ya Ulinzi Stars ya Kenya imetetea ubingwa wake katika mashindano ya mpira wa miguu ya majeshi ya kanda ya Afrika Mashariki. Hii baada ya kuifyatulia Tanzania risasi 1 bila jibu katika mchuano wa finali uliopigwa Jumapili katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura.

Wachezaji wa Ulinzi Stars wakipambana na Tanzania

 

Bao la kipekee na la ushindi la Kenya lilifungwa na Boniface Onyango katika kipindi cha kwanza. Vijana hao wa mkufunzi Benjamin Nyangweso walianza kampeni zao za kusaka ubingwa kwa kuifunga Burundi bao 1-0 na kulazimishwa sare ya 1-1 na Uganda katika mchuano wao wa pili. Baada ya kuhifadhi taji hilo, jitihada za wanajeshi hao wa Kenya zitaelekezwa katika Ligi Kuu ya Soka katika nchi yao, ambapo kufikia sasa wamekusanya pointi 32 katika mechi 20 za kwanza walizocheza katika ligi hiyo.

Tanzania yaikata ngebe Botswana

Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars imeidhalilisha Botswana kwa kuigaragaza mabao 2-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa Jumamosi ya Septemba 2 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Mabao mawili kutoka kwa wing'a wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika klabu ya Difaa Hassan al-Jadida ya Morocco, Simon Msuva yalitosha kuwapaisha vijana wa Taifa wakiupiga nyumbani. Msuva aliyejiunga na timu ya Ligi Kuu ya Morocco mwezi uliopita alicheka na nyavu dakika tano tu baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza mechi na kusajili bao la kwanza la Taifa Stars. Kipindi cha pili, Zebras walirudi kwa kasi ya juu na kuanza kufanya mashambulizi mfululizo dhidi ya Taifa Stars, lakini safu ya ulinzi ikiongozwa na kiungo mkongwe Kevin Yondan ilikuwa imara kudhibiti hatari zote.

Msuva na wenzake wakishangilia goli

 

Hatimaye Msuva akawainua tena vitini mashabiki wa nyumbani kwa kufunga bao la pili kunako dakika ya 63 baada ya kucheza nipa nikupe na Ramadhani Kichuya. Ushindi huo utaiwezesha Tanzania ambayo ipo nafasi ya 120 katika viwango vya FIFA izidi kupanda. Vijana wa Taifa Stars mara ya mwisho walivaana na Pundamilia wa Botswana katika Uwanja wa Taifa wa Dar mwezi Machi mwaka huu na kuwacharaza magoli 2-0, yaliyofungwa na Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anasakata kabumbu ya kulipwa kule Ubelgiji.

………………………TAMATI………………….

 

Tags