Apr 16, 2018 06:26 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Apr 16

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita..

Wanataekwondo wa Iran watawala Junior Championships Tunisia

Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetamalaki Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Taekwondo nchini Tunisia baada ya kutwaa medali kochokocho. Wanataekwondo hao wa Kiirani wameibuka kidedea baada ya kutwaa medali saba za dhahabu na mbili za fedha kwa upande wa wanaume. Kadhalika Vahid Abdollahi, raia wa Iran ametajwa kama mkufunzi bora wa mashindano hayo yajulikanayo kwa Kiingereza kama World Taekwondo Junior Championships yaliyopigwa mjini Hammamet. Russia imeibuka ya kwanza kwa upande wa akina dada huku kocha wake Andrey Ananchenko akitwaa taji la kocha bora kwa upande wa wanawake. Zaidi ya wanataekwondo elfu moja kutoka nchi 118 dunia wameshiriki mashindano hayo ya kimataifa. Iran sasa inajiandaa kushiriki mashindano mengine kama haya ya dunia ya taekwondo kwa upande wa vijana nchini Bulgari 2020.

Iran yazoa medali 3 katika mashindano ya Judo

Wanamichezo wa judo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali tatu katika mashindano ya kikanda ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Uzbekistan. Wanajudoka wa Iran walionyesha ustadi na ufundi wa hali ya juu katika mashindano hayo ya kuwania Kombe la Asia kwa upande wa wachezaji wa judo mabarobaro. Muirani Abolfazl Shojaei ameibuka wa pili na kutuzwa medali ya fedha katika fainali ya wanajudoka wenye kilo zisizozidi 90.

Timu ya Judo ya Iran

 

Reza Azizi na Maral Mardani waliipa Iran medali za shaba kila mmoja katika safu za wanajudoka wenye kilo 90 na 60 kwa utaratibu huo. Mashindano hayo yanayofahamika kwa Kimombo kama Junior Asian Judo Cup yalianza Aprili 11 na kufunga pazia lake Aprili 15 katika mji mkuu wa Uzbekistan, Tashkent, kwa kuwaleta pamoja wanajudoka 255 kutoka nchi 10 za bara Asia.

Michezo ya Jumuiya ya Madola

Michezo ya Jumuiya ya Madola imefunga pazia lake siku ya Jumapili mjini Gold Coast nchini Australia huku mwenyeji akiupa maana msemo usemao, mcheza kwao hutuzwa. Wenyeji wamemaliza wa kwanza kwa kupata medali 198, zikiwemo 80 za dhahabu, 59 za fedha na 59 za shaba. Uingereza imemaliza ya pili kwa medali 136, huku India ikifunga orodha ya tatu bora kwa kuzoa jumla ya medali 66. Afrika Kusini imamaliza katika nafasi ya sita duniani, ikiwa ya kwanza Afrika kwa kutia kibindoni medali 37, ikifuatwa na Nigeria ambayo imeshikilia nafasi ya tisa kwa kutwaa medali 24. Kenya imemaliza ya 14 duniani na ya tatu barani Afrika kwa medali 17, zikiwemo nne za dhahabu huku Uganda ikimaliza katika nafasi ya 15 duniani kwa medali sita, zikiwemo tatu za dhahabu. Wanariadha kutoka Kenya wameshindwa kupata medali katika siku hiyo ya mwisho kwa upande wa wanaume, lakini raia wa Uganda Munyo Solomom Mutai imeipa Afrika Mashariki medali ya fedha kwa kuibuka wa pili nyuma ya mwenyeji Michael Shelley wa Australia. Mganda huyo mwenye asili ya Kenya anasema ameridhishwa na matokeo hayo, lakini atakaza buti katika siku za usoni.

Mbali na riadha, timu ya taifa ya wanaume ya Australia imeshinda dhahabu katika mpira wa Kikapu huku New Zeland ikishinda dhahabu katika mchezo wa raga kwa wachezaji saba kila upande.

Walinda usalama mjini Gold Coast

 

Baada ya ngoja ngoja, hatimaye wanariadha wa Kenya walianza kutamalaki mbio za masafa marefu na za kadri katika mashindao hayo siku ya Alkhamisi. Kenya ilijipatia dhahabu ya kwanza kwenye michezo hiyo baada ya mwanariadha chipukizi Wyclif Kinyamal kumaliza wa kwanza katika mbio za mita 800 na kumbwaga mtimkaji mzoefu wa Botswana Nijel Amos.

Nchi hiyo ilishinda mbio za Mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa upande wa wanaume katika mashindano hayo ya Jumuiya ya Madola. Bingwa wa Olimpiki katika mbio hizo Conseslus Kipruto, aliwaongoza wenzake wawili kunyakua medali ya dhahabu, fedha na shaba. Kipruto aliibuka mshindi kwa muda wa dakika 8 sekunde 10 nukta 08 akifuatwa na Abraham Kibiwott na Amos Kirui.

Baada ya ushindi huo, Kipruto amesema alitaka Wakenya wenzake kuchukua nafasi ya pili na ya tatu na hivyo aliendelea kuwahimiza.

Dhahabu zingine za Kenya zilitwaliwa na Elijah Manang’oi na Hellen Obiri katika mbio za mita 1,500 na 5,000 kwa usanjari huo kwa upande wa wanaume na wanawake. Hata hivyo Kenya ilikosa medali ya dhababu katika mbio za Mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa upande wa wanawake, baada ya Mjamaica Aisha Praught kumaliza wa kwanza kwa muda wa dakika 9 na sekunde 21. Mkenya Celliphine Chepteek Chespol alimaliza wa pili kwa muda wa dakika 9 na sekunde 22, huku Mkenya mwingine Purity Cherotich akimaliza kwenye nafasi ya tatu. Mwakilishi mwengine wa kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania ambayo imewahi kutwaa medali 21 tangu ianze kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1966, haijang'ara katika mashindano hayo ya dunia yam waka huu.

Huku hayo yakirifiwa, Wanariadha 13 wa Afrika walioenda kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia wameripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha. David Grevemberg, Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola aliwaambia waandishi wa habari siku ya Alkhamisi mjini Gold Coast kuwa: "Wanariadha wengine watano raia wa Rwanda, Uganda na Sierra Leone wametoweka na kwenda kusikojulikana." Ameongeza kuwa, hii ni baada ya wanariadha wengine wanane kutoka Cameroon kutoweka hapo awali, na sasa idadi hiyo ya wanaichezo wa Kiafrika waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha nchini humo imefikia 13. Serikali ya Australia imetoa viza kwa wanamichezo wanaoshiriki katika michezo hiyo, kuendelea kuwa nchini humo hadi tarehe 15 mwezi Mei. 

Wakimbizi nchini Australia

 

Peter Dutton, Waziri wa Masuala ya Ndani ya Australia ameonya kuwa, mwanariadha yeyote atakayebaki nchini humo kinyume cha sheria baada ya muda wake wa viza kumalizika, atafurushwa nchini humo kwa nguvu.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2000 wakati wa mashindano mengine ya Jumuiya ya Madola jijini Sydney, wanaridha zaidi ya 100 waliendelea kuishi katika jiji hilo hata baada ya kumalizika kwa michezo hiyo. Michezo ijayo ya Jumuiya ya Madola itafanyika mwaka 2022 jijini Birmingham nchini Uingereza.

Man City yatwaa EPL kwa mara ya 5

Hatimaye klabu ya Manchester City imetangazwa bingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza kwa mara ya tano sasa, baada ya watani wao wa jadi ambao wapo katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL, klabu ya Manchester United kupoteza mchuano muhimu wakiwa nyumbani wikendi. Mashetani Wekundu walizabwa bao moja la uchungu bila jibu na West Brom katika kitimutimu hicho kilichosakatwa ugani Old Trafford. Bao la kipekee na ulishindi la vijana wa Albion lilifungwa na Rodriguez kunako dakika ya 70.

Man City waliposhinda Kombe la Carabao

 

City wametangazwa kuwa mabingwa kwa kuwa na jumla ya point 87 na wamesalia na michezo mitano. Man City mara ya mwisho kutwaa taji la EPL ilikuwa mwaka 2014. Vijana wa Man City ambao wao siku ya Jumamosi ya April 14 walishuka dimbani kuvaana na Tottenham, walipata ushindi wa aina yake wa magoli 3-1. Mabao ya City katika Uwanja wa Wimbley yalifungwa na Gabriel Jesus, Gundogan aliyefunga penati, na Sterling aliyepachika wavuni bao la mwisho kunako dakika ya 72. City wametangazwa mabingwa kwani hata Man U ikishinda mechi zake zote na City ipoteze mechi zote zilizosalia, Mashetani Wekundu watakuwa na pointi 86, na haiyumkini hata kwa ndumba kufikia alama 87 ilizonazo Man City.

Kwengineko Newcastle imeinyuka Arsenal mabao 2-1 katika mechi nyingine ya Ligi Kuu ya Soka Uingereza huku jinamizi la rekodi mbaya kwa Arsenal msimu huu likiendelea kuiandama timu hiyo ya Arsene Wenger.

Nusu fainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya

Baada ya kumalizika kwa mechi za robo fainali za michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya almaarufu UEFA Champions League, Shirikisho la Soka Ulaya UEFA lilichezesha droo ya kupanga mechi za nusu fainali ya michuano hiyo. Liverpool, Bayern Munich, Roma na Real Madrid zimefuzu katika hatua ya nusu fainali kuwania taji la klabu bingwa barani Ulaya. Licha ya kutofungana, Bayern Munich ilifanikiwa kufika katika hatua hiyo jana usiku kwa jumla dhidi ya Sevilla ya Uhispania. Nayo Real Madrid ilipata ushindi mwembamba wa jumla ya mabap 4-3 dhidi ya Juventus ya Italiana kusonge mbele. AS Roma wakiwa nyumbani wameushangaza ulimwengu baada ya kupindua matokeo na kuitoa FC Barcelona katika hatua ya robo fainali ya UEFA Champions League, mchezo wa kwanza wa Roma dhidi ya Barcelona uliyochezwa Nou Camp ulimalizika kwa Barcelona kupata ushindi magoli 4-1, hivyo Roma kupata ushindi wa magoli 3-0 leo kumewafanya wafuzu hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa jumla ya magoli 4-4 ila goli la ugenini ndio linawabeba.

Magoli ya AS Roma katika ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya Barcelona yalifungwa na Eden Dzeko dakikaya 6, Daniele De Rossi aliyefunga goli dakika ya 58 kwa mkwaju wa penati na goli la mwisho likafungwa na Kostantinos Manolas dakika ya 82, AS Roma wanafanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza toka msimu wa 1983/1984 waliposhiriki kwa mara ya mwisho.

………………………..TAMATI………………….

 

 

Tags