Jun 03, 2018 14:59 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 35 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tuliashiria ongezeko la kutisha la chuki na ubaguzi dhidi ya dini ya Kiislamu na wafuasi wa dini hii nchini Austria kiasi kwamba hata watoto wa Kiislamu wanaozaliwa nchini humo, hutuhumiwa kuwa ni magaidi wapya waliozaliwa, kitendo ambacho kinayaweka hatarini maisha ya watu hao.

Rais Donald Trump wa Marekani

Ndugu wasikilizaji kuhusu kipindi cha utawala wa mwaka mmoja wa Rais Donald Trump wa Marekani, gazeti la The Independent la nchini Uingereza liliandika kwamba, tangu alipooingia madarakani mtawala huyo, alianzisha kampeni yake ya kueneza chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu, suala ambalo lilichangia kuongezeka mara tatu zaidi chuki dhidi ya Uislamu nchini humo. Katika ripoti hiyo, gazeti hilo liliandika: "Kando na kampeni za uchaguzi nchini Marekani ambapo Trump mara nyingi alikuwa akiwashambulia Waislamu na kuahidi kuwazuia kuingia nchi hiyo, na mbali na kuongezeka makundi yaliyo dhidi ya Uislamu, hujuma na jinai zilizokuwa zikisababishwa na chuki dhidi ya Waislamu ziliongezeka hata kabla ya kuingia kwake madarakani." Linda Sarsour, mwanaharakati mashuhuri wa Kiislamu mwenye asili ya Palestina na anayeishi nchini Marekani aliliambia gazeti la kila wiki la nchini Marekani la Times kwamba: “Baada ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani hapo 2001 tulishuhudia ongezeko la kesi za chuki dhidi ya dini ya Kiislamu na wafuasi wa dini hiyo. Ujasusi ulio kinyume cha sheria, kufukuzwa Waislamu nchini Marekani, kufuatiliwa maisha ya Waislamu, kuzuiwa kusafiri kwa ndege na kuongezeka mashambulizi yanayosababishwa na chuki dhidi ya Uislamu ni miongoni mwa mambo tuliyoyashuhudia wakati huo.” Mwisho wa kunukuu.

Linda Sarsour, mwanaharakati mashuhuri wa Kiislamu mwenye asili ya Palestina na anayeishi nchini Marekani

Hivi sasa pia na baada ya kupita muda mrefu na kupungua chuki katika jamii ya Marekani dhidi ya Waislamu, kwa mara nyingine tena wimbi hilo limeibuka na kushika kasi kufuatia kuingia madarakani Rais Donald Trump wa nchi hiyo. Hivi sasa Waislamu nchini Marekani wanapitia wakati mgumu kutokana na ongezeko hilo la chuki na ubaguzi dhidi yao. Hata hivyo sambamba na ongezeko hilo la chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu, wanaharakati wanaopinga wimbi hilo, nao wamekuwa wakiendeleza harakati zao katika uwanja huo. Linda Sarsour anasema tena: “Kuingia madarakani Rais Trump akiambatana na chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na kadhalika hatua zake hasi kuwalenga Waislamu kukiwemo kuwazuia raia wa baadhi ya nchi za Kiislamu kuingia Marekani, kumepelekea asilimia kubwa ya Wamarekani kuungana pamoja kuwaunga mkono Waislamu na kumpinga rais huyo mwenye chuki nchini humo.” Bi Sarsour ambaye hivi karibuni aliratibu maandamano ya wanawake wa Marekani dhidi ya Trump anaendelea kusema: “Kushiriki kwangu katika maandamano hayo ya kumpinga rais huyo nikishirikiana na raia wengine wa Marekani, kulikuwa na taathira chanya kwa Waislamu, kwa kuweza kuvutia hisia za Wamarekani kuwahusu Waislamu hao.” Mwisho wa kunukuu.

Chama cha Alternative for Deutschland chenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani

Maandamano ya wanawake wa Marekani dhidi ya Rais Donald Trump yalifanyika tarehe 21 Januari mjini Washington. Kadhalika miji mingine 30 ya Marekani ilishuhudia maandamano kama hayo kwa lengo la kuunga mkono haki za wanawake, kufanyiwa marekebisho sheria ya uhajiri na kuzingatiwa uadilifu mkabala wa ubaguzi.

**********

Kwa hakika baada ya kuingia madarakani Trump mwenye chuki dhidi ya Uislamu, vitendo vya hujuma na ubaguzi vilishtadi zaidi. Barani Ulaya pia hali ikawa hivyo hivyo ambapo sambamba na kuongezeka kwa wimbi hilo, ndivyo ambavyo vyama vya mrengo wa kulia na vyenye kuchupa mipaka na chuki dhidi ya Uislamu vilizidi kupata mafanikio. Kama tulivyosema huko nyuma, moja ya vyama hivyo vya mrengo wa kulia na vyenye misimamo ya kigaidi barani Ulaya ambavyo vilipata mafanikio makubwa ya kisiasa kilikuwa ni chama cha Alternative cha nchini Ujerumani ambacho kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge wa tarehe 24 Septemba mwaka jana. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, kwa chama cha mrengo wa kulia, chenye misimamo ya kibaguzi na ugaidi na chuki dhidi ya Uislamu kuweza kupata karibu asilimia 13 ya kura na kati ya viti 96 katika bunge la Bundestag nchini Ujerumani.

Bendera ya chama chenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani

Chama hicho kwa kifupi (AfD) ni chama cha kwanza na kikuu kinachoongoza upinzani dhidi ya siasa za uhajiri zinazotekelezwa na serikali ya nchi hiyo ambapo kinataka kupigwa marufuku kuingia nchi hiyo wahajiri. Mafanikio ya chama hicho mwaka uliopita kimsingi yalitokana na upinzani wa jamii ya walio wengi miongoni mwa raia wa Ujerumani juu ya siasa za Bi Angela Merkel kuhusiana na wahajiri. Hii ni kusema kuwa, chama hicho cha kupinga wahajiri cha Alternative for Deutschland kinaitaka serikali kufunga mipaka ya Umoja wa Ulaya sambamba na kudhibitiwa kikamilifu mipaka ya nchi hiyo kuwazuia wahajiri. Kwa imani ya chama hicho, dini ya Uislamu inakinzana na jamii na tamaduni za Ujerumani. Mitazamo ya chuki dhidi ya Uislamu ya viongozi wa chama cha Alternative for Deutschland ndio inayokaririwa kila siku katika vyombo vya habari nchini Ujerumani.

Björn Höcke kiongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho

Kwa mfano, Björn Höcke kiongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho alitangaza hivi karibuni kuwa, ikiwa atachaguliwa basi ataingia katika vita dhidi ya Uislamu. Kwa mujibu wa Höcke chama chake kitafanya juu chini kuzuia ujenzi wa misikiti nchini Ujerumani na Ulaya kwa ujumla. Matamshi hayo ya Höcke yalichapishwa na magazeti ya nchi hiyo likiwemo lile la Die Welt. Akifafanua suala hilo, Björn Höcke alisema: “Wakati wowote tutakaposhika madaraka Ujerumani, tutaanza kuchukua hatua za haraka ili tuweze kuishi maisha ya uhuru hapo baadaye. Katika hali hiyo tutatekeleza hatua kali kuzuia mambo matatu makuu, yaani jina la Muhammad, waadhini na minara ya misikiti.” Mwisho wa kunukuu.

**********

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo wa chama cha mrengo wa kulia cha Alternative, hivi sasa chama hicho kinafanya juhudi kwa ajili ya kuzuia ujenzi wa misikiti barani Ulaya. Aidha kwa mujibu wa Björn Höcke kuanzia sasa, Waislamu hawatoweza kutumia ‘uhuru wa dini’ kujenga misikiti wala maeneo yao ya ibada barani humo. Hayo ni matamshi ya wazi zaidi na ya chuki ya hali ya juu dhidi ya dini ya Kiislamu kuwahi kutolewa na kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha Alternative for Deutschland. Ni kwa ajili hiyo ndio maana matamshi hayo ya chuki na ubaguzi yakaakisiwa kwa ngazi ya juu zaidi ndani na nje ya Ujerumani.

Frauke Petry, kiongozi wa zamani wa chama hicho cha Alternative for Deutschland

Awali Frauke Petry, kiongozi wa zamani wa chama hicho cha Alternative for Deutschland alipendekeza kutimuliwa Björn Höcke kutoka ndani ya chama hicho kutokana na misimamo yake ya kuchupa mipaka. Hata hivyo itafahamika kuwa, licha ya chuki na ubaguzi huo wa hali ya juu na wa wazi dhidi ya dini ya Uislamu, Waislamu kwa upande wao wameendelea kufikisha ujumbe bora na wa kuvutia wa dini hiyo ya mbinguni ndani ya mioyo ya watafuta ukweli wa Ulaya. Sambamba na wimbi hilo la chuki la Björn Höcke, kumeripotiwa matamshi mengine kama hayo kutoka kwa kiongozi mwingine wa chama hicho kuulenga Uislamu.

Ndugu wasikilizaji, sehemu ya 35 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

Tags