Jun 03, 2018 15:11 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 36 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tuliashiria njama na juhudi za viongozi wa chama cha Alternative for Deutschland kwa ajili ya kuzuia ujenzi wa misikiti na maeneo ya ibada ya Waislamu katika nchi za Ulaya. Ama leo tutaashiria kadhia ya kusilimu mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho huko nchini Ujerumani. Ndugu wasikilizaji Arthur Wagner, mmoja wa wajumbe wa ngazi za juu wa chama cha Alternative for Deutschland katika jimbo la Brandenburg ameamua kusilimu na kuchagua jina la Ahmad kuwa jina lake.

Bendera ya chama cha Alternative for Deutschland

Wagner mwenye asili ya Russia alikuwa mjumbe wa ngazi za juu wa chama hicho katika jimbo hilo tangu mwaka 2015 hadi Januari mwaka huu. Kadhalika alikuwa mjumbe wa kamati maalumu ya jimbo la Brandenburg kwa ajili ya kufuatilia masuala ya makanisa na jamii za kidini eneo hilo. Sababu ya Arthur Wagner kuamua kusilimu na kujiunga na dini ya Uislamu ni kadhia ya Kanisa la Kiprotestanti kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja. Akizungumza na gazeti la Bild-Zeitung la nchini Ujerumani Wagner alisema: "Moja ya sababu za mimi kuhamia katika dini ya Uislamu ni muundo wa mabadiliko ya kanisa, mabadiliko ambayo kimsingi yamenifanya hata nishindwe kufahamu kiini chake." Alizidi kufafanua kutoridhwa kwake na mwenendo wa chama cha Alternative for Germany AfD na kadhia ya ndoa za watu wa jinsia moja. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 48 alisisitiza kwamba, sababu ya yeye kuendelea kusalia kuwa mwanachama wa chama hicho cha mrengo wa kulia, ni kuunda daraja la mawasiliano kati ya Waislamu wa Ujerumani na jamii ya Wajerumani. Kwa hakika uamuzi aliouchukua Wagner wa kuamua kuwa Muislamu uliwastaajabisha watu wengi nchini humo.

*******

Hata hivyo kitendo cha Arthur Wagner kusilimu, kimemfanya akabiliwe na upinzani mkali ndani ya chama hicho chenye misimamo ya chuki ya hali ya juu dhidi ya Uislamu kwa ajili ya uwakilishi wake bungeni na inaonekana kwamba ni suala zito la yeye kuweza kuendelea kuwa mwanachama wa chama hicho au angalau kuruhusiwa tu kuishi maisha ya amani nchini Ujerumani.

Arthur Wagner, mmoja wa wajumbe wa ngazi za juu wa chama cha Alternative for Deutschland aliyesilimu

Katika mahojiano na gazeti la Bild-Zeitung alielezea kupokea barua kadhaa za vitisho hasa baada ya hatua yake ya kutangaza kuwa Mwislamu. Wagner anasema: "Nimepokea barua kadhaa ambazo ndani yake zilinikejeli kwamba, kabla sijatia mkono wangu katika kuunda bomu, basi ninatakiwa niondoke Ujerumani." Mwisho wa kunukuu. Licha ya kwamba jamii ya Magharibi siku hadi siku inaendelea kujitenga mbali na misingi ya kuvumiliana na uhuru wa kujieleza na kuabudu, bado serikali za madola hayo ya Magharibi zimeendelea kuwahadaa walimwengu kwamba zinaheshimu misingi hiyo. Hii ni katika hali ambayo madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakijaribu hata kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kufuatilia kile yanachodai kuwa eti ni uhuru wa kiraia au uhuru wa kuabudu. Ndani ya mataifa hayo hayo jamii na dini za walio wachache hususan Uislamu  zinashuhudia ubaguzi na mipaka mbalimbali kuzilenga. Wiki haipiti bila kuripotiwa habari ya kuwekewa mashinikizo mapya Waislamu wa nchi za Magharibi au kushambuliwa moja ya maeneo yao ya ibada. Yote hayo yanaonyesha tofauti kubwa iliyopo baina ya nara tupu za nchi za Ulaya na matukufu ya uhuru wa kuabudu kwa ujumla, ambazo kwa makumi ya miaka zimekuwa zikipigiwa propaganda na madola hayo.

******

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi hii ikiwa ni sehemu ya 36.

Ndugu wasikilizaji mtakubaliana nami kwamba, msikiti ni mahala patakatifu kwa ajili ya ibada hususan kwa wafuasi wa dini ya Kiislamu. Katika kila mji na mahala Waislamu hukutana na kujadili kujenga msikiti kwa ajili ya kutekeleza ibada zao kwa jamaa. Na inaposhindikana kujengwa msikiti, basi Waislamu hujitahidi kuswali mahala hapo kwa pamoja na kuonyesha umoja na mshikamano wao. Aidha katika mafundisho ya dini ya Uislamu, ibada iliyo bora zaidi ni swala ambayo ina nafasi maalumu.

Jamii ya Waislamu katika nchi za Magharibi

Hii ni kwa kuwa swala ni dhihirisho la Uislamu, ambapo Waislamu katika saa za mwanzo kabisa za kila siku humwelekea Mwenyezi Mungu na kumwitikia kupitia swala hiyo. Mahala popote palipo msikiti, basi Waislamu hujitahidi kuswali kwa jamaa ndani yake suala ambalo linaimarisha umoja na upendo wao. Ndugu wasikilizaji moja ya mashambulizi ya chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi, ni kuwalenga Waislamu, misikiti na maeneo yao ya ibada. Kama tulivyosema awali,  ni vigumu kupita wiki bila kuripotiwa shambulizi dhidi ya misikiti au maeneo ya ibada ya Waislamu huko barani Ulaya. Mashambulizi hayo yanalenga kusambaratisha dhihirisho la Uislamu sambamba na kuwawekea mashinikizo makali yenye lengo la kuwatenga na hatimaye kuwafukuza kabisa katika nchi hizo wafuasi wa dini hiyo ya mbinguni.

Bekir Altaş Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu nchini Ujerumani

Kuhusiana na suala hilo, Bekir Altaş Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu nchini Ujerumani yenye makao yake mjini Cologne hivi karibuni alitoa ripoti ambayo ndani yake ilibainisha suala la ongezeko la mashambulizi dhidi ya misikiti na vituo vya Kiislamu katika nchi tofauti za Ulaya. Akiendelea kufafanua alisema: "Katika miezi ya hivi karibuni kumeongezeka zaidi mashambulizi dhidi ya misikiti, suala ambalo limewazidishia wasi wasi mkubwa Waislamu. Na moja ya sababu za wasi wasi huo ni kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na mashambulizi hayo." Kadhalika Bekir Altaş aliongeza kwa kusema: "Ni hivi karibuni tu ambapo misikiti ya miji ya Aachen  na Viersen nchini Ujerumani ilishambuliwa. Mbali na Ujerumani, mashambulizi kama hayo pia yameshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Ulaya kama vile Ufaransa. Kwa mfano tu watu wasiojulikana walioshambulia msikiti mmoja katika mji wa Bordeaux, Ufaransa wakiandika maneno ya vitisho dhidi ya Waislamu nchini humo." Mwisho wa kunukuu. Katika sehemu nyingine Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Kiislamu nchini Ujerumani alisisitizia juu ya umuhimu wa kukabiliana na mashambulizi hayo kuilenga misiki kwa kusema: "Matukio ya sasa yanaonyesha kwamba vikosi vya usalama na vyama vya kisiasa barani Ulaya, haviyapi umuhimu wowoye mashambulizi hayo na ni kwa ajili hiyo ndio maana hujuma hizo zimekuwa zikikaririwa kila mara."

******

Katika miaka ya hivi karibuni Ujerumani, imekuwa moja ya nchi ambazo zimewapokea kwa wingi wahajiri kutoka nchi mbalimbali. Ni katika kipindi hicho ndipo kuliposhika kasi pia harakati za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu kama vile harakati ya PEGIDA na chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD. Aidha Ujerumani imo katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya, katika hali ambayo Waislamu wanaunda asilimia tano na nusu pekee ya jamii ya watu milioni milioni 82 ya nchi hiyo.

Harakati za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu ya PEGIDA

Aidha Waislamu ni jamii ya wachache zaidi kati ya wafuasi wa dini katika nchi za Ulaya ambapo wanaheshimu kikamilifu sheria za nchi hizo. Ni wazi kuwa Waislamu hao hawataki kuona upendeleo maalumu ukifanyika kwa maslahi yao bali wanaochotaka ni kuona katiba ya Ujerumani ikitekelezwa kwa usawa kwa wananchi wote wa nchi hiyo.

Ndugu wasikilizaji, sehemu ya 36 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags