Jun 03, 2018 15:23 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 37 ya makala haya yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

Katika kipindi kilichopita tuliashiria kuwa, katika miaka ya hivi karibuni Ujerumani, imekuwa moja ya nchi zilizowapokea kwa wingi wahajiri kutoka nchi mbalimbali. Ni katika kipindi hicho ndipo kuliposhika kasi pia harakati za chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu kama vile harakati ya PEGIDA na chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany AfD. Ndugu wasikilizaji katiba ya Ujerumani inasisitizia uhuru wa dini kama ambavyo pia inaitaka serikali kudhamini usalama wa wafuasi wa dini zote na mafundisho yao. Aidha Ujerumani ina jumla ya misikiti 18 inayotambuliwa rasmi na ambayo tangu mwanzo ilijengwa kwa anwani ya misikiti, katika hali ambayo maeneo ya Waislamu yanakadiriwa kufikia 1000 hadi 1200.

Waislamu wa nchi za Magharibi

Akthari ya maeneo hayo yalianzishwa kwa matumizi ya muda mfupi, huku mengi yakiwa ni ya kulipia na maghala ya kuhifadhia vitu. Kwa mujibu wa takwimu ya kituo cha Kiislamu nchini humo, misikiti muhimu ndani ya Ujerumani inapatikana katika miji ya Mannheim, Hamburg, Berlin, Marl, Dortmund, Cologne, Weßling, Bonn, Frankfurt, Singen na Pforzheim, huku misikiti ya Aachen na Munich nayo ikitajwa kuwa na nafasi muhimu ndani ya taifa hilo. Hata hivyo isisahaulike kwamba, akthari ya misikiti hiyo ina mazingira mabaya kama ambavyo pia imejengwa mbali na miji, huku mingine ikiwa imejengwa katika maeneo ya viwanda. Licha ya mipaka na vizuizi ambavyo wamewekewa wafuasi wa dini ya Uislamu kutokana na chuki dhidi ya dini hiyo, lakini Waislamu wamekuwa wakijitahidi kuzingatia sheria na kutoenda kinyume na sheria za nchi hiyo. Katika uwanja huo Waislamu kupitia roho ya udugu na kupenda amani, wameweza kuwavutia watu wengi na hivyo kukabiliana na wimbi la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu nchini Ujerumani. Ndugu wasikilizaji mwezi Februari mwaka huu, mji wa Cottbus nchini Ujerumani, ulikuwa uwanja wa maandamano ya waungaji mkono na wapinzani wenye chuki kuwalenga wahajiri. Hii ni kusema kuwa wafuasi wa mrengo unaopinga chuki na ubaguzi dhidi ya wahajiri na ule wenye chuki na kupinga siasa za serikali kuwahusu wahajiri, walimiminika mabarabarani wakipiga nara kutetea misimamo yao.

*******

Nara dhidi ya dini tukufu ya Uislamu na kadhalika dhidi ya Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani, zilikuwa lengo kuu la maandamano hayo dhidi ya Uislamu. Mkabala wake wale wanaopinga ubaguzi waliandamana kwa kipiga nara za kulaani ubaguzi na chuki ndani ya jamii ya nchi hiyo.

Waislamu nchini Uingereza

Katika maandamano hayo pia washiriki walishikilia mikononi mwao baluni zenye rangi tofauti pamoja na maua wakionyesha ishara ya kulaani chuki na ubaguzi katika jamii. Inafaa kuashiria kuwa, mji wa Cottbus unaopatikana katika jimbo la Brandenburg lenye watu wasiozidi laki moja, katika wiki za hivi karibuni ulishuhudia mapigano kati ya wahajiri na baadhi ya raia wa nchi hiyo ya Ulaya, suala ambalo lilichochea wimbi la chuki na ukatili kuwalenga wahajiri. Kwa kuzingatia hali hiyo, hatimaye viongozi wa mji wa Cottbus, waliamua kusimamisha zoezi la kuwapokea wahajiri na wakambizi eneo hilo. Ni baada ya hapo ndipo viongozi kadhaa wa Brandenburg wakatangaza kusimamishwa zoezi la kupelekwa wahamiaji hao mjini hapo.
John Glowsman, mmoja wa viongozi wa idara ya vyombo vya habari ya mji huo alinukuliwa akisema: "Tunaweza kusema kuwa, kwa kipindi kifupi sana kumepatikana mabadiliko makubwa nchini." Mwisho wa kunukuu. Inafaa kuashiria kuwa, katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni, wahajiri wengi walitia kambi ndani ya mji huo kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 8.5, yaani sawa na ongezeko la mara mbili zaidi. Kuhusiana na suala hilo, John Glowsman anasema: "Ninakiri kwamba, kuna haja ya kuwapasha habari zaidi wakazi wa eneo hilo kuhusiana na suala hilo." Mwisho wa kunukuu. Nukta ya kuzingatia ni hii kwamba wakazi wa mji wa Cottbus wana uelewa mdogo katika uwanja wa kuamiliana na wahajiri, ikilinganishwa na raia wa nchi nyingine za Ulaya na ni kwa ajili hiyo ndio maana miamala yao kuwahusu wahajiri ikawa mibaya kila mara. Kwani akthari ya wakazi wa mji huo wanawaona wahajiri kama watu hatari kwa usalama wao.

Waislamu wa Uingereza

Jambo la kusikitisha ni kwamba, hata raia wengi wa Ujerumani, wana mtazamo hasi kuihusu dini ya amani ya Uislamu. Katika hali hiyo, serikali na vyombo vya habari nchini Ujerumani pia kwa kuzingatia malengo ya kisiasa, huwa vinatangaza habari za Waislamu kwa kuonyesha sura mbaya ya ukatili na ugaidi, ili kwa njia hiyo viweze kupigilia msumari wa chuki na ubaguzi dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ya mbinguni.

********

Kama kwanza ndio unafungua redio yako, kipindi kilichoko hewani ni makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi hii ikiwa ni sehemu ya 37. Ndugu wasikilizaji Mtume Muhammad (saw), ambaye ni mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, alilingania upole na kuoneana huruma. Katika sura ya 107 ya Suratul-Anbiya Mwenyezi Mungu anafafanua kuwa Mtume huyo ni rehma kwa walimwengu wote kwa kusema: "Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote." Mwisho wa aya. Hii ni kusema kuwa, wanadamu wote kuanzia waumini na makafiri, kwa pamoja wanategemea rehma za Mtume Muhammad (saw) katika maisha yao yote kwani huo ndio msingi wa utume wake ambao ni kumuokoa mwanadamu. Hii ikiwa na maana kwamba, iwapo kundi fulani litaamua kumfuata na kumwamini mtukufu huyo, huku lingine likiamua kumpinga, basi madhara yatalihusu kundi pekee lililompinga, kwani hilo halitoathiri katika rehma za Nabii huyo wa Allah kwa walimwengu wote. Suala hilo ni sawa na hospitali yenye nyenzo zote muhimu za matibabu sambamba na kuwa na madaktari waliobobea huku ikiwafungulia milango watu wote wanaohitajia matibabu.

Waislamu wa Magharibi wakipinga chuki za kidini dhidi yao

Hivyo inapotokea wagonjwa fulani kwa jeuri yao binafsi watakataa kwenda kutibiwa katika hospitali hiyo, hilo halitoathiri maendeleo yaliyopo ndani ya hospitali hiyo kwa ajili ya kila mtu, bali litawahusu wale wale waliosusa kwenda kwenye hospitali hiyo. Kwa ajili hiyo, ibara ya 'Walimwengu' ni yenye maana pana ambayo inawajumuisha pia watu wa karne zote na ni kwa ajili hiyo ndio maana aya hiyo ikasisitizia utume wa mwisho wa Nabii Muhammad (saw) kwani uwepo wake unatoa mustakbali na mwanga kwa wanadamu wote duniani. Je, dini ya Mtume wa namna hiyo, inaweza kuwa chanzo cha ukatili na utumiaji mabavu dhidi ya watu wengine?

*******

Tukiwa bado huko Ulaya, hivi karibuni Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitoa matamshi mapya dhidi ya Uislamu kupitia mpango wa marekebisho kuuhusu Uislamu na wafuasi wa dini hiyo nchini humo. Akizungumza na gazeti la Ufaransa la Le Journal du Dimanche Macron alibainisha kuandaliwa mpango maalumu kwa ajili ya kufuatilia harakati na nyendo zote za dini ya Uislamu nchini humo, mpango unaoenda sawa na hatua maalumu zilizoainishwa na serikali. Sambamba na kusisitizia umuhimu wa kuchunguzwa shughuli za Kiislamu nchini Ufaransa, Rais Emmanuel Macron aliahidi kuwasilisha mpango huo katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu 2018.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Aliendelea kusema kuwa, kwa kipindi ambacho mpango wake huo bado haujakamilika, hatofafanua zaidi kuhusu yale yaliyomo, huku akidai kwamba ameazimia kuweka mahusiano yenye mfumo bora na wa kimantiki kati ya taifa la Ufaransa na dini ya Uislamu kiasi kwamba, thamani zote za nchi hiyo zitatakiwa kuheshimiwa na harakati za Kiislamu ndani ya Ufaransa. Kadhalika alifafanua kwamba, katika kuratibu mpango huo, kumezingatiwa masuala mawili muhimu ambayo Mosi ni mahusiano ya Waislamu na taifa la Ufaransa na Pili ni kudhibitiwa harakati za kidini za Waislamu hao.

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 37 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

Tags