Jun 04, 2018 04:09 UTC
  • Jumatatu, Juni 4, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 19 Ramadhani 1439 Hijria, sawa na tarehe 4 Juni, 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1399 iliyopita, Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume Mtukufu SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiwa anaswali swala ya alfajiri katika msikiti wa mji wa Kufa na mtu aliyeitwa Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali A.S alikufa shahidi baada ya siku 3. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na uadilifu. Alipata elimu na mafunzo kutoka nyumba ya Mtume Mtukufu SAW, na alikuwa mwanamume wa kwanza baada ya Mtume SAW kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na hata kuhatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu huku akionyesha ushujaa mkubwa katika vita mbalimbali vya haki dhidi ya batili. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo. Kiasi ambacho moyo wake ulikuwa wenye kuathiriwa sana na kujawa na huruma kwa kuona machozi ya mtoto yatima. Imam Ali AS alipenda haki na uadilifu na kupambana vilivyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima Imam Ali AS anasema: 'Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake.'

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, alifariki dunia Ruhullah Musawi Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuishi humu duniani kwa miaka 87. Baada ya kutangazwa habari ya kufariki kwake, ilimwengu wa Kiislamu uligubikwa na wingu la simanzi na huzuni. Imam Khomeini alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1902 huko katika mji wa Khomein katikati mwa Iran. Alianza harakati zake za kisiasa sambamba na shughuli za kielimu na kiutamaduni. Kutokana na shughuli zake za kisiasa zilizokuwa zikiukera sana utawala wa kidhalimu wa mfalme Shah, utawala huo ulimbaidisha Imam katika nchi za Uuruki na kisha Iraq. Katika kipindi cha miaka 13 akiwa uhamishoni huko Iraq, Imam (MA) alilea na kuwafunza wanafunzi wengi na wakati huohuo kufichua maovu yaliyokuwa yakifanywa humu nchini na utawala wa Shah kwa ushirikiano wa karibu wa Marekani. Baada ya kupamba moto mapambano na harakati za Kiislamu zilizokuwa zikiongozwa na Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah, hatimaye Imam alilazimika kutoka nchini Iraq na kuhamia Ufaransa, hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipofikia ushindi hapa nchini hapo mwaka 1979. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Imam Khomeini (MA), mwanzilishi wa mfumo wa Kiislamu nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Baraza Linalomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mfumo wa Kiislamu wa Iran lilimchagua Sayyid Ali Khamenei, kuuongoza mfumo huu. Muda mfupi baada ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA), baraza hilo lilikutana kwa lengo la kumchagua mrithi wake. Wanachama wa baraza hilo ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi, walichunguza uzeofu wa kimapinduzi na sifa nyingine muhimu za Ayatollah Khamenei zikiwemo za ushujaa, uwezo mkubwa wa kuchambua mambo ya zama, ujuzi mkubwa wa masuala ya kidini, fikhi na sheria ya Kiislamu, uadilifu, utawala bora na kisha kumchagua kwa wingi wa kura kuwa Kiongozi Mkuu wa mfumo wa Kiislamu wa Iran.

Leo ni tarehe nne Juni, siku muhimu katika kalenda ya dunia ambayo inafahamika kama siku ya kuwaunga mkono watoto kutokana na mashambulizi na ukatili. Mwaka 1982 na katika kuchunguza hali ya watoto wa Palestina na Lebanon ambao ni wahanga wakubwa wa mashambulizi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, tarehe nne ya kila mwaka ilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa siku ya watoto wasio na hatia wahanga wa ukatili yaani ‘International Day of Innocent Chindren Victims of Aggression’ ambapo katika siku hiyo huchunguzwa machungu ya watoto wahanga wa ukandamizaji wa kimwili na kisaikolojia. Inafaa kuashiria hapa kwamba, hadi sasa karibu watoto laki mbili na elfu 50 duniani, wanatumikishwa kama askari katika migogoro mbalimbali. Akthari ya watoto hao hujiunga na makundi ya wabeba silaha kutokana na umasikini wa kupindukia. Aidha karibu nusu ya watu milioni 50 ambao wamelazimika kuwa wakimbizi duniani, ni watoto. Mbali na hayo ni kwamba, kati ya wakimbizi milioni 22 ambao wanasimamiwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), milioni 10 ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18. Kadhalika mamia ya watoto wanashikiliwa katika jela za kutisha za utawala haramu wa Kizayuni, huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

International Day of Innocent Chindren Victims of Aggression

Siku kama ya leo miaka 586 iliyopita, alifariki dunia Ologh Beig, msomi mkubwa wa elimu ya nyota wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 796 Hijiria eneo la Soltaniyeh, moja ya miji ya magharibi mwa Iran na kulelewa katika taasisi ya babu yake, Timur ambayo ni moja ya silsila ya utawala wa Timur. Akiwa na umri wa miaka 16 aliteuliwa kuwa kamanda wa jeshi katika mji wa Mā warāʼ al-Nahr (Transoxiana), mji wa katikati mwa Asia. Kinyume na utawala wa Timur, yeye hakupendelea kupanua dola hilo na badala yake akajikita katika utafiti na utalii. Katika kipindi hicho aliasisi kituo cha kielimu ambacho kilitoa elimu ya nyota. Aidha hatua yake nyingine ilikuwa ni kujenga kituo cha kufuatilia nyota huko katika mji wa Samarqand hapo mwaka 828 Hijiria, ambacho kilitoa wasomi wengi wa masuala ya nyota.

Ologh Beig

Siku kama ya leo miaka 607 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa hisabati na nyota wa Iran, Ghiyathud-Din Jamshid Kashani. Alikuwa mahiri katika hisabati na nyota huku akihusika pia kuvumbua nyenzo nyingi muhimu kwa ajili ya kuchunguza nyota. Alibobea katika mahesabu kiasi kwamba aliweza kubuni kanuni kadhaa za taaluma hiyo. Aidha alihusika katika ujenzi wa kituo muhimu cha kuchunguza nyota cha Samarghand huku akiwa pia ameacha athari mbalimbali za elimu ya hisabati na nyota. Miongoni mwa athari hizo ni kitabu cha Miftaahul-Hisaab na 'Risaalat Aalaat Rasad.'

Siku kama ya leo miaka 223 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 52, Alexis Claude Clairaut, mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Akiwa kijana mdogo alikuwa na maandalizi ya hali ya juu ya kielimu kiasi kwamba akiwa na miaka 10 tayari alikuwa amekuwa na uhodari katika masuala ya hesabati. Alipotimiza miaka 13 aliandika makala muhimu kuhusiana na hesabati. Aidha  alipotimiza umri wa miaka 16 Alexis Claude Clairaut aliandika makala mengine katika uwanja huo ambayo yaliwashangaza wasomi wengi wa hesabati wa zama hizo. Utunzi wake huo ulimfanya kuteuliwa kujiunga na chuo kikuu akiwa na umri mdogo ambapo aliendeleza utafiti wake uliozaa matunda katika uga huo.

Alexis Claude Clairaut,

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, serikali ya China ilishambulia na kuwaua wanachuo wengi katika uwanja wa Tiananmen huko Peking mji mkuu wa nchi hiyo. Siku hiyo na licha ya kuwepo onyo la serikali dhidi ya kufanyika maandamano hayo, lakini maelfu ya wanachuo walikusanyika katika uwanja huo ili kuishinikiza serikali iruhusu kuwepo uhuru wa shughuli za kisiasa, kupunguzwa uwezo wa chama cha kikomonisti, kuongezwa uwezo wa bunge na kuchaguliwa wabunge moja kwa moja na wananchi. Baada ya kuona kuwa maandamano ya wanachuo hao yalikuwa yanaongezeka badala ya kupungua, polisi na jeshi la China liliamua kuyavunja kwa nguvu kwa kuua na kuwakandamiza wanachuo hao.

Tiananmen

Tags

Maoni