Jul 23, 2018 02:24 UTC
  • Jumatatu tarehe 23 Julai, 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na 23 Julai, 2018.

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita alifariki dunia mfalme Hassan wa Pili wa Morocco baada ya kuongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 38. Alizaliwa mwaka 1929 na kukalia kiti cha ufalme wa Morocco miaka mitano baada ya uhuru wa nchi hiyo. Mfalme Hassan wa Pili alinusurika kuuawa mara kadhaa akiwa madarakani. Dikteta huyo wa Morocco aliwakandamiza upinzani wake jambo ambalo lilizusha upinzani na malalamiko ya wananchi wa Morocco dhidi ya kiongozi huyo. Mwana wa kiume wa mfalme Hassan yaani Muhammad wa Sita alichukua kiti cha ufalme na kuiongoza Morocco akiwa na umri wa miaka 36 baada ya kufariki dunia baba yake.

Mfalme Hassan

Siku kama ya leo miaka 189 iliyopita mashine ya kwanza ya kuandika (typewriter) ilivumbuliwa na kusajiliwa. Tarehe 23 Julai mwaka 1829 Mmarekani William Brett alisajili mashine ya kuandikia katika jimbo la Michigan ambayo ilisemekana kuwa ndiyo ya kwanza ya kufanya kazi hiyo. Baada ya hapo hakukuashiriwa tena mashine hiyo ya kuandikia iliyotengenezwa na William Brett. Miaka 31  baadaye yaani mwaka 1867 Wamarekani wengine watatu katika mji wa Milwaukee kwenye jimbo la Wisconsin, walitengeneza mashine ya kuandikia ambayo ilikuwa rahisi zaidi kutumia. Ni vyema kukumbusha kuwa juhudi za kutengeneza mashine ya kuandikia (typewriter) zilianza katika karne ya 14 lakini hazikuzaa matunda hadi karne ya 18.

Mashine ya zamani ya kuandikia

Tarehe 23 Julai miaka 220 iliyopita jeshi la Napoleon liliwasili katika mji wa Cairo huko Misri na mji huo ukakaliwa kwa mabavu na majeshi vamizi ya Ufaransa. Utawala wa silsila ya Mamaliki ulifikia kikomo huko Misri baada ya mji wa Cairo kukaliwa kwa mabavu na wavamizi wa Kifaransa. Napoleon alielekea Cairo mji mkubwa zaidi wa Misri ambao pia ulikuwa mji mkuu wa utawala wa silsila ya Mamalik baada ya jeshi lake kuikalia kwa mabavu bandari ya Alexandria kwa kutumia zana za kisasa za kivita.

Napoleon

 

Tags

Maoni