Sep 10, 2018 04:08 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Sep 10

Huu ni mkusanyiko wa matukio muhimu ya spoti yaliyojiri duniani ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa

Voliboli: Timu ya akina dada walemavu ya Iran yaibuka ya 2

Timu ya taifa ya voliboli ya walemavu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo yaliyofanyika nchini Thailand. Timu hiyo ya viti vya magurudumu ya Iran siku ya Jumatano ilishindwa kufurukuta mbele ya mwenyeji Thailand na hivyo kuambulia kichapo cha vikapu 40-25 katika kitimutimu cha fainali.

Timu ya wanawake ya viti vya magurudumu ya Iran

 

Timu ya wanawake ya Iran ilifungua kampeni zake za kusaka ushindi kwa kupata ushindi wa kishindo wa vikapu 64-16 iliposhuka dimbani kuvaana na Laos. Kadhalika iliizaba Cambodia vikapu 71-8 na kufanikiwa kutinga fainali baada ya chachafya Korea Kusini vikapu 51-19. Mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama Thailand Open yalianza Septemba 2 na kufunga pazia lake Jumatano ya Septemba 9 katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok.

Kiongozi Muadhamu awapongeza wanariadha wa Iran kwa kung'ara

Kiongozi Muadhamu Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewamiminia pongezi kedekede wanariadha wa Iran kwa kufanya vyema katika Michezo ya Asia mwaka huu 2018 iliyofanyika nchini Indonesia. Katika ujumbe wake wa mkono wa tahania, Ayatullah Ali Khamenei amesema, "Mumewafurahisha mno wananchi wa Iran na kuiletea izza na fahari bendera yetu." Wanariadha wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliambulia nafasi ya sita katika mashindano hayo ya kikanda yanayofahamika kwa Kimombo kama 2018 Asian Games kwa kuzoa jumla ya medali 62, zikiwemo 20 za dhahabu.

Kiongozi Muadhamu Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Nchi za Asia zilizoongoza jedwali la medali ni pamoja na China, Japan, Korea Kusini, Indonesia na Uzbekistan. Duru ya 18 ya Michezo ya Asia mwaka huu 2018 iling'oa nanga Agosti 18 na kufunga pazia lake siku ya Jumapili katika miji ya Jakarta na Palembang.

Tiketi za Afcon; Kenya yavuka kiunzi, Tanzania yalazimishwa sare

Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars siku ya Jumamosi ilifanikiwa kuwika nyumbani kwa kupata ushindi hafifu wa bao 1-0 dhidi ya Black Stars ya Ghana kwenye mechi ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019. Stars wakiongozwa na mshambuliaji matata Michael Olunga walivuna alama tatu muhimu kupitia bao safi la kujifunga kutoka kwa beki Mghana Nicholas Opoku. Huku nambari 45 duniani Ghana ikiomboleza kupoteza alama zote jijini Nairobi, nambari 112 duniani Kenya inasherehekea kupata ushindi wa kihistoria baada ya kufuzu matumaini ya kurejea AFCON kwa mara ya kwanza tangu ishiriki makala ya mwaka 2004 nchini Tunisia.

Washindi wa AFCON mwaka jana 2017

 

Mchezaji Joash Onyango alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 61 na kuilazimisha Kenya kusakata dakika zilizosalia ikiwa na wachezaji 10. Baada ya mchuano huu wa kusisimua, ambao ulihudhuriwa na kinara wa upinzani Raila Odinga na Waziri wa Michezo Rashid Echesa, Wakenya waliendeleza gumzo kuhusu ushindi huo kwenye mitandao ya kijamii. Kenya imepata ushindi huo mwembamba licha ya kiungo wa Kati wa klabu ya Tottehham Hotspurs Victor Wanyama, kutokuwepo katika kikosi cha timu ya taifa ya Kenya, wakati Harambee Stars ilipomenyana na Ghana siku ya Jumamosi, jijini Nairobi, katika mechi hiyo muhimu ya hatua ya makundi kufuzu katika fainali ya Afrika mwakani nchini Cameroon.

Huku hayo yakiarifiwa, Uganda Cranes ilishindwa kujizolea alama tatu dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania licha ya kuupigia nyumbani. Hata hivyo timu hiyo ambayo haijashinda mechi kubwa chini ya ukufunzi wa Sebastien Desabre bado inaongoza katika kundi L baada ya mechi mbili ikiwa na pointi nne.

Siku ya Jumapili, Amavubi ya Rwanda ilipata pigo kubwa katika mechi yake ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 baada ya kuchabangwa na Ivory Coast mabao 2-1.

...............................TAMATI........................

 

 

Tags