Oct 09, 2018 02:32 UTC
  • Jumanne, Oktoba 9, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 29 Muharram 1440 Hijria sawa na tarehe 9 Oktoba 2018.

Siku kama ya leo, miaka 537 iliyopita alifariki dunia Muhammad Heravi, mwanahistoria wa Waislamu huko mjini Herat, magharibi mwa Afghanistan ya leo. Heravi, alizaliwa katika familia maarufu mjini Balkh, kaskazini mwa nchi hiyo lakini aliishi zaidi umri wake wote katika mji wa Herat. Kutokana na elimu yake kubwa, alipewa heshima na mazingatio makubwa na Ali-Shir Nava'i, waziri mwanasayansi wa silsila ya watawala wa Mughal, ambaye alikuwa akiwaheshimu sana wasomi na wanazuoni. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Tarikh Raudhati Safaa kinachochunguza historia ya dunia tangu kuumbwa kwake hadi zama za msomi huyo. 

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, yaani tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa chini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Muingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye walifanikiwa kupatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo.

Bendera ya Uganda

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra za Che Guevara za kuanzisha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alikutana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa serikali ya Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la Marekani, CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi.

Ernesto Che Guevara

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsiya mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia. Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina.

Majid Abu Sharar

 

Tags