Dec 22, 2018 07:31 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (135)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

 

Kipindi chetu kilichopita kilijadili madhui ya ‘Kupenda Dunia na Kuiacha au Kuipa Mgongo. Kama mnakumbuka tulisema kuwa, chimbuko la dhambi na kughafilika na utajo wa Mwenyezi Mungu ni kupenda dunia. Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema: Kuipenda dunia ni chimbuko la kila kosa (dhambi). Tulieleza kwamba, madhumuni ya kuichukia dunia na kuipa mgongo ni kuipuuza ile dunia ambayo inamuweka mbali mwanadamu na malengo na matakwa yake makuu na ambayo inamvuta mwanadamu na kumfanya aache njia ya saada na ufanisi na kuelekea upande wa mashaka na matatizo. Aidha tulibainisha kwamba, kama mtu ataitazama dunia kwa ibra ataiona kuwa ina mafunzo na mambo mengi ya ibra na mazingatio. Lakini kama mtu ataitazama dunia na kukodolea macho mapambo yake na kisha kuzama katika ladha na matamanio yake itampofusha mhusika. Kadhalika tulikunukulieni hadithi kadhaa kutoka kwa Imam Ali bin Abi Twalib AS ikiwemo ile inayosema: Itazame dunia kwa mtazamo wa mtawa aliyejitenga, na wala usiitazame kwa mtazamo wa ashiki aliyeikufia. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 135 ya mfululizo huu kitazungumzia maudhui ya ‘kushukuru’ na kukunukulieni baadhi ya hadithi kuhusiana na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.

Tunakianza kipindi chetu cha leo kwa hadithi kutoka kwa Imam Jaafar bin Muhammad al-Swadiq AS inayosema: Kushukuru ujazi na neema ni kujiepusha na dhambi na kushukuru neema hizo kwa ukamilifu ni mja kusema: ‘Alhamdulilahi Rabbi al-Alamiin’. Hivyo basi, endapo mtu atafanya jambo na amali kwa ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu kwa kutumia mkono, ulimi, kalamu, mali, cheo na daraja aliyonayo atakuwa ameshukuru neema za Mwenyezi Mungu alizojaaliwa na kuruzukiwa na Allah. Lakini endapo kwa kutumia moja kati ya nyenzo hizo akafanya dhambi, atakuwa amekufuru ujazi na neema za Mwenyezi Mungu.

الحمد لله رب العالمین

Kushukuru maana yake kushukuruku ni kuthamini kwa ulimi na vitendo neema za Mwenyezi Mungu. Wasomi na wanazuoni wa elimu ya Akhlaqi na maadili wameigawa shukurani au kushukuru katika sehemu tatu za ulimi, moyo na vitendo. Kushukuru kwa ulimi, ni shukurani ambayo mtu anaibainisha kwa kutumia ulimi wake na kwa maneno kama vile kutamka, Alhamdulilahi, au Shukran Lilahi.

Miongoni mwa mifano na misdaqi ya kushukuru kwa ulimi ni kuonyesha udhaifu na kutokuwa na uwezo wa kutoa shukurani kwa neema ambazo mja amepatiwa na Mola Muumba. Imam Mussa ibn Jaafar al-Kadhim AS amenukuliwa kuhusiana na hili akisema kuwa, mtu ambaye atataja himidi za Mwenyezi Mungu na kusema ‘Alhamdulilahi’ atakuwa ameshukuru na kuonyesha shukurani zake kwa Mwenyezi Mungu kwa neema alizopatiwa na hamdu yake hiyo ni bora zaidi na iko juu zaidi ya neema aliyopatiwa.

Sehemu ya pili ni kushukuru kwa moyo. Kushukuru kwa moyo ni kitendo cha kuonyesha shukurani kwa moyo na roho kwa neema ambazo mwanadamu amepatiwa na Mwenyezi Mungu na kuonyesha furaha na shukurani. Imam Jafar bin Muhammad al-Swadiq AS amenukuliwa akisema: Mtu ambaye amepatiwa ujazi na neema na Mwenyezi Mungu na moyo wake ukawa na ufahamu na welewa kwamba, neema ile ni adia na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa na maarifa hayo ya moyo anakuwa ametoa shukurani kwa neema.

Himidi zote za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote

Inanukuliwa katika kitabu cha Jamius Sa’adaat kwamba: Nabii Mussa AS alisema katika moja ya dua na munajaat zake kwa Mwenyezi Mungu kwamba:  Ewe Mola Muumba! Umemuumba Adam kwa mkono Wako, ukamuweka katika pepo Yako na ukamchagulia Bi Hawa awe mke wake, vipi alishukuru hayo? Mwenyezi Mungu akamjibu Nabii Mussa kwa kumwambia: Adam alifahamu kwamba, neema zote hizo ni kutoka kwangu na kwa maarifa na welewa huo akawa amenishukuru.

Wapenzi wasikilizaji aina ya tatu ya kushukuruku ambayo ni kushukuru kwa amali na vitendo ni kutumia kila neema mahala pake. Kwa mfano, macho ni moja ya neema kubwa za Mwenyezi Mungu kwa wanadamu na shukurani ya kivitendo kwa neema hii ni kushuhudia kwa macho athari za adhama ya Mwenyezi Mungu katika ulimwengu huu na kwa kuona viumbe wa Allah tuongeze maarifa yetu. Aidha kukufuru neema hizo ni kutumbukia katika uchafu wa dhambi. Kushukuru kivitendo kwa ulimi neema za Allah ni kubainisha uhakika, kunong’ona na Mwenyezi Mungu na kadhalika. Aidha kukufuru neema hizo ni kuzichafua kwa uongo, kusengenya, kutoa tuhuma na kadhalika. Imam Jafar bin Muhammad al-Swadiq anasema: Shukurani ya neema ni kujiepusha na dhambi.

Aidha katika hadithi nyingine inanukuliwa kwamba, mtu mmoja alimuuliza Imam Swadiq AS, je kumshukuru Mwenyezi Mungu kuna mpaka na kiwango ambacho mtu akikifikia anahesabiwa kuwa ni mshukurivu? Imam akajibui ndio. Bwana yule akauliza, linakuwaje hilo? Imam akasema: Amshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu kwa neema zote iwe ni katika familia au katika mali alizopatiwa na kama katika mali aliyopatiwa kuna haki ya mtu basi aitoe haki hiyo.

Baadhi ya neema za Mwenyezi Mungu humfikia mja kupitia watu wengine. Katika mazingira kama haya, mja mbali na kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ndiye mtoaji wa asili wa eema hiyo, anapaswa kumshukuru pia mtu ambaye alikuwa wenzo wa neema hiyo kumfikia. Mtume SAW analizungumzia hilo kwa kusema: Ambaye hatamshukuru kiumbe atakuwa hajamshukuru Muumba. Hatua ya mja kushukuru neema za Mwenyezi Mungu huwa chanzo na sababu ya Muumba kumuoongezea na kumzidishia mtu huyo neema. Mwenyezi Mungu anasema katika Surat Ibrahim aya ya saba kwamba:

Mkishukuru nitakuzidishieni;

Kadhalika, kukufuru neema za Allah matokeo yake ni kupata adhabu kali ya Allah.

Mwenyezi Mungu anasema katika aya hiyo hiyo ya 7 ya Surat Ibrahim kwamba:  Na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.

Asiyewashukuru watu hajamshukuru Mwenyezi Munguu

Aidha kukufuru neema za Allah huwa sababu ya neema alizopatiwa mtu kuondoka moja baada ya nyingine na mwishowe kumtoka kikamilifu neema hizo.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anatahadharisha na kueleza matokeo ya kukufuru neema katika hekima ya 244 katika Nahaja al-Balagha kwa kusema: Mwenyezi Mungu ana haki katika kila neema, kila mwenye kutekeleza haki hiyo neema humuongezekea na mwenye kupuuza hilo neema (aliyonayo) huwa katika hatari ya kuondoka.

Wanadamu na waja ambao wamefikia daraja ya juu ya ufahamu na welewa, humshukuru Allah hata wakiwa katika mazingira magumu kabisa kama maradhi na mitihani mingine. Lakini wanadamu wa kawaida humshukuru Allah katika uzima na afya njema. Kimsingi mwanadamu anapaswa kumshukuru Allah kwa neema alizompatia akiwa katika mazingira yoyote yale na si katika furaha, raha na neema bali hata katika mazingira magumu ya ghamu, huzuni na mitihani kama maradhi na kadhalika.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili ambapo tumejadili na kuzungumzia namna ya kushukuru neema za Mwenyezi Mungu pamoja na madhara ya kukufuru neema Zake.

Bila shaka mmenufaika na yale niliyokuandalieni kwa leo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Na Salum Bendera

Tags