Dec 29, 2018 07:09 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (137)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

 

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kujadili maudhui ya kushukuru na kuthamini neema za Mwenyezi Mungu. Wanadamu wengi wanapopata nguvu na utajiri hughafilika na kumsahau Allah ambaye kimsingi ndiye mmiliki wa asili wa neema na hivyyo kutoshukuru neema walizotunukiwa.

Tuliashiria kisa cha Nabii Suleiman na jinsi mjumbe huyo wa Allah, alivyoshukuru na kuuthamini neema za Allah. Tulisema pia kuwa, akili, uzima wa afya, uongofu, imani na uwepo wote wa mwanadamu katika ulimwengu huu ni ujazi na neema za Mwenyezi Mungu ambazo wanadamu tunapaswa kutoa shukurani na kumshukuru Mola Muumba kwa kututunuku neema hizi.  Hata hivyo nguvu ya kushukuru nayo ni kutoka kwa Allah. Kwa maana kwamba, hata tawfiki ya kuweza kushukuru nayo ni neema kutoka kwa Allah. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 137 ya mfululizo huu, kitajadili na kuzungumzia suala la kukufuru neema. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kukufuru neema ni kitendo ambacho kiko mkabala wa kitendo cha kushukuru neema. Kukufuru neema kunahesabiwa kuwa moja ya sifa mbaya. Mtu ambaye anakufuru neema na kwa kupuuza kwake neema nyingi na zenye thamani za Mwenyezi Mungu anakuwa amefunika na kukana neema hizo au hazithamini. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Msikufuru neema, kwani chimbuko na msingi wa kufru ni kukufuru neema na kutoshukuru.

 

Wakati Mwenyezi Mungu SWT katika Qur’ani anapobainisha sifa mbaya na zisizofaa za kibinadamu analitaja suala la kukana na kukufuقu neema za Mwenyezi Mungu kuwa ni moja ya sifa hizo. Anasema katika aya ya 112 ya Surat al-Nalh:

Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na khofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anasema: Faadhaqaha yaani akauonjesha vazi la njaa na khofu, katika hali ambayo, vazi ni la kuvaa sio la kuonja. Ibara hii ina nukta mbili za kuzingatia: Mosi, njaa, ukame na hofu itawatawala na kuwazunguka watu wa mji huo kiasi kwamba, kama vile hilo limekuwa ni vazi lao yaani liko pamoja nao na limewagubika mwili mzima. Pili ni kuwa, wahusika watauhisi umasikini na hofu kama vile wanaionja hali hiyo kwa ndimi zao.

Katika kutoa ufanunuzi kuhusiana na aya iliyotangulia, Imam Ja’afar Swadiq AS anasema: Mwenyezi Mungu amewapatia waja neema. Lakini waja hao hawakuishukuru neema hiyo. Natija ya hilo ikawa ni neema hizo kuwa chimbuko la hali mbaya, matatizo na masaibu kwao. Kwa hakika, nukta ya kuzingatia hapa ni kwamba, endapo mtu atapatiwa neema na kisha asishukuru, basi neema hiyo hugeuka na kuwa chimbuko la masaibu na matatizo kwa mja aliyekufuru neema hiyo.

Imam Jawad AS anasema: Neema ambayo haitashukuriwa, ni mithili ya dhambi isiyo na maghurifa.

Hii ina maana kwamba, kutoshukuru neema ambayo mja ametunukiwa na kuruzukiwa na Mwenyezi Mungu ni kama dhambi ambayo haina msamaha na maghufira isipokuwa adhabu. Hivyo basi, neema ambayo haijatolewa shukurani hufuatiwa na adhabu.

Inafaa ieleweke kwamba, kukufuru neema hakuwahusu makafiri na watu wasio na dini tu, bali wakati mwingine hata walioshikamana na imani hukumbwa na hali hii. Ndio maana Nabii Suleiman (AS) alipokiona kiti cha enzi cha Malkia Bilqis kimewekwa mbele yake: Akasema: Haya ni katika fadhila zake Mola wangu Mlezi, ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru, kwa hakika, anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake; na anaye kufuru, kwa hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi na Karimu.

Alhamdulilahi

 

 

Imenukuliwa kutoka kwa Imam Ja’afar Swadiq AS kwamba: Katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani, kufru imekuja kwa maana tano ambapo moja ya maana hizo ni kukufuru neema na kisha akaashiria maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo ni hekaya na kisa cha Nabii Suleiman.  

Kukufuru neema huwa chanzo cha kuondoka neema ambazo mwanadamu ameruzukiwa na Allah. Hii ni kutokana na kuwa, Mwenyezi Mungu ni Mwenye Hekima na mambo yote anayoyafanya ni kwa mujibu wa hekima na maslahi. Hivyo basi hampatii kitu mtu bila ya sababu kama ambavyo pia hampokonyi mtu kitu pasina ya sababu.

Hata hivyo wale ambao hawashukuru kwa neema walizopatiwa na wanazikufuru, kwa hakika hawalaiki na kustahiki neema za Mwenyezi Mungu, na hekima ya Mwenyezi Mungu inalazimu kupokonywa neema hizo. Mkabala na wanaokufuru neema, kuna waja washukurivu ambao hushukuru neema za Allah kwa ndimi zao na kusema: Sisi ni waja wenye kuthamini neema Zako, hivyo tuongezee neema.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Kukufuru neema huwa sababu ya kuondoka neema na kushukuru ni sababu ya kudumu na kuendelea neema.

Kadhalika Imam Swadiq AS amesema: Endapo mtashukuru neema zitabakia na kudumu na mkizikufuru zitaisha. Kukufuru neema ni miongoni mwa madhambi ambayo adhabu yake hutekelezwa haraka na hapa hapa duniani. Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS anasema: Adhabu ya haraka zaidi ni ya kukufuru neema.

Aidha Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa, adhabu za dhambi tatu ni za haraka na hapa hapa duniani, na si zenye kucheleweshwa hadi katika ulimwengu wa akhera: Moja ni kuwaudhi kwa maneno na vitendo wazazi wawili (baba na mama), pili, kuwadhulumu watu na tatu ni kukufuru neema na kutoshukuru.

Kukufuru neema na kutushukuru neema za Allah humfanya mhusika asiwe mshukurivu pia mbele ya watu wengine. Mtu wa aina hii hujiona kuwa kila anachofanyiwa na watu wengine ni jukumu la watu hao kufanya hivyo na hivyo kwa namna moja huwa ni mdai. Katika mazingira kama haya, watu humchukia na kwa utaratibu huo hukumbwa na hali ya kutengwa kijamii na kutokuwa na rafiki wala mtu wa kumsaidia au kusuhubiana naye. Taba’ani, aina hii ya muamala chimbuko lake ni udhalili, uduni na shakhsia ya mtu mwenyewe.

Imam Hassan al-Mujtaba AS amenukuliwa akisema: Udhalili na uduni ni kutoshukuru neema.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa tukutane tena wiki ijayo.

 

Tags