Jan 17, 2019 02:43 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 17 Januari, 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Jamadil Awwal 1440 Hijria sawa na Januari 17 mwaka 2019.

Miaka 10 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni maghasibu walilazimika kutangaza usitishaji vita baada ya jeshi la utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya kinyama ya siku 22 dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. Katika mashambulizi hayo, utawala wa Kizayuni ulikusudia kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas au kwa uchache kuilazimisha harakati hiyo ikubali mazungumzo eti ya mapatano. Hata hivyo uungaji mkono wa Wapalestina kwa harakati ya Hamas na vilevile malalamiko makali ya walimwengu dhidi ya jinai za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, yaliulazimisha utawala haramu wa Israel usitishe mashambulio yake.

Ukanda wa Gaza

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa chini ya uongozi wa Marekani vilizishambulia ngome za wanajeshi wa Iraq huko Kuwait na Iraq ili kukomesha kukaliwa kwa mabavu Kuwait na jeshi la utawala wa Saddam. Mgogoro huo ulianza tarehe Pili mwezi Agosti mwaka 1990 baada ya utawala wa zamani wa Iraq kuikalila kwa mabavu ardhi ya Kuwait. 

Kundi la kwanza la askari wa Marekani laingia Saudi Arabia.

Katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, Sayyid Mahdi Hakim aliyekuwa mjumbe muhimu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq na mwana wa Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu aliuawa shahidi na makachero wa utawala wa Saddam Hussein dikteta wa zamani wa Iraq, huko Khartoum mji mkuu wa Sudan. Sayyid Mahdi Hakim alikuwa mmoja wa wanafunzi wa shahidi Ayatullah Sadr na mmoja wa wapinzani wakuu wa utawala wa Saddam Hussein.

Sayyid Mahdi Hakim

Miaka 58 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliuawa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Mwanamapinduzi huyo shujaa aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."

Patrice Lumumba

Katika siku kama ya leo miaka 63 iliyopita yaani tarehe 27 Dey 1334 Hijria Shamsia, Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.

Navvab Safavi

Tarehe 17 Januari miaka 159 iliyopita, alizaliwa Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa Urusi. Chekhov alizaliwa katika familia ya kipato cha chini na kupitia matatizo mbalimbali. Pamoja na hayo Anton Chekhov alifanya bidii kubwa ya masomo hususan katika fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Moscow na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Akiwa kijana alipendelea sana masuala ya uandishi na kuanza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na wa makala tofauti za wakati huo. Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na hivyo kutokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari" na vitabu vingine kadhaa. Anton Chekhov alifariki dunia nchini Ujerumani mwaka 1902 Miladia. 

Anton Chekhov

 

Tags

Maoni