Mar 21, 2019 03:56 UTC
  • Alkhamisi tarehe 21 Machi 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 14 Rajab 1440 Hijria sawa na Machi 21 mwaka 2019.

Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1398 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni kama Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 (yaani tarehe Mosi Farvardin) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita yaani tarehe 14 Rajab mwaka wa pili Hijiria, kulijiri vita baina ya Waislamu na washirikiana wa Makka mwanzoni kabisa mwa kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu. Mapigano hayo ya kwanza ya Waislamu baada ya kusimamisha dola mjini Madina, yaliongozwa na Abdullah bin Jahsh Asadi, huku upande wa pili ukiongozwa na Omar bin al Hadhrami ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa Maquraish. Katika mapigano hayo Omar bin al Hadhrami aliuawa. Mapigano hayo yanajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Sariyyatu Abdullah bin Jahsh.

Siku kama ya leo miaka 251 iliyopita inayosadifiana na 21 Machi 1768, alizaliwa Joseph Baron Fourier mwanahisabati na mwanafizikia mashuhuri wa Ufaransa. Baron Fourier alikuwa ni miongoni mwa wahadhiri wa mwanzoni kabisa waliofundisha somo la hesabati mara baada ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Paris.

Joseph Baron Fourier

Katika siku kama hii ya leo miaka 94 iliyopita barua rasmi za serikali ya Iran zilianza kuandikwa kwa kutumia tarehe ya mwaka wa Hijria shamsia kufuatia azimio lililopasishwa na Bunge la Taifa. Kwa utaratibu huo kalenda ya Iran ilibadilika kutoka mwaka wa Hijria Qamaria na kuwa Hijria Shamsia. Mwanzo wa miaka hiyo miwili ya Qmaria na Shamsia ni mmoja yaani hijria na tukio la kuhama Mtume (saw) kutoka Makka na kwenda Madina katika mwaka wa 13 baada ya kupewa utume (mwaka 622), lakini mwaka wa Qamaria unahesabiwa kwa kuzunguka mwezi mara 12 kandokando ya sayari ya dunia, na mwaka wa Shamsia unahesabiwa kwa dunia kuzunguka jua mara moja. Kwa kuwa mwaka wa Hijria Shamsia una siku365, kila mwaka huwa na siku 11 Zaidi ya mwaka wa Hijria Qamaria ambao huwa na siku 354.

Miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku ya mauaji ya umati dhidi ya wazalendo weusi nchini Afrika Kusini yaliyotokea mwaka 1960 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Kufuta Ubaguzi wa Rangi". Waafrika weusi wapatao 69 waliuawa na wengine 180 kujeruhiwa katika siku kama ya leo, baada ya askari makaburu kuwafyatulia risasi watu hao waliokuwa wakiandamana kwa amani huko Sharpeville nchini Afrika Kusini kupinga siasa za ubaguzi wa rangi.Japokuwa sera za ubaguzi wa rangi zimefutwa nchini Afrika Kusini lakini ubaguzi na ukosefu wa usawa vingali vinashuhudiwa nchini humo katika sura mbalimbali.

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano makubwa kati ya harakati ya PLO ya Palestina na majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Karama ulioko Jordan. Kwa uchache wanajeshi 1,230 wa Kizayuni waliangamizwa na makumi ya vifaru kutekelezwa au kuchukuliwa ngawira na wanamapambano wa Kipalestina kwenye mapigano hayo. Harakati ya PLO ilianza kupoteza hadhi yake ya kimapambano baada ya kulegeza misimamo yake ya kimapinduzi mwaka 1991 na kukubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya amani na utawala ghasibu wa Israel; mazungumzo ambayo hayajawa na matunda yoyote kwa wananchi wa Palestina.

Tarehe 21 Machi 1990, nchi ya Namibia ilipata uhuru kutoka kwa Afrika Kusini. Mwishoni mwa karne ya 19, wakoloni wa Kijerumani, Uingereza na Ureno walianza kuvutana kwa minajili ya kudhibiti na kupora utajiri na maliasili za Namibia. Uhuru wa Namibia ulipatikana kutokana na mapambano ya harakati ya SWAPO chini ya uongozi wa Sam Nujoma.

Bendera ya Namibia

 

Tags