Aug 18, 2019 02:25 UTC
  • Jumapili tarehe 18 Agosti mwaka 2019

Leo ni Jumapili tarehe 16 Dhulqaada 1440 Hijria sawa Agosti 18 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, baada ya vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq, hatimaye Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi kusimamishwa vita hivyo kwa mujibu wa moja ya vipengee vya azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la umoja huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, madola yanayopenda kujitanua ambayo yaliona maslahi yao yamo hatarini hapa nchini yalianza kutekeleza njama mbali mbali ili kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran. Saddam Hussein kibaraka wa madola ya Magharibi na hasa Marekani, wakati huo akiwa Rais wa Iraq alitumiwa na Washington na kuanzisha vita vya miaka minane dhidi ya taifa la Iran akitumia visingizo visivyo na msingi wowote. Mwanzoni mwa vita hivyo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio la kutaka kusimamishwa vita hivyo, ingawa cha kusikitisha katika azimio hilo ni kwamba, baraza hilo halikuashiria hata kidogo uchokozi wa majeshi vamizi ya Iraq dhidi ya taifa la Iran.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Agosti 1964, Afrika Kusini ilipigwa marufuku kushiriki kwenye mashindano ya 18 ya Olimpiki yaliyofanyika Tokyo Japan, baada ya kukataa kulaani vitendo vyake vya ubaguzi wa rangi dhidi ya wazalendo weusi nchini humo. Uamuzi huo ulichukuliwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) baada ya kumaliza kikao chake huko Lausanne Uswisi. Ujumbe wa Afrika Kusini ulisusia kikao hicho. 

Siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, alifariki dunia Muhammad Ghaffari aliyekuwa na lakabu ya Kamal al-Mulk mchoraji mahiri wa Kiirani. Alisoma katika skuli ya Darul Funun ya Tehran na kupata mafanikio makubwa katika fani ya uchoraji aliyokuwa akiipenda. Kipindi fulani Muhammad Ghaffar alifanya kazi katika utawala wa Nasseruddin Shah Qajar na kufanikiwa kutengeneza athari zenye thamani kubwa za uchoraji.

Kamal al-Mulk

Siku kama ya leo miaka 1366 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.

Ramani ya eneo la Ajnadeen karibu na Palestina

 

Tags

Maoni