Sep 29, 2019 05:50 UTC
  • Ruwaza Njema (24)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Tunakukaribisheni tusikilize kwa pamoja sehemu hii ya kipindi mkipendacho cha Ruwaza Njema ambapo kwa leo tutazungumzia Hadithi nyingine za watukufu wetu wa kidini kuhusiana na tabia njema za Bwana Mtume (saw) ambapo sote Waislamu tumetakiwa na maandiko matakatifu ya Qur'ani Tukufu tuige na kumfuata Mtume huyo katika tabia na mienendo yake yote. Katika kipindi cha leo tutazungumzia tabia nyingine njema ya Mtukufu Mtume (saw) katika kulisha na kuwakirimu watu. Alimsifu mpendwa wake Shahidi Ja'ffar at-Tayyar bin Abi Talib (sa) kwa tabia hii njema. Sheikh mwema Ahmad al-Barqi amenukuu katika kitabu chake cha al-Mahasin Hadithi iliyopokelewa na Dawoud bin Abdallah bin Muhammad al-Ja'ffari, kutoka kwa baba yake kwamba: 'Mtume Mtukufu (saw) alikuwa katika moja ya vita vyake ulipopita karibu yake msafara huku akiwa anaswali. Msafara huo ulisimama kwa muda mbele ya masahaba zake na kuwauliza hali ya Mtume (saw). Watu waliokuwa kwenye msafara huo walimwombea dua Mtume na kumtukuza. Walisema: Kama hatungekuwa na haraka tungemsubiri, (hata hivyo) mfikishieni salamu zetu na hapo wakaondoka. Mtume (saw) (baada ya kumaliza swala) alipoyasikia hayo alikasirika na kuwaambia masahaba zake: Msafara unasimama mbele yenu, kunijulia hali na kisha kunitumia salamu halafu nyinyi hamuwakaribishi kwa chakula cha mchana?! Haingewezekana, kwa Ja'ffar (at-Twayyar) kuwa miongoni mwa kundi, halafu msafara upite mbele yake bila ya kula chakula chake!' – Yaani kama Ja'ffar angekuwa miongoni mwenu bila shaka jambo kama hili halingetokea.

 

Wapenzi wasikilizaji, mbali na Mtume (saw) kupenda kulisha na kuwakirimu watu lakini pia alichukua tahadhari kubwa kutotumia vibaya chakula na kuonyesha unyenyekevu mkubwa katika suala hilo. Tunasoma katika kitabu cha Sunan an-Nabii cha Allama Tabatabai akinukuu Hadithi ambayo imenukuliwa katika kitabu cha Waram kutoka kwa Abu Huraira kwamba alisema: 'Mtume na familia yake hawakuwahi kushiba kamwe kutokana na mkate wa ngano kwa siku tatu mfululizo, hadi alipoaga dunia. Naye Aisha ananukuliwa katika kitabu hicho hicho akisema: Kamwe Mtume (saw) hakuwahi kushiba kwa siku tatu mfululizo hadi alipoaga dunia. Kama angetaka angeshiba lakini alikuwa akiwafadhilisha wengine juu ya nafsi yake. Na katika kitabu hicho pia: Mtume (saw) hakuwa akiweka vyakula vya aina mbili mdomoni kwake kwa wakati mmoja. Kama ilikuwa ni nyama, haikuandamana na mkate, na kama ulikuwa ni mkate haukuandamana na nyama. Na katika kitabu hicho hicho pia: Kamwe vyakula vya aina mbili havikuwahi kuwekwa mbele ya Mtume (saw) ila alikula kimoja na kutoa sadaka cha pili.'

Na katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq kuna Hadithi inayosema: 'Ibn Khuli alimpa Mtume Mtukufu (saw) chombo kilichokuwa na asali pamoja na maziwa ndani yake. Mtume alikataa kunywa na kusema: Vinywaji viwili kwenye kinywaji kimoja (wakati mmoja) na vyombo viwili kwenye chombo kimoja?! Mtume (saw) akakataa kunywa na kusema: Siliharamishi hili lakini mimi ninachukia kujifaharisha na hatimaye kesho (siku ya Kiama) nihesabiwe kwa mambo ya ziada ya dunia, bali ninapenda kunyenyekea kwa sababu Mwenyezi Mungu humuinua kila anayemnyenyekea.'

 

Ndugu wasikilizaji, tunashuhudia mfano mzuri na wa kuvutia wa Imam Ali (saw) kumuiga kipenzi na Bwana wake, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) katika tukio linalofuata ambalo limenukuliwa na wanahistoria wakati wa kuaga kwake shahidi (as): 'Ulipoingia usiku wa kuamkia tarehe 19 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, na baada ya kuswali Magharibi na nawafil alizotaka, Imam Ali (as) alijiandaa kufuturu. Ilikuwa ni kawaida yake (as) kula chakula cha jioni usiku mmoja kwa Hassan, usiku mwingine kwa Hussein na usiku mwingine kwa Abdallah bin Ja'ffar (mumewe Zainab (as)), na wala hakuzidisha (hakula zaidi ya) matonge matatu ya chakula. Aliulizwa katika moja ya nyusiku za Ramadhani ni kwa nini alikuwa akila chakula kidogo hivyo naye akajibu: 'Amri ya Mwenyezi Mungu (kinaya ya mauti na shahada) itanifika hivi karibuni, na ninapenda kwenda kwa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa nina tumbo lililo tupu na lenye njaa. Binti yake, Ummu Kulthum aliweka mbele yake kitambaa cha chakula kilichokuwa na mikate miwili ya shayiri, chombo cha maziwa na chumvi. Akasema (as): Binti yangu! Umemletea baba yako mikate miwili na mchuzi kwenye sinia moja?! Kwani unataka nichukue muda mrefu (kuhesabiwa) mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiama? Mimi ninataka kumfuata ndugu yangu na mtoto wa ami yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Hakuwahi kukabidhiwa chakula cha aina mbili kwenye sinia moja hadi alipoaga dunia. Binti yangu! Hakuna mtu yoyote anayekula chakula kizuri na kitamu na kuvaa nguo nzuri na za kuvutia ila kusimama kwake mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Siku ya Kiama kutachukua muda mrefu. Binti yangu! Kuna hesabu katika halali ya dunia na adhabu kwenye haramu yake….!'

************

Katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq kuna Hadithi hii inayosema kwamba, 'akiwa safarini na masahaba zake, Mtume (saw) aliwaamuru wamchinje kondoo. Mmoja wao akasema: Mimi nitamchinja, mwingine akasema mimi nitamchuna ngozi, wa tatu akasema mimi nitamkatakata vipande na wa nne akasema, mimi nitampika. Hapo Mtume Mtukufu (saw) akasema: Na mimi nitakusanya (chanja) kuni. Masahaba wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tunaapa kwa baba na mama zetu! Usipate taabu. Sisi tutakufanyia kazi hiyo. Akasema: Ninajua; lakini Mwenyezi Mungu anachukia kuona mja wake akiwa na rafiki zake na kisha kujitenga nao. Hapo Mtume (saw) akasimama na akawa anakusanya kuni.'

Kutokana na Hadithi hii Mtume (saw) anaashiria hapa nukta hii muhimu kwamba, ushirikiano unapasa kuonyeshwa safairini kwa sababu safari hiyo huwa ni ya watu wote wanaoishiriki. Hivyo juhudi za kukidhi mahitaji ya safari zinapaswa kufanywa na wote wanaoshiriki safari hiyo.

************

Imam Swadiq (as) amepokelewa akisema katika Hadithi ambayo imenukuliwa katika Kitabu cha an-Nubuwwa: 'Siku moja mwanamke mmoja bedui mwenye matusi mengi - iliyeonekana kuwa na maradhi fulani - alipita pembeni ya Mtume Mtukufu (saw) ambaye alikuwa ameketi chini sakafuni huku akiwa anakula chakula. Mwanamke huyo akasema: Ewe Muhammad! Wallahi unakula na kuketi kama anavyofanya mtumwa. Mtume (saw) akamwambia: Ole wako! Je, ni mtumwa yupi mwingine ambaye ni mtumwa zaidi kuniliko mimi? Yule mwanamke akasema: Nimegee tonge la chakula unachokula. Mtume akammegea tonge na kumpa. Akasema: Hapana Wallahi! Ila kilichoko kinywani kwako. Hapo Mtume Mtukufu (saw) akatoa chakula kilichokuwa mdomoni kwake na kumpa mwanamke huyo, naye akakila. Aba Abdillah as-Swadiq (as) anasema: Hapo mwanamke yule hakuwahi kupata tena maradhi hadi alipoaga dunia.'

Na hatimaye tunasoma Riwaya inayofuata kuhusiana na msamaha na huruma kubwa aliyokuwa nayo Mtume (saw) hata kwa wakorofi na wajeuri. Anas bin Malik amepokelewa katika kitabu cha Makarin al-Akhlaq akisema: 'Nilikuwa nikitembea njiani na Mtume (saw)…….Hapo akafika bedui mmoja wa Kiarabu na kuvuta kwa nguvu joho alilokuwa amelivaa Mtume (saw). Nilipomtazama Mtume (saw) shingoni, niliona kuna alama iliyokuwa imeachwa hapo kutokana na makali ya mvuto huo. Kisha bedui huyo akasema: Ewe Muhammad! Toa amri nipewe sehemu ya mali ya Mwenyezi Mungu unayoimiliki. Mtume (saw) aligeuka upande wake, akacheka na kisha akatoa amri apewe kitu kidogo.'

 

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe sote taufiki ya kuweza kuiga na kufuata mfano mwema wa tabia na mienendo ya Bwana wetu Mtume Mtukufu (saw) katika maisha yetu ya kila siku……Allahuma Ameen.

Tunakushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, kwa kuwa pamoja nasi hadi muda huu. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaliwa yake Mwenyezi Mungu, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

Tags