Sep 29, 2019 06:01 UTC
  • Ruwaza Njema (26)

Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Hii ni sehemu ya 26 ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho huwa kinachambua baadhi ya Hadithi zinazohusiana na mienendo na tabia njema za Mtume Mtukufu (saw) kwa lengo la kutuwezesha na sisi tuzifuate tabia hizo kama tunavyotakiwa kufanya na kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Katika kipindi cha leo tutaona ni jinsi gani Mtume (saw) alikuwa akishukuru na kumdhikiri Mumba wake Subhanahu wa Taala. Karibuni

********

Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) amenukuliwa akisema: 'Mtume (saw) alikuwa amempanda ngamia wake wa kike safarini. Ghafla akawa ameteremka na kusujudu mara tano na kisha kumpanda tena ngamia wake. Aliokuwa nao safarini wakamuuliza: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Tumeona ukifanya jambo ambalo tulikuwa hatujawahi kukuona ukilifanya! Mtume akasema: Nam; Jibrili aliniteremkia na kunibashiria mambo kadhaa kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ni kutokana na hilo ndipo nikamsujudia Mwenyezi Mungu sijda ya shukrani kwa kila bishara aliyonibashiria.'

Na katika Hadithi inayofuata wasikilizaji wapenzi, tunashuhudia kwa namna ya kuvutia jinsi Maimamu watoharifu (as) walivyoiga na kumfuata Bwana wao al-Habib al-Mustafa (saw) katika jambo hilo la kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kila jambo analotufanyia.

Hashim bin Ahmar amenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Nilikuwa ninatembea na Abu al-Hassan al-Imam Musa al-Kadhim (as) katika moja ya viunga vya mji wa Madina ambapo ghafla alishuka kutoka kwenye kipandio chake na kusujudu kwa muda mrefu sana. Aliinua kichwa chake na kisha kukipanda tena kipandio chake. Nikasema: Umerefusha sana sijda yako! Akasema: Hakika nimekumbuka neema ambayo Mwenyezi Mungu alinineemesha kwayo, nami nikaona ni vyema nimshukuru.'

 

Wapenzi wasikilizaji, tunaendelea kubakia kwenye kitabu hichohicho cha al-Kafi ili tupate kuelimika zaidi na sira ya Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw) kuhusiana na ibada ya kushukuru ambayo ni ibada bora zaidi. Thiqatul Islam al-Kuleini amemnukuu Abu Ja'ffar al-Imam al-Baqir (as) katika kitabu hicho akisema: 'Usiku mmoja Mtume (saw) alikuwa nyumbani kwa Bibi Aisha naye akamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni kwa nini unajitaabisha hali ya kuwa Mwenyezi Mungu tayari amekwishakusamehe dhambi zako zilizopita na zitakazokuja baadaye? Mtume (saw) akamjibu: Ewe Aisha! Je, nisiwe ni mja anayeshukuru? Akasema: Na Mtume (saw) alikuwa akisimama kwenye ncha za vidole vya miguu yake; hapo Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha Aya hii: 'Twaha. Hatukukuteremshia Qur'ani ili upate mashaka.'

Na katika kitabu cha al-Kafi pia kumenukuliwa Hadithi nyingine kuhusiana na suna za Mtume (saw) katika kushukuru. Abu Abdallah, al-Imam as-Swadiq (as) anasema: 'Mtume (saw) alipokuwa akifurahishwa na jambo fulani alikuwa akisema: 'Alhamdulillah kwa neema hii, na alipofikwa na jambo lililomuhuzunisha alikuwa akisema: Alhamdulillahi katika kila hali.'

Na tunasoma katika kitabu cha Sunan an-Nabii cha Allama Tabatabai ambapo Imam Ali (as) amenukuliwa akisema: 'Mtume (saw) aliposahau jambo, alikuwa akiweka paji la uso wake kwenye kiganja cha mkono wake na kisha kusema: Allahumma! Hamdu zote ni zako, ewe mkumbushaji wa kila jambo na mtendaji wake (halisi)! Nikumbushe nilichokisahau. Na kila mara alipokuwa akitazama kwenye kioo, alikuwa (saw) akisema: Hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye alikamilisha umbo langu na kuboresha sura yangu. Amenipa kile ambacho hakuwapa wengine, ameniongoza kwenye Uislamu na kunineemesha kwa Utume.'

 

Wapenzi wasikilizaji, tunasoma katika kitabu hichohicho cha Sunan an-Nabii cha Allama Muhammad Hussein Tabatabai (MA) ambaye pia ameandika kitabu mashuhuri cha tafsiri ya Qur'ani Tukufu cha al-Mizaan akimnukuu Ahmad bin al-Fahd kwamba alisema: 'Mtume (saw) alipokuwa akiomba dua alikuwa akinyanyua juu mikono yake kama anavyofanya masikini anayeomba chakula.'

Na kitabu cha Ghawali al-La'ali, kinasema: 'Mtume (saw) alipopanda kipandio chake akiwa ameazimia safari, alikuwa kisema 'Allah Akbar' mara tatu na kisha kusema: ' Ametakasika aliyemfanya huyu (mnyama/kipandio) atutumikie, na tusingeliweza kufanya haya wenyewe. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu. Allahumma! Katika safari hii tunakuomba utujaalie tuweze kutenda mema na kuwa na takwa, na kufanya matendo yanayokuridhisha. Allahumma! Turahisishie safari hii na utufupishie urefu wake! Allahumma! Wewe ni msaidizi wetu kwenye safari na khalifa (mlinzi) wetu kwenye familia (nyumba) zetu. Allahumma! Ninajikinga na kukukimbilia Wewe katika machungu na mashaka ya safari, huzuni ya nyumbani na kuona mabaya kuhusiana na familia na mali.' Na Aliporejea kutoka safarini alisema: 'Tumerejea nyumbani kwetu hali ya kuwa tunamwomba toba Mwenyezi Mungu, tunamuabudu na kumshukuru.'

*********

Wasikilizaji wapenzi, tunasoma pia katika kitabu cha Sunan an-Nabii cha Allama Tabatabai akisema kwamba imepokelewa katika kitabu cha Iqbal kuwa: 'Mtume (saw) alipokula tonge la chakula alikuwa akisema: Allahumma! Hamdu zote ni zako; umetupa chakula, kinywaji na kutuvunjia kiu. Hivyo tunakushukuru bila kukupuuza, kuachana Nawe wala kutokuwa na haja Nawe.'

Na Imam Ali (as) amepokelewa akisema katika kitabu cha al-Majalis: 'Mtume alipoona tunda jipya alikuwa akilibusu, kuliweka kwenye macho yake mawili na kwenye midomo (lips) yake na kisha kusema: Allahumma! Kama ulivyotuonyesha mwanzo wake tukiwa na afya nzuri tonyeshe pia mwisho wake tukiwa na afya nzuri.'

************

Na kwa Hadithi hiyo tukufu wasikilizaji wapenzi, ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni matumaini yetu kuwa mmenufaika vya kutosha na yale tuliyokundalieni kwa juma hili. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo siku na wakati kama huu,panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags