Nov 15, 2019 01:22 UTC
  • Ijumaa tarehe 15 Novemba 2019

Leo ni Ijumaa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 1441 Hijria sawa na Novemba 15 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1494 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake, Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Alipotimiza umri wa miaka 40, Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.

Siku kama hii ya terehe 17 Rabiul Awwal miaka 1358 iliyopita pia alizaliwa mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali. Imam Sadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani.

Siku kama ya leo miaka 389 iliyopita, alifariki dunia Johannes Kepler, mwanahisabati, mnajimu na mtaalamu wa nyota wa Kijerumani. Kepler alizaliwa mwaka 1517 na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Austria na kuanza kufundisha. Baadaye Kepler alifahamiana na Tycho Brahe, mnajimu mtajika wa Denmark na kuanzia hapo taratibu akavutiwa na elimu ya nyota kutoka kwa msomi huyo. Kepler alichunguza na kufanya utafiti katika uwanja huo kwa miaka mingi.

Johannes Kepler

Siku kama ya leo, miaka 150 iliyopita, alizaliwa Vasily Bartold, mustashiriki maarufu wa Russia huko mjini Saint Petersburg. Bartold alisoma na kuhitimu elimu katika chuo kidogo cha lugha za mashariki huko huko Saint Petersburg huku akiwa hodari katika lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kituruki. Akiwa na umri wa miaka 27 alifikia daraja la mhadhiri msaidizi katika chuo hicho ambapo alifundisha historia ya mataifa ya mashariki, huku akifanya pia utafiti na utalii mkubwa katika uwanja huo. Aidha kwa kipindi fulani alifanya safari huko Turkestani kwa minajili ya kuendeleza utafiti wake na kubahatika kuandika utafiti huo katika kitabu chake alichokipa jina la 'Turkestani katika kipindi cha mashambulizi ya Mongoli.'

Vasily Bartold

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, utungaji na upasishaji wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulikamilishwa na Baraza la Wataalamu. Katiba hiyo ilianisha na kuupasisha mfumo wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi ya mafunzo na matukufu ya Kiislamu hasa uadilifu katika jamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Baada ya katiba hiyo kupasishwa kulifanyika kura ya maoni ya wananchi wote na katiba hiyo ikapasishwa kwa wingi wa kura.

Tarehe 24 Aban miaka 40 iliyopita, siku chache baada ya kuvamiwa na kutekwa Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran, serikali ya Marekani katika radiamali yake kali dhidi ya hatua hiyo ya kimapinduzi, ilizuia fedha za kigeni za Iran katika mabenki yake yote duniani. Kufungwa kwa akaunti za Iran, kulipelekea mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua mkondo mpana zaidi. Siku chache kabla ya hatua hiyo, Iran ilikuwa imesimamisha uuzaji wa mafuta yake kwa Marekani kutokana na hatua na misimamo ya chuki ya Washington dhidi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

Wanafunzi wa vyuo vikuu wakivamia pango la ujasusi la Marekani, Tehran

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa, mfasiri mkubwa wa Qur'ani na msomi mashuhuri wa Kiislamu Allamah Muhammad Hussein Tabatabai akiwa na umri wa miaka 80. Mwanazuoni huyo mkubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa hodari sana katika elimu za falsafa, irfani, tafsiri ya Qur’ani na vilevile katika masuala ya fasihi, hisabati na fiqihi. Allamah Tabatabai ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni tafsiri ya Qur'ani ya al-Mizan.

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

Na katika siku kama ya leo miaka 19 iliyopita aliaga dunia Muislamu wa Italia, Mahdi Edoardo Agnelli. Edoardo Agnelli alikuwa mtoto wa kiume wa pekee wa seneta mashuhuri wa Italia na mmiliki wa kiwanda cha magari ya Fiat, Gianni Agnelli. Alizaliwa mwaka 1954 katika mji wa New York nchini Marekani na akahitimu chuo kikuu katika taaluma ya dini na falsafa za Mashariki. Alipokuwa na umri wa miaka 20, Edoardo Agnelli alipata kitabu cha Qur'ani kwa sadfa katika maktaba za Marekani na akaikumbatia dini tukufu ya Uislamu baada ya kufanya uchunguzi kuhusu dini hiyo. Alichagua jina la Hisham Aziz na baadaye kidogo alikhitari kufuata madhehebu ya Ahlulbait na kubadili jina lake na kuwa Mahdi Edoardo Agnelli. Miaka ya awali ya baada ya mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Edoardo Agnelli alifanya safari nchini Iran na kukutana na Imam Ruhullah Khomeini. Kusilimu mtoto huyo wa seneta wa Italia, mmiliki wa kiwanda cha magari ya Fiat na klabu ya soka ya Juventus kulitambuliwa kuwa kosa kubwa kwa familia yake kiasi kwamba alitishiwa kuwa atanyimwa urithi kwa kosa hilo. Alikuwa akisema mara kwa mara kwamba anahofia kuuliwa na Wazayuni. Hatimaye tarehe 15 Novemba mwaka 2000 maiti ya Mahdi Edoardo Agnelli ilikutwa chini ya daraja moja la mji wa Turin nchini Italia ikiwa na alama za kupigwa na kujeruhiwa. Maiti yake ilizikwa harakaharaka bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kubaini sababu ya kifo chake kilichotokea katika mazingira ya kutatanisha. 

Mahdi Edoardo Agnelli

 

Tags

Maoni