Dec 12, 2019 08:07 UTC
  • Alkhamisi tarehe 12 Disemba 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Rabiuthani 1441 Hijria wasa na Disemba 12 2019.

Tarehe 12 Disemba 1963, yaani siku kama hii ya leo miaka 56 iliyopita, Kenya ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Kenya ilianza kuvamiwa na Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20 na mwaka 1920 ikakoloniwa rasmi. Harakati ya wananchi iliyoongozwa na Jomo Kenyata ilipambana na wakoloni hao katika vuguvugu la kupigania uhuru dhidi ya Uingereza. Hatua ya wazungu hao wakoloni ya kuhodhi madaraka ya nchi na mivutano ya ndani vilikaribia kuitumbukiza Kenya katika mapigano ya ndani katika muongo wa 1950. Baada ya kupamba moto wimbi la kupigania uhuru la wazalendo wa Kenya, kulipasishwa katiba ambayo ilidhamini usawa wa watu wa rangi zote nchi humo. Nchi hiyo ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza tarehe 12 Disemba 1963 chini ya uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta na siku hii inajulikana kwa jina la Jamhuri Day au Siku ya Jamhuri.

Bendera ya Kenya

Miaka 118 iliyopita katika siku kama ya leo, kulianza ukurasa mpya katika historia ya mawasiliano ya mwanadamu baada ya kuzinduliwa mawasiliano ya njia ya mawimbi ya redio bila ya kutumiwa nyaya. Tukio hilo lilifanyika kwa kuwasiliana kwa maneno kutoka eneo moja la Italia kwenda jingine. Mtu aliyetumia mawasiliano ya aina hiyo kwa mara ya kwanza alikuwa mwanafizikia wa Italia Marconi ambaye baadaye alivumbua pia redio. Hii leo vyombo vya mawasiliano vinavyotumia mawimbi ya redio vinatumiwa katika masuala mengi duniani. 

Marconi

Na katika siku kama ya leo miaka 198 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Kifaransa, Gustave Flaubert katika mji wa Rouen nchini Ufaransa. Alipenda sana taaluma na fasihi akiwa bado kijana na kwa sababu hiyo aliacha masomo ya sheria, akaondoka Paris na kwenda kuishi maeneo ya vijijini. Wakati huo ndipo alipoandika vitabu vilivyompa umashuhuri mkubwa. Japokuwa Gustave Flaubert hakuandika vitabu vingi lakini athari na vitabu vichache vya mwandishi huyo vinahesabiwa kuwa vya aina yake katika taaluma ya fasihi duniani. Vitabu mashuhuri zaidi ya Gustave Flaubert ni Madame Bovary, Sentimental Education na Three Tales. Flaubert aliaga dunia tarehe 8 Mei mwaka 1880 akiwa na umri wa miaka 59.

Gustave Flaubert

 

Tags