Jan 22, 2020 14:50 UTC
  • Mtoto alizaliwa Iran, baada ya kiinitete (embryo) chake kuhifadhiwa kwa muda wa miaka 13

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

@@@

Mkuu wa Shirika la Anga la Iran Morteza Barari amesema Iran inafanya mazugumzo na nchi moja ya kigeni kwa lengo la kushirikiana katika kutuma wanasayansi katika anga za mbali. Barari amesema Shirika la Anga la Iran tayari limeshaanza ushirikiano wa awali na nchi hiyo ambayo amesema ni miongoni mwa nchi ambazo zimepiga hatua kubwa zaidi duniani katika kutuma wanasayansi katika anga za mbali. Barari hakuitaja nchi hiyo lakini amesema mkataba unakaribia kutiwa saini.

Aidha amesema lengo la Iran ni kutuma wanasayansi katika anga za mbali ili kushiriki katika miradi ya kimataifa na kwamba hatua hiyo itatangazwa katika mustakabali wa karibu. Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa inayojulikana kwa jina la Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009. Pia imetangaza kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanaadamu katika anga za mbali. Tayari mazoezi yameshafanyika kuhusiana na lengo hilo kwa kutumwa nyani hai katika anga za mbali ambaye alirejea ardhini akiwa salama. Mafanikio haya ya Iran yanajiri pamoja na kuwepo vikwazo vya kila upande vya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.

Wakati huo huo, Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Iran Jabbar Ali Zakeri amesema chuo hicho kimemaliza utengenezaji wa satalaiti inayojulikana kama Zafar. Aidha amesema satalaiti hiyo imeshakabidhiwa Shirika la Anga za Mbali la Iran kwa lengo la kurushwa katika anga za mbali katika kipindi cha miezi michache ijayo.

Amesema satalaiti ya Zafar imeundwa na wataalamu wa chuo hicho na ina uzito wa kilo 90 na ina kamera zenye uwezo wa kupiga picha za rangi. Aidha amesema satalaiti hiyo itakuwa na jukumu la kufanya utafiti kuhusu hifadhi za mafuta, madini, misitu na pia maafa ya kimaumbile.

@@@

Mwezi Disemba mwaka 2019, mtoto wa kike alizaliwa katika mji wa Isfahan kati mwa Iran, baada ya kiinitete (embryo) chake kugandishwa na kuhifadhiwa kwa muda wa miaka 13. Hii ni mara ya kwanza kwa kiinitete cha mwanadamu kugandihshwa kwa muda mrefu zaidi katika eneo la Asia Magharibi na kisha kuzaliwa bila matatizo.

Msichana huyo aliyepewa jina la Nafas alizaliwa Disemba 12 2019. Akizungumza na waandishi habari, Daktari Asadollah Kalantari ambaye ni mtaalamu wa ginekolojia amesema kuna idadi kubwa ya viinitete ambavyo vimegandishwa na kuwekwa katika benki maalumu. Anasema hivi sasa kuna viinitete zaidi ya nusu milioni kote Iran ambavyo vimehifadhiwa kwa niaba ya familia za Iran na pia za watu wa mataifa mengine duniani.

Agosti mwaka 2016, mwanamke mmoja kutoka Australia alijifungua mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 63. Mama huyo mwenyeji wa Melbourne alifaulu kujibebea ujauzito huo baada ya kutumia teknolojia ya kisasa ya kuhamisha kiinitete. Mama huyo alijaaliwa kujifungua mtoto wa kike baada ya kuchangiwa kiinitete hicho. Inasemekana kuwa bibi huyo alikuwa amejaribu sana kupata mtoto kupitia teknolojia ya kupandikiza mimba au IVF lakini bila mafanikio.

@@@

Mapema mwezi Januari Iran ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Sekta ya Masoko ya Kidijitali na Mashirika ya Kiteknolojia. Kongamano hilo limefanyika kwa lengo la kuarifisha teknolojia za kisasa katika mbinu za kujipenyeza katika masoko. Wataalamu katika uga wa masoko ya kidijitali, mashirika ya kiteknolojia na wazalishaji huduma waliwasilisha mbinu za kisasa katika uga wa masoko ya kidijitali katika sera za uchumi, sayansi na tiba. Aidha washiriki  waliweza kubadilishana mawazo kuhusiana na mafanikio waliyoweza kupata katika sekta husika. Mkutano huo ulikuwa na washiriki 1,800 wakiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu, wakurugenzi wa mashirika na wanafunzi.

@@@

 

Wagonjwa wa saratani ya titi husasan katika nchi za kipato cha chini wamepata matumaini makubwa baada ya Shirika la Afya Duniani WHO kuidhinisha kutengenezwa dawa ya mfanano (biosimilar medicine ) ya gharama nafuu inayoitwa trastuzumab. Katika tangazo ambalo lilitolewa mara ya kwanza kati kati ya mwezi Disemba 2019, WHO inasema kuwa dawa hiyo ya gharama nafuu ni mfano wa dawa ambayo imekuwa ya gharama kubwa na sasa itapatikana kwa wanawake wanaougua saratani kote duniani.

Hii ni mara ya kwanza kwa WHO kuidhinisha uzalishaji wa dawa ya gharama nafuu kwa tiba dhidi ya saratani ya titi, ugonjwa ambao unakumba wanawake wengi duniani.

WHO inasema kuwa wanawake milioni 2.1 walipata saratani mwaka 2018 ambapo kati ya hao 630,000 walifariki dunia, na wengi wao ni kwa sababu ya kushindwa kupata matibabu.

Trastuzumab ilijumuishwa katika orodha ya WHO ya dawa muhimu mwaka 2015 kama tiba muhimu kwa takribani asilimia 20 ya saratani ya titi ambapo tayari imeonesha kutibu awamu za mwanzo za ugonjwa wa saratani na wakati mwingine hata hatua za mwisho.

Akizungumzia hatua ya WHO, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt. Tedros Ghebreyesus alisema ni hatua muhimu sana kuidhinisha Trastuzumab kuweza kufikia wanawake wote kokote ulimwenguni.

Amesema wanawake wengi hasa katika nchi masikini wanashindwa kupata matibabu kutokana na gharama kubwa ya dawa. Gharama halisi ya matibabu ya dawa hiyo kwa mwaka ni wastani wa dola elfu 20 ambapo itakayotengenezwa kufanana nayo itakuwa nafuu kwa asilimia 65.

Tayari uchunguzi umefanyika kuwa inatibu na inaweza kununuliwa hata na mashirika ya Umoja wa Mataifa na hata mashirika ya kitaifa.

Katika nchi tatu za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, utafiti ulifanyika kwa wanawake 1325 ambapo ilibainika kuwa wanawake 227 hawakuwa wameanza matibabu mwaka mmoja hata baada ya kubainika kuwa na saratani ilihali 185 walikuwa na saratani ya hatua ya 1 hadi ya 3. Wengi wao walisema hawawezi kutafuta tiba kutokana na gharama kubwa ya matibabu. Mwezi Julai mwaka 2018, WHO  ilizindua mradi muhimu wa kupanua wigo wa kuidhinisha dawa za matibabu zinazotokana na vyanzo vya kibayolojia au vitu vingine vyenye uhai, au Biotherapeutic kwa lengo la kupunguza gharama za dawa hususan kwa nchi zinazoendelea.

Dawa hizi hutengenezwa kwa kutumia chanjo za matibabu, damu, jeni na tishu pamoja na vitu vingine na kwa hivyo Trastuzumab ni dawa ya kwanza ya mfanano kutokana na mradi huo kifani. Wanasayansi wa Iran wanatumia mbinu ya vitrification, ambayo ni ya kisasa zaidi duniani, kugandisha viinitete.

@@@

Naam wapenzi wasikilizaji hadi hapo tunafika mwisho wa Makala yetu ya Sayansi na Teknolojia. Shukran kwa kujiunga nasi. Hadi wakati mwingine panapo majaaliwa yake Mola, Kwaherini.

 

Tags