Jan 22, 2020 14:55 UTC
  • Iran yazindua dawa ya Edaravone Alsava ya kutibu Sklerosisi ya kimiotrofia ya pembezoni (ALS)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika Makala hii ambayo huangazia matukio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa nami hadi mwisho.

@@@

Shirika moja la Iran limezindua utengenezaji wa dawa inayojulikana kama Edaravone Alsava kwa ajili  ya wagonjwa wanaougua Sklerosisi ya kimiotrofia ya pembezoni -kwa Kiingereza Amyotrophic lateral sclerosis, kifupi ALS. Ugonjwa huu pia hujulikana kama Ugonjwa wa Lou Gehrig na ugonjwa wa Charcot, ni hali inayohusisha kuharibika kwa nyuroni. Barani Ulaya jina linalotumiwa ni ugonjwa wa nyuroni mota (MND). ALS hubainishwa kwa misuli migumu, kushtuka kwa misuli na udhaifu unaokithiri kutokana na kupungua kwa ukubwa wa misuli. Hii hupelekea ugumu katika kuongea, kumeza na hatimaye kupumua.

Ili kukabiliana na ugonjwa huo,  wanasayansi wa Iran wamefanikiwa kutengeneza dawa hiyo ya Edaravone Alsava. Dawa hiyo ilizinduliwa Januari 12 katika sherehe iliyohudhuriwa na Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya teknolojia Dkt. Sorena Sattari. Ugonjwa wa ALS huathiri watu walio na umri wa miaka 60 kwenda juu na katika visa vya kurithiwa katika umri wa miaka 50. Kwa mujibu wa takwimu muda wa wastani wa kuishi waliopata ugonjwa huo ni miaka mitatu hadi mine baada ya kuupata. Wengi hufariki kutokana na matatizo ya kupumua. Kwa msingi huo dawa iliyotengenezwa na wanasayansi Wairani itatoa mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya watu wengi duniani.

@@@

Vikwazo vya kidhalimu vya Marekani vimepelekea wagonjwa wanaougua magonjwa maalumu na nadra kupoteza maisha na wengine wengi wako katika hatari ya kupoteza maisha. Kwa mujibu wa Kianoush Jahanpour msemaji wa Mamlaka ya Dawa na Chakula Iran, wagonjwa wanaougua ugonjwa wa MPS (Mucopolysaccharidosis) nchini Iran wanakaribia kumaliza dawa zao kutokana na vikwazo vya Marekani. Amesema dawa hizo nadra za MPS zinatengenezwa na shirika ambalo liko Marekani lakini kutokana na vikwazo vya utawala wa Donald Trump, shirika hilo halijaweza kuuzia Iran dawa hizo. Amesema tayari waziri wa afya Iran ameshamuandikia barua mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani ambapo amekosoa sera za Marekani za kutumia vikwazo kuzuia dawa muhimu kuwafikia wagonjwa wa MPS nchini Iran. Aidha amesema mashirika ya Korea Kusini ambayo yanatengeneza dawa hiyo yameshindwa kufanya biashara na Iran kutokana na kuhofia vikwazo vya Marekani.

Mwezi Disemba mwaka 2019, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takht-Ravanchi alihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni haramu, na ni kinyume cha maadili na ubinadamu. Alisema vikwazo hivyo vya Marekani vinalenga kuwaadhibu wananchi wa Iran jambo ambalo linakatazwa hata katika wakati wa vita. Katika hotuba yake hiyo, Majid Takht-Ravanchi alitoa mfano na kusema shirika moja la Ulaya limeshinikizwa na Marekani ili kuacha kuiuzia Iran dawa maalumu na hivyo kuwasababishia wagonjwa masaibu makubwa. Amesema katika mji wa Ahvaz kusini mwa Iran, mtoto aliyekuwa na umri wa miaka miwili kwa jina la Ava, ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa Epidermolysis Bullous kwa kifupi EB aliaga dunia. Ugonjwa wa EB ni ugonjwa wa ngozi kwa watoto. Ngozi ya watoto wenye ugonjwa huu hubanduka mara kwa mara na hivyo wanahitaji bendeji maalumu. Hivi sasa kutokana na vikwazo vya Marekani, mashirika ya Ulaya yamekataa kuiuzia Iran bedeji hizo. Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisema vikwazo vya Marekani vimepelekea watoto wasio na hatia kama Ava kuaga dunia. Alisema kisa cha Ava ni mfano tu wa watoto na watu wazima wenye magonjwa nadra na saratani wanavyokumbwa na masaibu huku wakipoteza maisha baada ya maumivu makali.  Mashirika ya Iran yanayonunua dawa au bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi hukumbwa na matatizo  ya kuhamisha pesa kwa njia ya benki.

Hivyo ni wazi kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimekiuka haki za binadamu na sheria zote za kimataifa.

@@@

Na Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO limesema mwaka uliopita wa 2019 unashikilia rekodi ya pili ya kuwa wenye joto kali zaidi duniani baada ya mwaka 2016.

Taarifa iliyotolewa Januari 15 imewasilisha tathimini ya kina ya hali ya joto kwa mwaka 2019 ambapo WMO inasema wastani wa joto katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015-2019) na miaka kumi iliyopita (2010-2019) vipindi na viwango vya joto vilikuwa vya juu katika historia.

Tangu miaka ya 1980 kila muongo umekuwa wa joto kali kuliko uliotangulia, na mwenendo huu unatarajiwa kuendelea kwa sababu ya ongezeko la joto hewani linalotokana na gesi ya viwandani.

Kwa mujibu wa wastani wa takwimu zilizokusanywa na kutumiwa kutoa tathimini hii kiwango cha joto cha kimataifa kwa mwaka 2019 kilikuwa nyuzi joto 1.1°C zaidi ya kiwango cha wastani kilichokuwa kati ya miaka 1850-1900, ambacho ndio kilitimika kuelezea wastani wa kiwango cha joto katika nyakati za kabla ya mapinduzi ya viwanda.

WMO inasema “Mwaka 2016 unasalia kuwa ndio mwaka uliokuwa na kiwango cha juu zaidi cha joto katika historia kwa sababu ya mchanganyiko wa matukio makubwa ya El Niño ambayo huwa yanaambatana na wimbi la joto kali na mabadiliko ya muda mrefu ya tabianchi.”

Katibu mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema “Wastani wa kiwango cha joto duniani umeongezeka kwa takribani nyuzi joto 1.1°C tangu nyakati za kabla ya mapinduzi ya viwanda na kiwango cha joto baharini kimefikia rekodi ya juu zaidi. Kwa kuzingatia hali ya hivi sasa, utoaji wa hewa chafuzi ya ukaa tunaelekea kwenye ongezeko la joto la nyuzi joto 3°C  hadi 5°C ifikapo mwisho wa karne hii.”

Mkuu huyo wa WMO amesema viwango vya joto ni sehemu tu ya hadithi hii. Mwaka uliopita na muongo uliopita imeelezwa kuwa ni ya kuyeyuka kwa barafu, kuongezeka kwa kiwango cha kina cha baharí, ongezeko la joto baharini, ongezeko la tindikali kwenye maji na majira mabaya ya hali ya hewa.

Shirika hilo linasema haya yote yamesababisha athari mbaya kwa afya ya ustawi wa binadamu na mazingira. “Mwaka 2020 umeanzia pale ulipoachia mwaka 2019 kwa matukio mabaya ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi. Australia ilishuhudia mwaka wenye joto kupindukia na kwenye ukame wa hali ya juu 2019 na kuwa mfano wa moto mkubwa wa nyika ambao uliathiri watu, mali zao, wanayama pori, mfumo wa maisha na mazingira “ alisema Bwana Taalas.

@@@

Naam wapenzi wasikiliza na hadi hapo ndio tunafikia mwisho wa makala yetu ya Sayansi na Teknolojia. Ni matumaini yangu kuwa umeweza kunufaika na niliyokuandalia.

 

Tags