Jan 27, 2020 04:19 UTC
  • Jumatatu, tarehe 27 Januari, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe Mosi Jamadithani 1441 Hijria sawa na 27 Janiari 2020.

Miaka 129 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Ilya alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Uhispania na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi pia. Ehrenburg alifahamika vyema nchini humo kama mwandishi wa hadithi na mwanahabari, khususan pale alipokuwa akiripoti matukio katika Vita vya Kwanza vya Dunia, vya Pili na vile vya ndani vya Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 vikiwemo vy "Tufani" na "Kuanguka Paris". Ilya alifariki dunia mwaka 1967.

Ilya Ehrenburg

Katika siku kama ya leo miaka 120 iliyopita mfamasia wa Kijerumani Felix Hoffmann alitengeneza dawa ya kwanza ya kutuliza maumivu. Dawa hiyo hii leo inajulikana kwa jina la Aspirin. Waingereza pia waliamua kutengeneza dawa hiyo katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya uingizaji dawa hiyo nchini Uingereza kusimamishwa. Mbali na kutuliza maumivu, Aspirin ina sifa nyingine kadhaa ambazo ni pamoja na kuzuia damu isigande na kuzuia mshtuko wa moyo.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini yalitiwa saini mjini Paris, Ufaransa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka minne. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Paris, Marekani ilikubali kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini. Japokuwa baada ya kutiwa saini makubaliano hayo vita kati ya Marekani na Vietnam Kaskazini havikusitishwa, lakini serikali ya Washington ililazimika kuondoa majeshi yake huko Vietnam Kusini baada ya kupata hasara kubwa za hali na mali. Makubaliano ya Paris yalikuwa pigo kubwa kwa siasa za uingiliaji kati na za kibeberu za Marekani nchini Vietnam ambazo zilianza kutekelezwa mwaka 1964.

Vita vyay Vietnam

Na katika siku kama ya leo miaka 24 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul Aziz Tabatabai Yazdi. Alizaliwa mwaka 1348 Hijria katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa mji huo akiwemo Atayullah Sayyid Abdul Aala Musawi Sabzavari, Sheikh Sadra Badkubeh na Sayyid Abul Qassim al Khui. Alielekea katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran mwaka 1354 Hijria Shamsia na kujishughulisha na kazi za uandishi na uhakiki. Alkuwa miongoni mwa wataalamu mashuhuri na wakubwa wa historia, hadithi, rijali na amefanya kazi kubwa ya kutayarisha faharasa ya Maktaba Kuu ya Haram ya Imam Ridhaa (as) katika mji mtakatifu wa Mahs'had na Maktaba ya Amirul Muuminin katika mji wa Najaf. Ayatullah Abdul Aziz Tabatabai Yazdi ameandika makumi ya vitabu vikiwemo vya Adhwaa A'ala al Dhari'a na al Mahdi fii al Sunna Annabawiyyah. 

Ayatullah Sayyid Abdul Aziz Tabatabai Yazdi

 

Tags

Maoni