Feb 09, 2020 08:07 UTC
  • Mafanikio ya Iran katika uga wa sayansi na teknolojia baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran wiki hii inaadhimisha mwaka wa 41 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na katika kipindi cha miongo minne iliyopita, kati ya mafanikio makubwa ambayo yameweza kupatikana ni ustawi wa kasi katika uga wa sayansi na teknolojia.

Kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kulijiri mabadiliko makubwa katika nyuga zote. Moja ya mafanikio yaliyopatikana ni ustawi wa nchi kielimu.

Sisitizo na uzingatiaji wa kipekee wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ulazima wa kustawi nchi kwa kasi ni jambo ambalo limepelekea Iran hadi sasa kuwa miongoni wa nchi bora duniani katika nyuga mbali mbali ambapo kwa mfano katika uga wa teknolojia na utafiti wa seli shina, Iran inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani na katika uga wa teknolojia ya nano inashika nafasi ya sita au saba duniani.

Hali kadhalika Iran imeweza kupata mafanikio makubwa katika uga wa anga za mbali. Katika utafiti wa anga za mbali na makombora ya masafa marefu, Iran imeweza kupata mafanikio ya aina yake.

Anton Evstratov ambaye ni mataalamu Mrussia katika masuala ya Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) anasema mafanikio ya wasomi Wairani katika uga wa roboti ni ya kushangaza: "Ushindi wa roboti zilizoundwa  katika Jamhuri ya Kiislamu katika mashindano ya kitaalamu ya kimataifa ni jambo linaloweka wazi ukweli huu."

Evstratov anaendelea kuashiria kushiriki wasomi Wairani katika miradi ya nishati ya nyuklia katika uga wa kimataifa na kusema: "Ustawi huu unaonyesha kuwa wataalamu Wairani wanaongoza katika nyuga mbali mbali za kisayansi katika uga wa kimataifa.

Katika uga wa tiba vile vile, Iran imeweza kupata mafanikio makubwa sana ambapo si tu kuwa huduma za afya zinazotolewa Iran zimeboreka sana baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979  pamoja na kuwepo vikwazo vya kidhalimu bali pia sasa matumaini ya kuishi yameongezeka, vifo vya kina mama na watoto vimepungua sana na idadi ya wanafunzi wanaohitimu katika vyuo vikuu vya kitiba imeongezeka kwa kasi, kuna ustawi katika mbinu mpya za matibabu na pia kuna mafanikio katika utengenezaji dawa kwa mujibu wa teknolojia za kisasa; na hayo yote yameiweka Iran miongoni mwa nchi bora duniani katika uga wa tiba.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatollah Sayyed Ali Khamenei akitembelea maonyesho ya sayansi na Teknolojia mjini Tehran Oktoba 8, 2019

Pamoja na kuwepo vikwazo na mashinikizo ya madola ya kibeberu na kiistikbari duniani, Iran imetegemea wasomi wa ndani ya nchi na jitihada za vijana wake wataalamu katika kufikia uwezo wa kukamilisha mchakato kamili wa fueli ya nyuklia. Katika uga wa sayansi na teknolojia ya nyuklia, hivi sasa Iran ni miongoni mwa nchi zilizostawi zaidi duniani.

Ustawi wa kisayansi wa Iran katika baadhi ya teknolojia umefanyika katika kipindi kifupi sana jambo ambalo limewashangaza wengi na hata vyombo vya habari vya kimataifa vimekiri ukweli huo.

Tovuti ya idgconnect katika taarifa iliyochapishwa Januari 19 2015 ilichapisha makala iliyokuwa na anwani ya " Nafasi ya Kisayansi ya Iran" iliyoandikwa na Andrew Brown na ilihusu kasi ya uzalishaji wa kisayansi nchini Iran. Makala hiyo ilisema: “Watu wa nchi za Magharibi wamezoea kusikia madai kuwa Iran ina silaha za nyuklia na kwamba imewekewa vikwazo vya kimataifa na sheria za kuibana. Kwa hivyo yamkini ikawa vigumu kwa Wamagharibi kusikia kuwa Iran inaongoza duniani katika ustawi wa utafiti wa kisayansi. Hata hivyo kwa wale ambao wamekuwa wakifuatilia mpango wa nyuklia wa Iran si jambo la ajabu kusikia habari hizo za ustawi.”

Mpango wa nyuklia wa Iran una malengo ya amani na Iran inaendeleza shughuli za kisayansi za kuimarisha mpango  huo kwa kutegemea wanasayansi wa ndani ya nchi.

Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran akizungumza kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Nyuklia sambamba na uzinduzi wa kituo cha tiba ya kinyuklia aina ya PET radio medicine ambacho kinatumia mfumo wa FDG alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi ya nne duniani na ya kwanza Asia Magharibi yenye teknolojia kama hiyo. Mradi wa majaribio wa isotope katika kituo cha  nyuklia cha Fordo utakuwa muhimu katika uga wa utafiti wa kistratijia nchini.”

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha kimataifa cha makala za kisayansi Scopus, Iran ni ya 17 duniani kwa kiwango cha uzalishaji makala za utafiti. Kituo hicho ni chenye itibari zaidi duniani katika uchapishaji makala za utafiti wa vyuo vikuu na huchunguza na kuziorodhesha nchi kwa mujibu wa makala za kisayansi.

Andrew Brown anasema kasi ya uzalishaji wa kisayansi nchini Iran katika nyuga mbali mbali ndio sababu ya ustawi wa Iran kisayansi. Anaongeza kuwa: “Kama sehemu nyingine yoyote, ustawi wa kasi katika uzalishaji wa kisayansi nchini Iran haujatokea kwa sadfa kwani serikali ya Iran inaunga mkono kwa kiwango kikubwa utafiti wa kisayansi na hutoa asilimia 75 ya bajeti yote ya utafiti wa kisayansi.”

Shlomo Maital, msomi wa ngazi za juu katika utawala wa Israel mnamo Januari 6 2016 aliandika makala katika tovuti ya Jerusalem Post kuhusu ustawi wa kasi wa Iran katika muongo uliopita na kuwaonya wakuu wa Israel katika makala hiyo kwa kuhoji: “Je, Iran itashinda vita vya teknolojia?

Shlomo Maital anasema mkuu wa wakati huo wa Idara ya Ujasusi katika Jeshi la Israel Herzl Halevi mnamo Oktoba 29 2016 alihutubu katika kikao cha siri cha Kitivo cha Uongozi cha Tel Aviv na kusema: “Ukiniuliza iwapo katika kipindi cha miaka 10 ijayo kutajiri vita baina ya Israel na Iran, jibu langu litakushangaza. Lazima nisema hapa kuwa hivi sasa tuko vitani na Iran; tuko katika vita vya kiteknolojia na Iran. Hivi sasa wahandisi wetu wako vitani na wahandisi Wairani na kila siku vita hivi vinaendelea kuwa vigumu na shadidi.”

Katika mahojiano na gazeti la Kizayuni la Haaretz, Herzl Halevi alisema: “Tokea wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi sasa, idadi ya vyuo vikuu na wanafunzi Wairani imeongezeka mara 20 katika hali ambayo katika kipindi hicho kiwango hicho Israel kilikuwa ni mara 3.5. Kuna idadi kubwa ya wanafunzi wa Iran wanaosomea taalamu za uhandisi, teknolojia na sayansi za msingi.

Shlomo Maital anasema hivi sasa kuna zaidi ya wanachuo milioni mbili katika taaluma  za uhandisi na sayansi za msingi nchini Iran hili likuwa ni ongezeko la asilimia 161 tokea mwaka 2004. Anakiri kuwa ustawi wa Iran kisayansi umeishangaza dunia. Msomi huyo wa Israel katika kujibu swali la ustawi wa kasi Kisayansi nchini Iran pamoja na kuwepo vikwazo vya kimataifa anasema: “Kichekesho ni kuwa vikwazo vya kiuchumi vya nchi za Magharibi vimewekwa ili kuishinikiza Iran lakini vikwazo hivyo sasa ni sababu kuu ya kasi ya uzalishaji wa kisayansi nchini Iran.”

Kiwanda cha utegenezaji dawa nchini Iran

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika ripoti iliyochapishwa na taasisi yake ya kisayansi iliyopewa anwani ya “Kuelekea 2030” limedokeza kuwa: “Vikwazo dhidi ya Iran ni changamoto ambayo imepelekea viongozi wa Iran waelekeze uchumi wa nchi hiyo kwenye uzalishaji elimu.” UNSESCO inasema Iran imestawi katika uga wa makala za kisayansi zinazohusiana na teknolojia ya nano na inashika nafasi ya saba duniani na kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 mashirika ya Iran yanayojihusisha na utafiti na ustawi (RD) yameongezeka zaidi ya maradufu.

Kuingia Iran katika kundi la nchi zilizostawi katika uga wa sanyansi mpya kama teknolojia ya nano ni kati ya mafanikio makubwa ya nchi hii baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo Iran ni ya saba katika uga huo. Katika sanyasi na teknolojia mpya vijana Wiarani wameweza kupata mafanikio makubwa duniani ambapo mara kadhaa wameshika nafasi za kwanza katika olimpiadi za kimataifa za kisayansi na nukta hiyo inaonyesha kuwa, pamoja na kuwepo vikwazo vya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya nchi yoyote, Iran imeweza kufanikiwa na kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya hotuba zake aliashiria mafanikio makubwa ya Iran kisayansi na kusema: “Haya mafanikio yote ya kisayansi, kijamii na kiufundi yamejiri wakati wa vikwazo. Hii ni nukta yenye umuhimu mkubwa. Walitufungia milango ya sayansi na teknolojia, walifunga njia zote na hawakutuuzia bidhaa tulizozihitaji na ni katika mazingira kama hayo tumeweza kustawi.

Ayatollah Khamenei katika kubainisha umuhimu wa ustawi huu sambamba na kukata kikamilifu utegemezi kwa Marekani anasema: “Adui anafuatilia kwa karibu matukio na harakati za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ana wasiwasi na hasira kubwa kutokana na kubadilika Iran kutoka kuwa nchi iliyobaki nyuma na tegemezi na kuwa nchi yenye taathira, ushawishi na yenye nguvu zinazoongezeka za kisiasa na kiulinzi.

 

Tags