Feb 16, 2020 02:45 UTC
  • Jumapili, tarehe 16 Februari, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 21 Mfunguo Tisa Jamaduth-Thani 1441 Hijria, sawa na tarehe 16 Februari 2020 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1057 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Jamaduth-Thani mwaka 384 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria, alifariki dunia Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi, malenga na mwanahistoria mashuhuri wa Waislamu. Tanukhi alikuwa na kipawa katika uga wa kuhifadhi mashairi na fasihi ambapo ameacha turathi ya mashairi. Aidha kwa muda mfupi Muhsin Bin Ali Tanukhi alikwea hatua za kielimu na kidini katika zama zake na kisha akajishughulisha na kazi ya ukadhi. Kitabu cha ‘Faraj baada sh-Shiddat’ kinachozungumzia matukio ya kihistoria na kijamii ya zama zake, ni miongoni mwa athari zilizoandikwa na msomi huyo. Aidha kati ya vitabu vyake vingine ni kitabu cha ‘Al-Masaajid’ ambacho kinazungumzia kwa kiasi kikubwa masuala ya akhlaqi.

Muhsin Bin Ali Tanukhi, mtaalamu wa fasihi na malenga 

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 16 Februari 1918 Miladia, Lithuania ilijitangazia uhuru wake baada ya kudhoofika Russia kutokana na kushiriki kwake katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kutokea mapinduzi nchini humo mwaka 1917.  Pamoja na hayo, Moscow iliendeleza mipango yake ya kuiunganisha tena Lithuania na ardhi za Umoja wa Kisovieti, ambapo mwaka 1940 ilifanikiwa kufikia lengo hilo. Ujerumani ya Kinazi iliikalia kwa mabavu Lithuania kwa zaidi ya miaka mitatu katika kipindi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Bendera ya Lithuania

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Februari 1946 Miladia, kwa mara ya kwanza kura ya veto ilitumiwa na mjumbe wa Urusi ya zamani katika Umoja wa Mataifa. Siku hiyo mwakilishi wa Urusi, alipinga moja ya mapendekezo ya Baraza la Usalama na hivyo kutumia kwa mara ya kwanza haki ya veto. Haki ya kura ya veto inayolalamikiwa na nchi nyingi za dunia, inamilikiwa na nchi tano tu wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambazo ni Marekani, Uingereza, Ufaransa, China na Russia. Mpango wa kutumia veto ulipasishwa na Marekani, Uingereza na Urusi ya zamani katika mkutano wa Yalta wa mwaka 1945. Tangu wakati huo kumekuwepo malalamiko ya kupinga kupewa nchi hizo tu kura hiyo ya veto hasa kwa kuzingatia kuwa, baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiitumia haki hiyo kwa malengo ya kisiasa.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita yaani tarehe 27 Bahman 1357 Hijiria Shamsia, idadi kadhaa ya viongozi wa utawala wa Kipahlavi walinyongwa baada ya kupatikana na hatia ya khiyana na kutenda jinai dhidi ya wananchi wa Iran. Licha ya kuwa kwa mtazamo wa wananchi Waislamu wa Iran jinai za viongozi hao wa utawala dhalimu wa Shah zilikuwa wazi na bayana, lakini kwa amri ya Imam Khomeini MA mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu kuliundwa Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu na kushughulikia kesi za viongozi hao waliokuwa wametiwa mbaroni na vikosi vya wananchi. Mmoja wa watu hao ni Nematollah Nassiri, mkuu wa shirika la ujasusi na usalama la Shah SAVAK ambaye aliongoza shirika hilo kwa kipindi cha miaka 13. Katika kipindi hicho aliwatia mbaroni maelfu ya wananchi wanamapambano wa Iran, na kisha kuwatesa na kuwaua.

 

Nematollah Nassiri

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Februari 1984, Sheikh Raghib Harb, Imam wa Swala ya Ijumaa katika kijiji cha Jibshit cha kusini mwa Lebanon na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon dhidi ya utawala ghasibu wa Israel aliuawa shahidi na vikosi vya utawala huo vamizi. Sheikh Raghib alikuwa mmoja wa wanazuoni wanamapambano amilifu kusini mwa Lebanon kabla ya kuuawa kwake shahidi aliwahi kutiwa mbaroni na makachero wa Wazayuni wavamizi kutokana na mapambano na wito wake wa kuwataka wananchi wasimame na kupambana na Wazayuni. Wakati wa kuzikwa mwili wa shahidi Sheikh Raghib Harb, kulitokea mapigano makali baina ya vijana wa kitongoji cha Jibshit na wanajeshi wa Israel ambayo yalipelekea kuuawa na kujeruhiwa idadi kadhaa ya Waislamu madhulumu wa Lebanon.

Sheikh Raghib Harb

Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, sawa na tarehe 16 Februari 1992, aliuawa shahidi katika shambulio la ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel Sayyid Abbas Musawi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, huko kusini mwa nchi hiyo. Shambulio hilo lilipelekea kuuawa pia watu kadhaa waliokuwa wameandamana naye akiwemo mke na mwanawe mdogo, pamoja na wasaidizi wake watatu. Shambulio hilo lilitokea wakati Sayyid Abbas Musawi alipokuwa akirejea nyumbani kutoka kwenye kumbukumbu za kuuawa shahidi Sheikh Raghib Harb aliyeuliwa na maafisa wa utawala huo miaka michache iliyopita kabla ya hapo. Sheikh Raghib Harb alikuwa mwasisi wa harakati za mapambano huko kusini mwa Lebanon. Hujuma hiyo iliamsha hasira kubwa za Waislamu kote ulimwenguni dhidi ya Israel. Hata hivyo madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, si tu kwamba, hayakulaani jinai hiyo bali pia yalijaribu kuihalalisha. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Abbas Musawi, Sayyid Hassan Nasrullah alichukua hatamu za kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah, na kutoa pigo kwa Israel mwaka 2000, baada ya kuyafukuza kwa madhila majeshi ya utawala huo katika ardhi za kusini mwa Lebanon.

Sayyid Abbas Musawi, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon

 

Tags

Maoni