Feb 16, 2020 07:56 UTC
  • Sibtain (Imam Hassan na Hussein) katika Qur'ani na Hadithi (1)

Al-Hassanan (Hassan na Hussein) katika Aya; (Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote) Allahumma waswalie al-Hassan wal-Hussein, waja, mawalii, wana wa Mtume wako, wajukuu wa rehema, na mabwana wa mabarobaro wa peponi, swala ambazo ni bora zaidi kuliko ulivyowaswalia watoto wa Manabii na Mitume wengine. Na Mswalie Muhammad na kizazi chake ambacho ni kiongozi na chenye baraka.

Assalaam Aleikum ndugu zangu watukufu, Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kusikiliza sehemu ya kwanza ya kipindi hiki kipya ambacho kitakuwa kikikujieni saa na siku kama ya leo kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kipindi hiki kitategemea Vizito Viwili yaanai Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume (saw) na watukufu wengine wa nyumba yake, katika kubainisha sifa na fadhila za Maimamu wawili watukufu al-Hassan na al-Hussein (as).

Tunaanza ndugu wasikilizaji, kwa kuashiria hapa nukta hii muhimu kwamba kila mtu anayesoma Qur'ani Tukufu na kuielewa vyema anatambua kuwa kitabu hiki kitakatifu kwa kawaida huashiria matukio mbalimbali bila kuyafafanua kwa undani na kwamba ni Hadithi na Riwaya ndizo huja zikafafanua mambo yaliyokusudiwa kwenye Aya za kitabu hicho cha mbinguni. Kwa mfano kuna Aya nyingi ambazo huzungumzia matukio tofauti katika historia ya Kiislamu bila kufafanua zaidi wala kutaja sababu za kuteremka Aya hizo. Bali kuna Riwaya ambazo zimepokelewa kutoka wa Mtume (saw) na watukufu wengine wa nyumba yake ambazo hufafanua makusudio ya Aya hizo na kuna vitabu na tafsiri nyingi tu za Qur'ani ambazo zimeandikwa na wasomi pamoja na wanazuoni wa Kiislamu zikiashiria Hadithi zinazofafanua mambo mengi ambayo hayajabainishwa kwa uwazi na Aya takatifu za Qur'ani. Hadithi hizo ndizo zinazowafanya Waislamu wote waafikiane kwamba Aya fulani iliteremka kwa ajili ya tukio, sehemu na mtu fulani.

**********

Wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, moja ya Aya hizo ambazo zilimteremkia Mtume Mtukufu (saw) na kukusudia watu iliowakusudia ni Aya mashuhuri ya Majina ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu  anasema: Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya (vitu) hivi ikiwa mnasema kweli. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyotufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hekima. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipowaambia majina yake alisema (Mwenyezi Mungu): Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mnayaficha? (al-Baqarah 31-33).

Wafasiri wengi wa Qur'ani Tukufu wamezungumzia kwa mapana na marefu makusudio ya Aya hizi tukufu na hasa kuhusiana na maana ya majina yaliyotajwa humo. Wamejadili na kutoa mitazamo mingi kuhusiana na majina ya vitu alivyofundishwa baba wa jamii ya wanadamu, Nabii Adam (as) na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala. Wamesema mambo mengi sana katika uwanja huo, ikiwemo kwamba Mwenyezi Mungu alimfundisha maana ya majina na lakabu za vitu pamoja na sifa zake. Hii ni katika hali ambayo Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai, mwandishi mashuhuri wa tafsiri ya Qur'ani ya al-Mizan anaona kwamba majina yaliyowekwa na Mwenyezi Mungu mbele ya Malaika ni viumbe wenye utukufu mkubwa ambao wamehifadhiwa na kuwekwa katika hali ya ghaiba kwa wanadamu mbele Yake. Mwenyezi Mungu aliteremsha majina ya viumbe hao duniani na kutokana na baraka ya nuru yao, akaumba vitu vyote vilivyomo mbinguni na ardhini kutokana na nuru hiyo. Na huenda tafsiri na maana hii, ndugu wasikilizaji, ikawa ndiyo inayokaribia zaidi ukweli wa mambo kutokana na ufafanuzi na ibara zilizotumika katika Aya hiyo. Majina hayo bila shaka ni yenye utukufu mkubwa na maalumu na ni kutokana na utukufu huo ndipo Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala akateremsha baraka zake na kuviumba viumbe vyote vilivyomo duniani. Kuhusiana na suala hilo wasikilizaji wapenzi huenda tukahitajia hapa jambo linalothibitisha tafsiri na mtazamo huu uliobainishwa na Allama Muhammad Hussein Tabatabai na bila shaka ili kupata thibitisho madhubuti tunahitajia tafsiri ya watu ambao Qur'ani yenyewe iliteremkia nyumbani kwao nao si wengine bali ni Mtume Mtukufu (saw) na Watu wa Nyumba yake (as). Hivyo endeleeni kuwa nasi baada ya kipande hiki kifupi cha kasida/mziki.

***********

Katika kitabu cha kuvutia kinachoitwa, Allawamiu' an-Nuraniyyati fi Asmai Ali wa Ahlu Beitihi al-Qur'aniyya, Sayyid Hashim al-Bahrani ananukuu Hadithi kutoka kwa Imam Ja'ffar (as) akisema katika kufafanua Aya hiyo ya Majina: 'Mwenyezi Mungu Mtukufu alimfundisha Adam majina ya Mahujja (viongozi wateule/makhalifa) wake, Mahujja wote wa Mwenyezi Mungu na kisha kuyawasilisha (wakiwa katika hali ya kiroho isiyo ya kiwiliwili) kwa Malaika na kuwaambia: Niambieni majina ya (vitu) hivi ikiwa mnasema kweli - Yaani ya kwamba nyinyi mnayo haki ya kupewa ukhalifa duniani kutokana na kusabihi kwenu na kumtukuza Mwenyezi Mungu  kumliko Adam. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyotufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hekima. Mwenyezi Mungu Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipowaambia majina yake - yaani Adam alipowaambia Malaika majina ya Mahujja (makhalifa wa Mwenyezi Mungu) – Wote walisimama kutokana na heshima kubwa aliyonayo mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na hapo wakawa wamejua (yaani Malaika) ya kwamba wao (yaani Mahujja) ndio walio na haki ya kuwa makhalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi (dunia) yake na Mahujja wake kwa viumbe wake.

Na maneno haya ya Imam Swadiq (as) wapenzi wasikilizaji yananasibiana na kuoana kikamilifu na Aya tulizotangulia kuzisoma kwa sababu kabla ya Aya hizo kuna maneno mengine ya Mwenyezi Mungu yanayosema: Na pale Mola wako alipowaambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyoyajua.

Hivyo suala hili limetubainikia wazi wapenzi wasikilizaji, ila tu kuna jambo moja ambalo halijabainishwa kwenye Aya hii tukufu nalo ni kuhusiana na kuwa je, ni majina yapi hayo na yaliwahusu watu gani? Imam Swadiq (as) anatubainishia wazi suala hili kwa kusema: 'Mwenyezi Mungu alipomuumba Adam, (Adam) aliwatazama, yaani Muhammad, Ali, Fatwimah, al-Hassan na al-Hussein (as) wakiwa upande wa kulia wa Arshi (ya Mwenyezi Mungu) na kuuliza: Ewe Mola! Ni nani hawa?! Akamjibu: Ewe Adam! Hawa ni wabora wangu na walio karibu yangu. Nimewaumba kutokana na nuru ya utukufu wangu na kuwapa majina yanayotokana na majina yangu. Akasema: Ewe Mola! Kwa haki uliyonayo kwao, nifundishe majina yao. Akasema: Ewe Adam! Wao ni amana kwako na siri katika siri zangu, asije akaijua mtu mwingine yoyote isipokuwa wewe, ila kwa idhini yangu….. Hivyo akawa amechukua agano kutoka kwake na kumfundisha majina yao na kisha kuyaweka mbele ya Malaika ambao hawakuwa wakiyajua. Akawaambia: Niambieni majina ya (vitu) hivi ikiwa mnasema kweli. Wakasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyotufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hekima. Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipowaambia majina yake, Malaika walitambua kwamba yeye ni mteule na amefadhilishwa kutokana na elimua liyokuwa nayo. Hapo wakaamrishwa kusujudu, ambapo sijda hiyo ilikuwa ni alama ya kuonyesha fadhila ya Adam na ibada kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu hiyo ilikuwa ni haki yake.'

Na kwa Hadithii hii ya Imam Swadiq wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa sehemu ya kwanza ya kipindi jiki kipya cha As-Sibtan yaani Maimamu wawili watoharifu al-Hassan wal Hussein (as) katika Qurani na Hadithi Tukufu. Hivyo tunakuombeni mjiunge nasi tena wiki ijayo kusikilize sehemu nyingine ya kipindi hiki, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags