Mar 26, 2020 07:13 UTC
  • Ujue ugonjwa wa COVID-19 (corona) na namna ya kujikinga

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika Makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.

 

Ugonjwa wa COVID-19 ambao pia ni maarufu kama corona umeenea kote duniani na katika siku za hivi karibuni nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Tanzania na Rwanda zimetangaza kuwepo waathirika wa ugonjwa huo katika nchi hizo na hivyo kumeanzishwa kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu ugonjwa huo. Katika sehemu ya kwanza ya kipindi chetu tutajaribu kuangazia kirusi hiki kwa kifupi.

Corona ni jamii kubwa ya virusi vinavyosababisha maradhi kwa wanyama na binadamu. Kwa binadamu, jamii kadhaa za virusi vya Corona vinafahamika kusababisha maambukizi kwenye njia ya hewa na mfumo wa upumuaji.  Maradhi yaliyowahi kusababisha madhara makubwa kutokana na virusi vya Corona ni pamoja na MERS na SARS yaliyozuka mwanzoni mwa miaka ya 2000. Kirusi cha Corona kilichogundulika hivi karibuni kinasababisha ugonjwa unaofahamika kama COVID-19.

Katika kufafanua, hapa tunaweza kusema kuwa COVID-19 ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Corona. Virusi hivyo vipya havikuwa vikifahamika hapo kabla na sayansi ya tiba. Na vilianzia nchini China mwezi Disemba mwaka 2019.

 

Wengi wanajiuliza kuhusu dalili za corona na ni vipi wanaweza kubaini iwapo wameambukizwa ugonjwa huo. Hapa, inatupasa kusema kuwa, dalili kuu za corona ni pamoja na homa kali, uchovu na kikohozi kikavu na zinatokea taratibu. Dalili kubwa na inayoweza kutia hofu, ni mtu kukosa pumzi. Lakini hilo lisikutishe, kwani kwa mujibu wa takwimu zilizopo, ni mtu 1 pekee kati ya watu 6 walioambukizwa virusi vya corona hufikia dalili hiyo ya hatari.

Shirika la Afya Duniani, WHO limebainisha watu ambao wako katika hatari ya kuambukizwa COVID-19.

WHO inasema wazee na watu wenye magonjwa sugu na ya kudumu kama shinikizo la damu, kisukari, matatizo ya figo ndio walio kwenye hatari zaidi ya kuathika pindi wanapopatwa na virusi vya corona. Aidha wataalamu wanasema watu wa umri wa wastani na wenye afya imara wanaweza kupata virusi vya corona na kupona.

Hatari ya kuambukizwa

Baada ya kubaini hapo wale ambao wako katika hatari ya kuambukizwa corona, ni muhimu sana kufahamu namna virusi vya corona vinavyosambaa.

Mwanadamu anaweza kupata Virusi vya Corona kutoka kwa mtu aliyeambukizwa. Virusi vinaweza kusambaa kupitia maji maji kutoka kwenye pua au mdomo wa aliyeathirika. Iwapo mtu anagusa maji maji kama mafua, mate na makohozi ya mtu aliye na virusi na kisha kujigusa mdomo, macho na pua anaweza kupata virusi vya Corona.

Kwa kuzingatia hayo, ni vipi tunaweza kujikinga na  virusi hivyo? Kwanza kabisa nawa vizuri na kila wakati mikono yako kwa maji ya vuguvugu, sabuni au dawa za kuua vijijidudu kwa angalau sekunde 20. Nukta ya pili ni kuwa unapaswa kukaa umbali wa angalau hatua mbili kutoka mtu anayepiga chafya au kukohoa. Nukta ya tatu ni kuwa unapaswa kuepuka kugusa macho, pua na mdomo kwa mikono isiyo safi kwa sababu mikono hushika sehemu nyingi na ni rahisi kubeba vimelea vya maradhi. Nukta ya nne ni kuwa uhakikishe wewe, na walio karibu yako wanazingatia ustaarabu wa kuzuia pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya. Nukta ya tano ni kubaki nyumbani ikiwa hujisikii vizuri. Iwapo una mafua makali, homa, kikohozi na kushindwa kuhema nenda hospitali kwa sababu huko wataalamu watakupatia msaada muhimu. Nukta ya sita ni kuwa unapaswa kuepuka kuwa sehemu yenye msongamano, kama vyombo vya usafiri, maduka na maeneo yenye mgandamizo wa hewa. Nukta ya saba ni kuwa ni vyema kuwa na kifunika mdomo na pua yaani maski na kukikavaa ukiwa kwenye mikusanyiko. Na nukta ya mwisho muhimu ambayo unapaswa kuzingatia ni kufuatilia taarifa za afya na matangazo yake kuhusu virusi vya corona.

Karantini

Wengi wanajiuliza ni kwa nini watu wanawekwa karantini wakati wanashukiwa kuwa na corona.

Kwa ufupi neno Karantini linamaanisha kuwa sehemu maalumu chini ya uangalizi. Watu wenye dalili au wanaotokea maeneo yenye maambukizi makubwa ya virusi vya corona hulazimika kuwekwa karantini (kutengwa na watu wengine) ili kufuatilia afya yao kwa karibu na kuzuia kueneza virusi. Ukiambiwa unapaswa kuwekwa Karantini, usiogope. Ni kwa ajili ya afya yako na ya wengine. Katika ugonjwa wa COVID-19 muda wa karantini ambao wataalamu wanashauri ni siku 14.

Tiba

Baada ya hayo yote swali ambalo wengi wanauliza ni kuwa je, virusi vya Corona vina tiba?

Hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya virusi vya Corona lakini kwa sababu virusi hivyo vinaleta dalili mfano wa zile za mafua makali, mchanganyiko wa tiba unatumika kupunguza athari za virusi vya Corona. Wataalamu wa nchi mbali mbali kama vile China, Iran, Ujerumani, Uswisi na Marekani wako mbioni kujaribu kutengeneza dawa au chanjo ya COVID-19 na inatazamiwa kuwa katika wiki zijazo kutakuwa na habari zenye kuleta matumaini.

Kwa kuzingatia kuwa hakuna dawa au chanjo ya corona, wengi wana hofu na wasiwasi kuhusu ugonjwa huo. Lakini weledi wa mambo wanasema hakuna haja ya kuwa na hofu.

Kilicho muhimu ambacho wataalamu wanashauri ni kuchukua tahadhari. Kila mtu duniani yuko kwenye uwezekano wa kupata virusi vya Corona lakini kama tulivyokufahamisha, athari zake bado hazitishi.

Na mwisho kabisa kumekuwa na tetesi au uvumi kuwa watu weusi hawawezi kupata Corona. Lakini ukweli ni kuwa , kama ilivyo kwa watu wa rangi na jamii zote, watu weusi au Waafrika pia wanaweza kuambukizwa virusi vya Corona. Kuna mifano kadhaa ya watu weusi walioambukizwa corona. Kwa mfano mgonjwa aliyepatikana na corona Kenya ni Mwafrika asili. Hivyo uvumi huo hauna msingi na la muhimu ni kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuvuka kipindi hiki kigumu.

Naam wapenzi wasikilizaji na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia ambapo leo tumeangazia ugonjwa wa COVID-19 au corona ambao unazidi kuenea kote duniani.

 

Tags