Apr 16, 2020 07:34 UTC
  • Iran yavumbua kifaa cha kugundua corona, wanafunzi Kenya waunda mashine ya kupumua + Video

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine. Ni matumaini yetu kuwa utakuwa nasi hadi mwisho.

Kwa mara ya kwanza duniani, Jamhuri ya Kislamu ya Iran imevumbua kifaa chenye uwezo wa kugundua mwili na sehemu kilipo kirusi cha corona katika umbali wa mita 100 tena katika kipindi cha sekunde chache tu. Kifaa hicho kimepewa jina la "Musta'an 110."

Kifaa hicho kilizinduliwa jana Jumatano kwa mara ya kwanza katika sherehe zilizohudhuriwa na Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, jeshi ambalo liko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya corona nchini Iran. 

Kamanda Mkuu huyo wa jeshi la IRGC amesema kwenye sherehe hizo kwamba, teknolojia hiyo mpya ina uwezo wa kugundua maeneo na watu walioambukizwa corona katika kipindi cha sekunde chache tu. Ni teknoljia mpya kabisa ambayo imevumbuliwa na wanasayansi wa jeshi la kujitolea la Basiji. Amesema, kifaa hicho kinatumia teknolojia mpya, ya kisasa na ya kipekee

Wataalamu wa IRGC wanasema kifaa hicho kipya hakihitajii kuchukua vipimo vya damu, bali kinaweza kugundua maeneo na watu walioambukizwa korona katika masaha ya hadi mita 100 na tayari kimeshafanyiwa majaribio mengi mahospitalini na kimekuwa na matokeo mazuri kwa asilimia 80. 

Akitoa ufafanuzi kuhusu kifaa hicho kipya, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC amesema, huu ni uvumbuzi mpya wa sayansi na teknolojia na ni wa kipekee. Ni teknolojia iliyovumbuliwa na wanasayansi wa jeshi la kujitolea la Basiji katika kipindi hiki kifupi cha kuenea corona humu nchini. Ni kifaa ambacho kinaweza kuongozwa kwa mbali na kinaweza kutumika si kwa ajili ya kugundua kirusi cha corona tu, bali pia jamii nyingine za virusi.

Aidha amesema chombo hicho kinatumika katika oparesheni za kupuliza dawa kwenye maeneo mbalimbali ili kuua virusi vya corona na hivyo hakutakuwa na haja ya kupuliza dawa katika maeneo yasiyo na  virusi.

Meja Jenerali Salami amesema chombo hicho kimefanyiwa majaribio katika mahospitali nchini Iran na uwezo wake wa kufanya kazi bila makosa ni asilimia 20 huku akiongeza kuwa watazidi kukiboresha ili kifanye kazi kwa njia bora zaidi.

@@@@

Mkuu wa Kituo cha Uhusiano wa Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya na Tiba ya Iran amesema kuwa tayari nchi hii imetengeneza kipimo cha antibodi yaani kinga ya mwili ya Covid-19 na kipimo cha haraka cha corona (rapid test) kwa ajili ya kutambua antibodi. Dakta Kianush Jahanpur ameandika katika mtandao wake wa Twitter kwamba kufuatia juhudi chungu nzima na ushiriki wa watafiti wa Kiirani hivi karibuni kipimo hicho cha kutambua kinga ya mwili (antibodi) ya covid-19 na kipimo cha haraka cha corona kitapatikana nchini.

Jahanpur ameongeza kuwa aina hii ya utambuzi wa haraka na wa gharama nafuu utarahisisha kutekelezwa marhala ya mchakato bora wa kutokaribiana katika wiki zijazo.

@@@

Tukiwa bado katika uga wa kukabiliana na corona nchini Iran, kiwanda kikubwa zaidi cha kutengeneza maski za kitiba eneo la Asia Magharibi kimezinduliwa katika Eneo la Kiviwanda la Eshtehard katika mkoa wa Alborz magharibi mwa Tehran. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha masiki milioni tatu kwa siku zikiwemo maski maalumu za N95 ambazo hutumiwa na wafanyakazi wa sekta ya afya.  Kiwanda hicho kimezinduliwa kwa kutegemea uwezo wa vijana wa Iran na mashirika ambayo msingi wake ni elimu yaani knowledge-based.

@@@

Mjadala mkali umeibuka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya serikali kukubali majaribio ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 au Corona. Raia wengi mjini Kinshasa walitupilia mbali pendekezo hilo na kuitaka serikali kurejelea hatua hiyo. Hatua ya serikali ya kuridhia kuendeshwa utafiti wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona nchini Congo imezua mjadala mkali hasa miongoni mwa  vijana. Kwenye mitandao ya kijamii raia wengi wametupilia mbali majaribio ya chanjo hiyo kuendeshwa nchini. Hiyo ni kufuatia matamshi ya kiongozi wa kamati ya kitaifa ya kupambana na ugonjwa wa Corona, Jean-Jacques Muyembe kuelezea kwamba Congo ni miongoni mwa nchi zilizochaguliwa ili kuanzisha majaribio ya chanjo dhidi ya Corona. Kwenye barua yao ya wazi kwa daktari Muyembe, mashirika ya kiraia yameeleza kwamba hakuwezi kuweko na chanjo ya majaribio pasina na mjadala wa kitaifa ili kuwashawishi raia. Bienvenu Matumo, mwanachama wa kundi la vijana kwa ajili ya mageuzi, LUCHA amesema kwamba chanjo ya majiribio ni lazima ianzie Ulaya au kwenye nchi zilizoathirika zaidi. Kufuatia mashinikizo ya wananchi, Dr Muyembe amebatilisha kauli yake na kusema hakutokuweko majaribio yoyote ya chanjo hadi hapo shirika la afya ulimwenguni litakapoidhinisha chanjo hiyo.

Mjadala huo umekuja baada ya watafiti wawili wa Ufaransa kupendekeza kuanzisha utafiti wa majaribio ya chanjo ya corona barani Afrika. Matamshi ya watafiti wawili wa Ufaransa ambao walielezea kwamba kabla ya kutumiwa nchini Ufaransa, chanjo hiyo ya majaribio inatakiwa kufanyiwa majaribio huko barani Afrika, yamewakasrisha sana watu wengi barani Afrika. Watafiti hao Wafaransa katika matamshi yaliyojaa dharau wamesema chanjo ya corona inapaswa kufanyiwa Waafrika hasa makahaba kwa sababu huwa wanawasiliana na watu wengi bila kinga. Waafrika wamekosoa vikali matamshi hayo na kuyataja kuwa mfano mwingine wa utumwa mambo-leo.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Gebreyesus aliyataja matamshi hayo kuwa ya kibaguzi na ya kikoloni. Gebreyesus aliendelea kusema kuwa, urithi wa tabia ya ukoloni unatakiwa kukomeshwa.

@@@

Mashine ya kupumua (ventilator) iliyoundwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta nchini Kenya wamefanikiwa kutegeneza mashine ya kusaidia kupumua ambayo ni muhimu kwa watu wanaougua ugonjwa wa COVID-19. Mashine hizo ambazo hutumika kuokoa wagonjwa mahutiti wa corona ni chache sana nchini Kenya na zote zilizoko huagizwa kutoka nje ya nchi.  Mashine hii hutekeleza jukumu la kupumua wakati ugonjwa huu unaposababisha mapafu kushindwa kufanya kazi. Mashine hiyo ya kupumua imetengenezwa na wanafunzi 16 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta mjini Nairobi na wametumia vifaa vya ndani ya nchi kiuunda. Mashine hiyo imeunganishwa na compyuta ambayo itawezesha madaktari kufuatilia kazi yake katika mwili wa mgonjwa.

Naibu Kansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta Profesa Paul Wainaina amesema chuo hicho kina uwezo wa kuunda mashine 50 za kusaidia kupumua kila wiki. Bernard Karanja, mmoja wa wanafunzi waliohusika katika mradi huo anasema waliamua kuunda ventilator baada ya kubaini kuwa kuna upungufu wa mashine hiyo katika nchi zote zenye idadi kubwa ya wanaoigua corona. Anaongeza kuwa kwa kuzingatia uhaba wa mashine hiyo duniani waliamua kuitengeneza chuoni hapo. Sasa Chuo Kikuu cha Kenyatta kinasubiri idhini ya wataalamu wa Wizara ya Afya ya Kenya kabla ya kuanza kuzalisha kwa wingi mashine hiyo ambayo moja itagharimu shilingi nusu milioni au takribani dola elfu tano.

@@@

Naam Wapenzi wasikilizaji na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia kwa leo, ni matumaini yetu kuwa mumeweza kunufaika na tuliyokuandalia. Hadi wakati mwingine panapo majaliwa yake Mola, Kwaherini.

Tags