Apr 16, 2020 07:42 UTC
  • Kenya yaunda kifaa cha kupima corona

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga na makala hii ambayo huangazia masuala ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utaweza kunufaika.

Jumatano tarehe 8 Aprili sawa na tarehe 20 Farvardin  ni "Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia" katika kutambua jitihada za kujivunia za wasomi wa nyuklia wa Iran katika kukamilisha mzunguko wa utengenezaji wa fueli ya nyuklia.

Wasomi na Wanasayansi wa Kiirani katika siku kama hiyo mnamo mwaka 2006 walifanikiwa kutengeneza mzunguko kamili wa fueli ya nyuklia katika maabara. Baada ya kutangazwa habari ya mafanikio hayo ya wasomi na wanasayansi Wairani katika urutubishaji urani na kuzinduliwa mchakato kamili wa urutubishaji urani kwa kutumia mashinepewa au centrifuge zilizoundwa nchini Iran, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA liliitangaza Iran kuwa miongoni mwa nchi ambazo zimeweza kumiliki teknolojia ya kurutubisha urani katika uga wa shughuli za nyuklia kwa malengo ya amani.

Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran alituma ujumbe kwa mnasaba wa Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia na kuashiria kuzinduliwa mafanikio mapya 122 ya taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yenye kutia matumaini ni mwanzo wa ukurasa mpya katika ustawi wa pande zote wa miradi ya kujivunia ya Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran. 

Salehi alibainisha kuwa katika hali ya vikwazo vya kidhulma vya uistikbari wa dunia dhidi ya Iran ya Kiislamu; Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran linalichukulia suala la kudhamini mahitaji ya kitiba kuwa jukumu la kitaifa na kiakhlaqi na kuongeza kuwa: Kuzidishwa pakubwa uzalishaji na huduma zinazohusiana na sekta ya matibabu ya kinyuklia na kuvidhaminia mahitaji ya dawa vituo vya tiba na afya hapa nchini Iran kunafanyika kwa kiwango cha juu na kwa kasi inayokubalika.  

Wakati huo huo, Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) imesema Tehran itaendelea kurutubisha urani kwa kiwango inachotaka, lakini inaweza kuangalia upya urutubishaji huo iwapo tu Umoja wa Ulaya utatoa dhamana ya kivitendo ya kuheshimu na kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa munasaba wa Siku ya Tenolojia katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran, kamati hiyo imesema kuwa, katika hali ambayo Umoja wa Ulaya umekuwa ukisisitizia udharura wa kuheshimiwa na kulindwa JCPOA, lakini umoja huo haujachukua hatua za kivitendo za kuonyesha kuwa unafungamana na mapatano hayo ya kimataifa. Ripoti hiyo ilieleza bayana kuwa, si Marekani wala Ulaya zimelipa gharama za hatua ya upande mmoja ya Rais Donald Trump ya kuindoa nchi yake katika mapatano hayo, bali pia Ujerumani, Uingereza na Ufaransa zimekuwa zikionyesha misimamo ya undumakuwili mkabala wa kitendo hicho cha Trump. Naye Behrouz Kamalvandi, msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran (AEOI) amesema lengo la shirika hilo ni kuongeza kiwango cha urutubishaji madini ya urani hadi kiwango cha Separative Work Unit (SWU) milioni moja.

@@@

Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya au 'Kenya Medical Research Institute' (KEMRI)  imetangaza kuanza kuunda kifaa cha kupima corona ambacho kinajulikana kama COVID-19 rapid test kit. Uundwaji wa kifaa hicho ni mchango mkubwa katika jitihada za serikali ya Kenya za kuwapima watu wanaoshukiwa kuambukizwa corona.

KEMRI ambayo iko mstari wa mbele kwa kupima ugonjwa wa COVID-19, ina kiwanda cha kuunda vifaa vya tiba ambacho sasa kinatumiwa katika vita dhidi ya corona.

Kwa mujibu wa taarifa, kifaa hicho kinaweza kupima corona kwa kasi na hivyo kusaidia katika kuwatenga haraka walioambukizwa. Kifaa hicho kilichoundwa na KEMRI kina uwezo wa kubaini kirusi cha corona katika kipindi cha baina ya dakika 3 hadi 15 na hata wale wanaotaka faragha wanaweza kupimwa ndani ya nyumba zao. Kabla ya kifaa hicho maabara za Kenya zimekuwa zikitumia mashine kubwa iliyo katika maabara inayojulikana kama PCR ambayo huchukua hadi masaa matatu kupima. Hata hivyo changamoto ya mashine ya PCR imekuwa ni kukusanya sampuli za wagonjwa katika maeneo yote ya Kenya. Mbali na vifaa vya kupima corona vilivyoundwa na KEMRI, serikali ya Kenya pia imenunua mashine zinazojulikana kama Cobas 8800 za kupima corona ambazo zitaweza kuchukua vipimo 10,000 kwa siku. (KEMRI) ni shirika la kiserikali lililoanzishwa kupitia marekebisho ya sheria ya sayansi na teknolojia ya mwaka wa 1979. Kama shirika la kiserikali lina jukumu la kufanya utafiti wa afya nchini Kenya. KEMRI imekuwa na nafasi muhimu katika utafiti wa afya ya binadamu, na hivi sasa imechukua nafasi bora katika utafiti wa afya barani Afrika na ulimwenguni.

@@@

Watafiti wamebaini kuwa, virusi vya Corona huweza kuishi katika vitu mara tano zaidi ya muda uliodhaniwa hapo mwanzoni. Mwanzo ilidhaniwa kwamba virusi hivyo huweza kuishi kwa siku 3.

Kituo cha Utafiti na udhibiti wa magonjwa nchini Marekani (CDC), kimeandaa ripoti kuhusiana na mada hiyo. Katika ripoti hiyo ilifahamishwa kwamba virusi vipya vya Corona au COVID-19 huweza kuishi katika nyuso za vitu muda mrefu zaidi kuliko ule uliodhaniwa kwa mara ya kwanza.

Katika ripoti hiyo ilisemwa kwamba virusi vilivyokuwa katika meli mbili zilizosafiri kutoka California na Japan, dalili zake zilionekana hata siku 17 baadae.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wataalamu walisema kwamba  walipata dalili za virusi vya Corona katika meli za abiria za  Japan, Diamond princess na ile ya California Grand Princess hata siku 17 baada ya kuwahamisha abiria kutoka katika meli hizo.

@@@

Tokea  kudhihiri mlipuko wa ugonjwa hatari wa corona duniani, kumekuwa na usambazaji wa haraka wa ujumbe kuhusu kirusi hiki katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Mojawapo ikiwa ni "Whatsapp". Watu wameonekana wakitumia Whatsapp kutuma jumbe za haraka kwa jamaa na marafiki. Lakini sio kila ujumbe unaotumwa au unaotumiwa ni wa kweli. Kumekuwa na usambazaji wa habari za uongo kwa kasi zaidi hasa katika kipindi hiki kigumu cha mlipuko wa Covid-19. Watu wamekuwa wakitumiwa jumbe za simu ambazo si za kweli na wao pia kuendelea kuzisambaza kwa watu tofauti.

Kutokana na jambo hili,Whatsapp imechukua hatua mpya kwa kuweka kiwango maalumu cha kutuma jumbe kama hizo.

Jumbe kama hizo zinaweza kutumwa mara moja tu, na sio zaidi ya hapo.Hatua hii imechukuliwa ili kupunguza kasi ya kusambaa kwa jumbe kama hizo.

Kabla ya marufuku hii, ujumbe mmoja ulikuwa unaweza kutumwa kwa watu watano tofauti au makundi tofauti kwa wakati mmoja.

@@@