May 23, 2020 02:42 UTC
  • Iran yapokea maombi ya kuuza vifaa vyake vya corona katika nchi 40

Mkuu wa Kamati ya Kielimu ya Idara ya Kitaifa ya Kupambana na virusi vya Corona nchini Iran amesema kuwa nchi 40 zimetuma maombi ya kutaka kununua vifaa vya kubaini Corona ambavyo vimetengenezwa na Shirika la Kielimu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mostafa Ghanei aliyasema hayo hivi karibuni ambapo sambamba na kubainisha kwamba kuna aina mbili za vifaa vya kubainia Corona, ameongeza kuwa, kuna kimoja cha kubaini molekuli ambacho kinahitajika nchini na hivyo hakiruhusiwi kuuzwa nje ya nchi, lakini kuna cha pili ambacho ni cha ELISA (cha kubaini Antibody), na ambacho kimetengenezwa kwa kiwango cha juu na tayari kina kibali cha kuuzwa nje ya nchi. Ghanei amesema kuwa, moja ya mashirika ya kielimu ya Iran ambayo yanahusika na uzalishaji wa vifaa vya kubaini Antibody limesema kwamba, kwa siku moja linaweza kuzalisha zaidi ya vifaa milioni moja,  na kwamba mahitaji ya Iran ni milioni moja pekee na hivyo vilivyosalia vinaweza kuuzwa nje ya nchi. Aidha Mkuu wa Kamati ya Kielimu ya Idara ya Kitaifa ya Kupambana na virusi vya Corona nchini Iran sambamba na kuashiria kwamba, jina la Shirika la Kielimu la Iran tayari limewekwa katika orodha ya mashirika yanayozalisha vifaa vya kubaini virusi vya Corona katika ngazi ya kimataifa, amesema kuwa, licha ya kwamba katika mtazamo wa kielimu uzalishaji wa kifaa cha ELISA cha Kiirani sio suala gumu na kwamba inatazamiwa kuwa nchi nyingi zilizo na teknolojia hiyo zitaweza kutengeneza kifaa hicho katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, lakini kasi ya uzalishaji wa kifaa hicho uliochukua miezi miwili pekee kutengenezwa tangu kuzuka virusi vya Corona na kupata vibali vya viwango na uuzaji nje ya nchi, ni sifa ya kipekee ya ushindani wa shirika la kielimu la Iran. Mostafa Ghanei ameendelea kubainisha kwamba hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya nchi tano za mwanzo katika utafiti wa Corona na kuongeza kuwa lengo la utafiti huo ni kutibu na kubaini dawa ya chanjo ya virusi hivyo. Mkuu wa Kamati ya Kielimu ya Idara ya Kitaifa ya Kupambana na virusi vya Corona nchini Iran ameashiria kufanyika tafiti 500 kimataifa katika uga wa Corona na kusema kuwa, nchini Iran pekee kunafanyika tafiti tofauti 250 kuhusu virusi vya Corona ambapo 25  kati ya hizo zinahusiana na njia sahihi za kutibu na kutengeneza dawa au chanjo ya Corona. 

@@@ 

Kenya sasa imeungana na jitihada za kimataifa za kutafuta chanjo ya COVID-19 baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuidhinisha ombi lake la kushiriki katika majaribio ya pamoja ya kutafuta tiba ya virusi hatari vya corona. Kundi la watafiti kutoka taifa hilo la Afrika Mashariki sasa linasubiri idhini ya mwisho kutoka kwa Baraza la Kenya la Sayansi na Teknolojia kabla ya kuanza mchakato wa kuwapata wagonjwa watakaoshirikishwa katika utafiti huo.

Endapo majaribio ya dawa hizo yataidhinsishwa, Wakenya ambao wamepatikana na virusi vya corona wataorodheshwa na kufanyiwa majaribio ya dawa aina nne ambazo zimeonesha matumaini ya kukabiliana na virusi hivyo. Wanasayansi wa Kenya watafanyia majaribio dawa tatu ili kubaini ikiwa dawa hizo zinaweza kutibu ugonjwa huo au la. WHO lilichagua dawa nne ambazo ziolinesha ushahidi wa kutibu virusi baada ya uchunguzi wa maabara kuonesha inaweza kutibu wanyama kutokana na uchunguzi wa kimatibabu uliofanywa na wataalamu kutoka maeneo tofauti duniani. Watafiti sasa wamepata idhini ya kufanyia majaribio aina nne za dawa ikiwa ni pamoja na: Remdesivir, ambayo awali ilitengenezwa kwa ajili ya kutibu Ebola, dawa ya kutibu malaria ya hydroxychloroquine, Lopinavir/ritonavir, ambayo pia imeidhinishwa kuwatibu wagonjwa walio na virusi vya HIV na Interferon beta-1a.

Kufikia sasa hakuna tiba rasmi ya COVID-19 lakini maafisa wa afya kutoka sehemu tofauti duniani wana matumaini kwamba majaribio ya pamoja ya chanjo yatasaidia kupatikana kwa chanjo haraka iwezekanavyo. Zaidi ya nchi 35 barani Afrika zimeonesha nia ya kushiriki katika majaribio hayo lakini ni mataifa sita pekee ndiyo yaliyopewa idhini. Kando na Kenya mataifa mengine yaliyopewa idhini ni pamoja na, Afrika Kusini, Misri, Zambia, Nigeria na Tunisia.

Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya kuambukiza katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta mjini Nairobi   Dkt Loice Achieng Ombajo anasema kwamba bado wako katika awamu ambayo hawawezi kubaini moja kwa moja ni dawa ipi inafanya kazi. Ameongeza kuwa katika majaribio ya tiba wagonjwa wengi wanashirikishwa bila mpangilio maalu lakini wote wanapewa dawa tofauti.

@@@

Na Ripoti mpya ya uchambuzi wa biashara mtandaoni iliyotangazwa na Kamati ya Biashara na Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD inasema kuwa hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba biashara ya mtandao inakua lakini bila uwiano katika mataifa yote. UNCTAD inasema kuwa mwaka 2018, mauzo ya bidhaa kupitia mtandaoni yalifikia thamani ya dola trilioni 25.6 duniani kote.

Hata hivyo katika nchi 10 zinazoongoza katika biashara hiyo hakuna hata moja kutoka mataifa machanga, mataifa hayo yakifanya biashara ya kampuni kwa kampuni au B2B na kampuni kwa mtumizi au B2C.

Ripoti hiyo imebaini kuwa, Marekani imeendelea kuongoza katika biashara hiyo ya mtandaoni ikifuatiwa na China na Uingereza. Kwa kuangalia wanunuzi wa mtandaoni, ripoti inasema kuwa katika chumi 20 za juu duniani, kiwango cha watu kutumia intaneti kununua bidhaa inatofautiana ambapo kwa mwaka huo wa 2018, asilimia 87 ya wakazi wa Uingereza walinunua bidhaa kupitia mtandaoni ikilinganishwa na Thailand asilimia 14 na India asilimia 11. Changamoto nyingine kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa, baadhi ya nchi haziweki takwimu sahihi za ununuzi mtandaoni na hata zinapochapisha, hazifuati kanuni za kibiashara zinazotambulika kimataifa wakati wa uchapishaji wa taarifa hizo.

Ni kwa mantiki hiyo ndipo  katika wiki ya biashara mtandaoni iliyoendelea hadi tarehe 1 mwezi Mei, ikiwaleta pamoja kwa njia ya mtandao mawaziri, wakuu wa mashirika ya kimataifa na watendaji wakuu wa biashara na mashirika ya kiraia, kulichambuliwa mbinu sahihi za kusonga mbele baada ya Corona na kutafutwa mbinu za kunufaika vyema na biashara kupitia mtandaoni.

Akizungumzia biashara ya mtandaoni na kiwango chake, Shamika Sirimanne ambaye ni Mkurugenzi wa Teknolojia UNCTAD amesema kuwa, “janga la COVID-19 limechochea utumiaji wa suluha za kimtandao kukiwemo kupata huduma na vifaa, lakini kwa ujumla bado ni vigumu kutabiri thamani ya biashara ya mtandaoni kwa mwaka huu wa 2020.”

@@@

Naam na hadi hapo wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia.

 

Tags