Jun 19, 2020 02:29 UTC
  • Ijumaa tarehe 19 Juni mwaka 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 19 mwaka 2020.

miaka 1100 iliyopita mwafaka na leo, alizaliwa malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasaman na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (sww) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa usomaji mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameacha tungo kadhaa za mashairi.

Abu Is'haq Kesa-i Marvazi

Siku kama ya leo miaka 153 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo. Baada ya Benito Juarez kujinyakulia urais wa Mexico mwaka 1855, aliwakata mikono wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini Mexico. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa, na kulazimika kutuma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji nchini humo.

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1877, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri. Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu wa Kipolandi, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait. Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza.

Bendera ya Kuwait

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita magaidi wa kundi la Munafiqin walitenda jinai kubwa ya kutisha katika haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) mjukuu wa Mtume Mtukufu (s.a.w) katika mji mtakatifu wa Mash'had. Bomu liliripuka ndani ya haram tukufu ya Imam Ridha (a.s) alasiri ya siku ya Ashura mwaka huo wakati watu walipokuwa wakifanya ziara na marasimu ya kukumbuka mapambano ya kihistoria ya kuuawa shahidi Imam Hussein(a.s). Makumi ya waumini na wapenzi wa Ahlul Bait (a.s) waliuliwa shahidi au kujeruhiwa katika haram hiyo. Mlipuko huo ulisababisha hasara na maafa mengi katika haram hiyo tukufu.

Haram ya Imam Ali bin Mussa al Ridha (as)

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia alifariki dunia Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, mlinganiaji mkubwa wa Uislamu katika kanda ya mashariki mwa Afrika. Hujjatul Islam Walmuslimin Rizvi alizaliwa huko mashariki mwa India na baada ya kupata masomo ya awali kwa baba yake alijifunza masomo ya juu na lugha za Kingereza, Kifarsi na Urdu na kupata daraja ya Fakhrur Afadhil. Baada ya kulingania dini kwa miaka mingi nchini India, Sayyid Akhtar Rizvi alihisi wajibu wa kuelekea Tanzania, barani Afrika na kuanza kueneza maarifa ya dini na mafundisho ya Ahlubaiti wa Mtume (saw). Allamah Rizvi ameandika na kufasiri vitabu vingi kwa lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafsiri ya Qur'ani ya al Miizan na kitabu cha Al Ghadir na kujenga makumi ya misikiti, madrasa, maktaba na zahanati. Alifariki dunia jijini Dar es Salaam katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 76.

Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

 

Tags