Jun 27, 2020 10:27 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (11)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao. Katika vipindi vyetu kadhaa vilivyotangulia tulimzungumzia Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid, mmoja wa Maulamaa na wanazuoni mashuhuri mno katika ulimwengu wa Kishia. Tulibainisha kwa kifupi historia ya maisha yake pamoja na juhudi kubwa alizofanya katika uga wa elimu, mchango wake pamoja na vitabu vyake muhimu ambavyo licha ya kupita karne nyingi, lakini vingali vina thamani kubwa kwa kizazi cha leo. Sehemu ya 11 ya mfululizo huu juma hili, itamzungumzia Abul-Hassan Muhammad bin Hussein bin Mussa, Musawi Baghdadi mashuhuri kwa jina la Sayyid Sharif Radhii mmoja wa wanafunzi wakubwa wa Sheikh Mufid. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Abul-Hassan Muhammad bin Mussa Musawi Baghdadi mashuhuri wa jina la Sayyid Radhii alikuwa alimu mkubwa na asiye na mithili katika zama zake na alitambulika kama mwanazuoni na msomi aliyekuwa amebobea na kutabahari katika elimu ya fiqih, teolojia na fasihi kama ambavyo pia alikuwa mfasiri stadi na mahiri wa Qur’ani. Sharifu Radhii ni ndugu wa Sayyid Murtadha msomi na mwanazuoni mwingine mtajika wa Kishia katika zama zake.

Sayyid Radhii alizaliwa mwaka 359 Hijria Qamaria katika mji wa Baghdad huko Iraq. Nasaba yake kwa upande wa baba inafika kwa Imam Mussa al-Kadhim (as) na kwa upande wa mama inafika kwa Imam Zeinul-Abidin (as). Baba yake yaani Abu Ahmad Hussein aliyekuwa na lakabu ya Tahir na Dhul-Mutaqbain alikuwa shakhsia mtajika na muhimu katika zama zake. Alikuwa kiongozi wa Masayyid, msimamizi na mshughulikiaji wa mashtaka ya watu na Amir wa Hija.  Fatma, binti wa Abu Muhammad, alikuwa mwanamke msomi na aliyejipamba kwa taqwa na uchaji Mungu na Sheikh Mufid alikiandika kitabu cha “Hukumu za Wanawake” kwa ombi la mwanamke huyo.

Nahaj al-Balagha (tarjuma ya Kifarsi)

 

Inasimuliwa kuwa, usiku mmoja Sheikh Mufid aliota na kumuona Bibi Fatma Zahraa (as) ambaye alimjia ndotoni hali ya kuwa amewashika mikono Imam Hassan na Hussein (as) wakiwa wadogo na kumwambia: Ewe Sheikh wafundishe elimu ya fiqihi watoto hawa wawili. Sheikh Mufid alipozinduka usingizini alishangazwa mno na ndoto hii ambayo ilishughulisha fikra na akili yake. Asubuhi ya siku hiyo hiyo, mama yake Sayyid Radhii na Sayyid Murtadha alimjia Sheikh Mufid hali ya kuwa amewashika mikono watoto wake hao wawili na kumwambia: Ewe Sheikh! Wafundishe watoto hawa elimu ya fiqihi. Baada ya kusikia hivyo na kukumbuka ndoto ya jana yake, Sheikh Mufid aliathirika mno na kububujikwa na machozi na kisha akasimulia ndoto yake. Hivi ndivyo Sheikh Mufid alivyochukua jukumu la kuwalea na kuwafundisha Massayid hawa wawili ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi wakubwa.

 

Sayyid Radhii alionyesha kipaji cha hali ya juu mbele ya mwalimu wake tangu awali na kadiri alivyokuwa akikwea daraja za elimu ndivyo alivyokuwa akisifiwa na kutajwa kwa wema na wanazuoni na wasomi wa zama zile na kuonewa husuda na maadui zake. Ni mashuhuri kwamba, alipokuwa na umri wa miaka 9 alikuwa akijibu kwa umakini mkubwa maswali ya Ustadhi mkubwa wa elimu ya Nahw ambapo hadhirina walikuwa wakishangazwa na kipaji na maarifa yake ya hali ya juu aliyokuwa nayo. Mbali na kuhudhuria masomo kwa Sheikh Mufid, Sayyid Radhii alisoma pia elimu ya dini kwa wanazuoni wengine wakubwa wa zama zake waliokuwa wakiishi mjini Baghdad. Alisoma elimu za nahw, sarf, balagha, tafsiri, hadithi, fikihi, Usul na teolojia na kustafidi vyema na kila elimu miongoni mwa elimu hizo. Sayyid Radhii alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza, kwani mbali na kunufaika na bahari ya elimu ya wanazuoni wa Kishia, alisoma pia kwa walimu wa Kisuni ili aweze kuwa na umahiri kwa vitabu vya hadithi na fiqihi vya madhehebu mbalimbali. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana akawa na uwezo mkubwa wa mijadala na midahalo.

Kaburi la Sayyid Radhii

 

Kabla ya kufikia umri wa kubaleghe, Sayyid Radhii alikuwa tayari amesoma na kuzijua vyema akthari ya elimu za zama zake na alipofikisha umri wa miaka 20 alikuwa tayari amebobea katika elimu zote za zama hizo. Sayyid Radhii alianza kualifu na kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 17. Vitabu vya alimu huyo vipo katika orodha ya juu kabisa ya vitabu vya dini vyenye thamani kubwa kabisa katika ulimwengu wa Kishia. Hata hivyo kitabu mashuhuri kabisa cha alimu huyu ni Nahaj al-Balagha yaani Njia ya Balagha. Katika kitabu hiki Sayyid Radhii amekusanyika kutoka katika vitabu mbalimbali hotuba, barua na semi za Imam wa Wachamungu Ali bin Abi Twalib (as) na kuziweka katika mpangalio maalumu.  Athari nyingine za Sayyid Radhii ni  Khassais al-Aimah na Tafsiri Mutashabihat Qur’ani ambapo muhtawa na kiwango cha vitabu hivi ni ithbati tosha juu ya uwezo wake wa kielimu na maarifa aali aliyokuwa nayo.

 

Sayyid Radhii ambaye ni mashuhuri zaidi kwa jina la Sharifu Radhii mbali na kubonbea katika elimu za kidini, alikuwa mwalimu mahiri pia wa zama zake katika fasihi ya lugha ya Kiarabu na hakuwa na mithili katika elimu za mashairi na nathari. Alianza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka kumi. Mashairi yake yalikuwa yakienea baina ya watu hatua kwa hatua na kuhifadhiwa. Diwani yake ya mashairi inajumuisha zaidi ya beti 6,300 za mashairi yenye thamani kubwa.

Sayyid Radhii alikuwa mashuhuri pia kwa ukarimu. Aidha pamoja na kutingwa na mambo mengi, lakini hilo halikumzuia kuasisi chuo na kuanza kuelea wanafunzi ambao baadaye waliondokea kuwa wasomi watajika. Na ili wanafunzi na watafuta elimu waweze kustafidi zaidi, aliwaandalia suhula za maisha ambapo katika zama hizo hilo halikuwa na mithili. Kazi nyingine ya thamani ya mwanazuoni huyu ni kuasisi maktaba kubwa. Chuo chake alikipa jina la Darul-Ilm. Chuo cha Darul-Ilm cha Sayyid Radhii kilitambulika kwa makumi ya miaka kabla ya Chuo cha Nidhamiyah cha Baghdad. Chuo cha Nidhamiya kilijengwa kwa bajeti kubwa ya dola ya wakati huo, lakini Sayyid Radhii yeye alijenga chuo chake kwa kutumia fedha zake binafsi. Aidha inanukuliwa kuwa, alimchongea ufunguo wa stoo kila mwanafunzi miongoni mwa wanafunzi wake ili aweze kuingia na kuchukua kitu anachokihitajia wakati wowote ule.

Mbali na kusoma na kufundisha, Sayyid Radhii alikuwa akibeba majumu mazito ya kijamii pia; kwani alikuwa akijitokeza katika medani za utoaji huduma za kijamii kwa Waislamu.

Msomi na mwanazuoni huyo wa Kishia hatimaye aliaga dunia kiwa na umri wa miaka 47. Inaelezwa kuwa, alimu huyo alikufa kifo cha ghafla na cha kutatanisha. Kuaga kwake dunia ghafla kulikuwa kwa huzuni mno kiasi kwamba, mawaziri, mafaqihi na makadhi wa Kisuni na Kishia baada ya kusikia taarifa ya kifo chake walielekea katika nyumba yake wakitembea peku.  Hatimaye Sayyid Radhii akazikwa huko Kadhmein, ingawa baadaye mwili wake ulihamishwa na kuzikwa Karbala.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Msisite kuwa pamoja nami katika sehemu ya ijayo ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags