Jun 27, 2020 10:31 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (12)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia wanazuoni wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao

Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Abul-Hassan Muhammad bin Mussa Musawi Baghdadi mashuhuri wa jina la Sayyid Radhii mashuhuri zaidi kwa jina la Sharifu Radhii aliyekuwa alimu mkubwa na asiye na mithili katika zama zake na alitambulika kama mwanazuoni na msomi aliyekuwa amebobea na kutabahari katika elimu ya fikihi, teolojia na fasihi kama ambavyo pia alikuwa mfasiri stadi na mahiri wa Qur’ani. Tulieleza kwamba, mwanazuoni huyo ndiye aliyekusanya semi, barua, na hotuba za Imam Ali bin Abi Talib (as) na kuziweka katika sura ya kitabu kinachojulikana kwa jina la Nahaj al-Balagha yaani Njia ya Balagha. Sehemu ya 12 ya kipindi chetu juma hili, itamzungumzia Sayyid Murtadha ambaye naye ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kishia. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Ali bin Hussein bin Mussa maarufu kwa jina la Sayyid Murtadha, Sharif Murtadha au Alamul Huda ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kishia aliyekuwa amebobea mno katika elimu za fikihi na teolojia na alihesabiwa kuwa, miongoni mwa shakhsia wa Kishia waliokuwa na ushawishi mkubwa wa kijamii. Aliishi katika karne ya 4 na ya 5 na kielimu alikuwa na daraja kubwa ambapo ilikuwa vigumu kumpata msomi mfano wake katika zama hizo.   Sayyid Murtadha alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu nyingi za zama zile kama teolojia, fikihi, Usul, tafsiri, falsafa, nujumu na isimu. Kimsingi Sayyid Murtadha ambaye ni ndugu yake Sharifu Radhii alihesabiwa kuwa, mwanafunzi mahiri zaidi wa Sheikh Mufid.

Baada ya baba na kaka yake, Sayyid Murtadha alikuwa kiongozi wa masharifu kwa muda wa miaka 30 na msimamizi wa mahujaji. Aidha alikuwa kiongozi wa mahakama ya waliodhulumiwa.

Mahakama hiyo ilikuwa na jukumu la kushughulikia mashtaka ya raia dhidi ya watawala na viongozi. Kwa mtazamo wa Sayyid Murtadha ambaye anajulikana pia kama Alamul Huda ni kuwa, ni sahihi na inafaa kufanya kazi na kushirikiana na mtawala dhalimu endapo kufanya hivyo kutakupa fursa ya kuondoa dhulma dhidi ya Waislamu na kusimama uadilifu.

Sayyid Murtadha "Alamul Huda"

 

Mwanazuoni huyo alikuwa mwanafikra aliyekuwa akitumia mno akili na akiamini nafasi ya akili katika mambo.

Alikuwa akiamini kuwa, ili kuthibitisha uwepo wa Mwenyezi Mungu, ni wajibu kutumia akili na hoja, na haiwezekani kuthibitisha uwezo wa Muumba kwa kutosheka tu na maandiko ya kidini. Hii ni kutokana na kuwa, maandiko ya dini nayo yanakuwa na itibari baada ya kuwa kabla ya hapo uwepo wa Mola Muumba umethibitishwa kwa kutumia akili na baadhi ya sifa zake kufahamika.

Itikadi hii ya Sayyid Murtadha ina chimbuko la mafundisho ya Qur’ani ambapo Usul Din yaani Misingi ya Dini ambayo ni Tawidi, Uadilifu, Utume, Uimamu, na Ufufuo ni misingi ya Kiislamu ambayo mtu hapaswi kuikubali kwa kufuata tu au kwa kusikia tu kutoka kwa wengine, bali inapaswa kumthibikia mtu kupitia akili. Alamul Huda alikuwa akitilia mkazo mno suala la akili kuwa ni hoja katika itikadi na masuala yanayohusiana na teolojia; na kitu chochote kinachopingana na akili alikuwa akikihesabu kuwa ni batili.

Ndio maana alipokuwa akikutana kuna mgongano wa baadhi ya riwaya na akili, alikuwa akisimama upande wa akili na alikuwa akiamini kwamba, hadithi zote zilizotufikia hakuna ulazima kuwa ziwe sahihi. Kwa kuwa, katika zama za Sayyid Murtadha, kulikuweko na wafuasi wa kundi la Mu’utazilah waliokuwa na harakati mjini Baghdad ambao nao kwa namna fulani walikuwa wakihesabiwa kuwa watu wa mrengo wa akili, baadhi ya watu wakamhesabu Sayyid Murtadha kuwa ni Mu’utazilah ilihali si kweli hata kidogo.

Sayyid Murtadha alikuwa mstari wa mbele pia katika kualifu na kutunga vitabu; kwani amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake katika ulimwengu wa Kishia vitabu na athari zenye thamani kubwa.

 Marhumu Allama Amini ametaja katika kitabu chake cha al-Ghadir, majina 86 ya vitabu vya Sayyid Murtadha ambapo moja ya vitabu vyake hivyo, ni Diwani ya Mashairi yenye beti 20,000. Kitabu chake kingine kinaitwa al-Intisar. Kitabu hiki ni miongoni mwa vitabu vya awali vya fikihi ambacho kinazungumzia masuala ambayo Mashia na Masuni wanatofautiana na kinajumuisha pia hukumu ambazo ni maalumu kwa Mashia.

Athari yake nyingine muhimu ya fikihi ni kitabu cha Naasiriyaat. Aidha kitabu cha "Dhariyah ilaa Usul al-Shariyah" ni athari nyingine muhimu ya Sayyid Murtadha, kitabu ambacho kinabainisha kwa mapana na marefu elimu ya Usul al-Fiqih na kinatoa hukumu kuhusiana na mitazamo ya Ahlu Sunna. Kitabu hicho kinahesabiwa kuwa, ufunguo wa kuundika elimu ya Usul ya Shia na kujitenga na elimu ya Usul ya Ahlu Sunna. Aidha ana vitabu vingine viwili muhimu ambapo cha kwanza ni Aamali chenye maudhui ya fiqih, tafsiri, hadithi, mashairi na taaluma ya isimu; na kitabu cha pili ni Shafi kinachozungumzia Uimamu.

Kaburi la Sayyid Murtadha "Alamul Huda"

 

Katika zama zake alimu huyo alikuwa mashuhuri mno na vikao vyake vya elimu vilikuwa vikijaa watu wakiwemo shakhsia mashuhuri wa zama hizo. Wakati mwingine hata mwalimu wake mkubwa, yaani Sheikh Mufid alikuwa akishiriki katika vikao vya elimu vya mwanafunzi wake huyo. Alikuwa na nyumba kubwa ambayo aliigeuza kuwa chuo na kufundisha elimu mbalimbali kama fiqih, teolojia, tafsiri, lugha, mashairi, nujumu na hisabati.

Watu wenye kiu cha elimu walikuwa wakimwendea kutoka maeneo mbalimbali ya dunia. Hata hivyo aghalabu ya wanafunzi hao hawakuwa na uwezo wa kudhamini mahitaji yao ya masomo na maisha. Sayyid Murtadha akatenga sehemu maalumu ya nyumba yake kwa ajili ya wanafunzi. Aidha aliwaandalia maktaba kubwa pia. Kama zama ambazo vitabu vilikuwa kwa sura ya hati ya mkono na hakukuweko na teknolojia ya uchapishaji, katika maktaba hiyo, Sheikh Murtadha alikuwa na takribani mijalada 80,000 ya vitabu.

Hatimaye Sayyid Murtadha aliaga dunia tarehe 25 Rabiul-Awwal 436 Hijria huko Baghdad akiwa na umri wa miaka 80 na kuzikwa huko. Baadaye mwili wake ulihamishiwa katika mji wa Karbala na kuzikwa jirani na haram tukufu ya Imam Hussein as.

Kwa leo tunakomea hapa Wapenzi Wasikilizaji. Tukutane tena wiki ijayo. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags