Jun 27, 2020 10:45 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (14)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popotev pale mlipo. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao

Kipindi chetu kilichopita kilianza kuzungumzia historia na maisha ya Abu Ja’far Muhammad bin Hassan Tusi mashuhuri kwa jina la Sheikh at-Taifah au Sheikh Tusi fakihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mahiri na mashuhuri wa Kishia wa elimu ya teolojia ambaye aliishi katika karne ya tano Hijria. Tulibainisha kwamba, Sheikh Tusi ndiye mwandishi na mtunzi wa vitabu viwili kati ya vitabu vinne muhimu vya hadithi vya Waislamu wa Kishia vinavyojulikana kama Kutub al-Arbaa kama ambavyo pia ndiye muasisi wa Chuo Kikuu cha Kidini au Hawza ya Najaf al-Ashraf. Sehemu ya 14 ya mfululizo huu juma hili itatupia jicho athari na vitabu vya mwanazuoni huyu. Jiungeni nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.

 

Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali za elimu za Kiislamu. Hii leo kuna athari takribani 50 zilizobakia. Athari za mwanazuoni huyo hivi sasa zimeratibiwa na kuchapishwa katika sura ya Dairatul-Maarifi  yaani Ensaiklopidia ambayo ni seti ya vitabu vinavyotoa taarifa kuhusu mambo mengi. Vitabu viwili kati ya vitabu vinne muhimu vya hadithi kwa Waislamu wa Kishia vinavyojulikana kwa jina la Kutub al-Ar’baa ambavyo ni Tahdhib al-Ahkam na Al-Istibsar vimeandikwa na Sheikh Tusi. Kila faqih na mujitahdi akiwa na lengo la kunyambua sheria na kutoa Fatuwa hana budi kurejea vitabu hivi vinne ambapo viwili kati ya hivi kama tulivyosema vimeandikwa na Sheikh Tusi. Kutub al-Ar’baa ni majimui ya vitabu vya hadithi ambavyo vinatumiwa na Maulamaa wa Kishia kama marejeo yao makubwa.

Sheikh Tusi

 

Kitabu cha Tahdhib al-Ahkam cha Sheikh Tusi kwa hakika ndicho kitabu chake cha kwanza kukiandika. Kitabu hiki ni moja ya vitabu vya hadithi vya Mashia vyenye itibari kuwa na kitabu cha tatu miongoni mwa vitabu vinne vya hadithi tulivyoeleza umuhimu wake miongoni mwa wanazuoni wa Kishia. Kitabu hiki kinakubaliwa na maulamaa na wanazuoni wote wa Fiqih wa Kishia. Kitabu hiki kinajumuisha hadithi 13,590 zenye maudhui ya fiqih na hukumu mbalimbali za kisheria, hadithi ambazo zimenukuliwa kutoka kwa Ahlul-Baiti (as).

Kitabu kingine cha Sheikh Tusi kama tulitangulia kusema kinaitwa al-Istibsar. Kitabu hiki kina jumla ya hadithi 5,511 na kinajihusisha na kuchunguza pamoja na kuchambua zile hadithi ambazo kidhahiri zina mgongano baina yao. Miongoni mwa riwaya na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Maimamu watoharifu (as), baadhi yazo kidhahiri zina mgongano. Sheikh Tusi aliandika kitabu hiki baada ya kundi la wanazuoni na wanafunzi wake kumtaka aalifu kitabu ambacho kitakusanya humo hadithi zinazopingana na kisha kuzichunguza na kuzichambua. Katika kitabu hiki, Sheikh Tusi amekusanya, hadithi zote zinazohusiana na masuala mbalimbali ya Kifiqih ambazo kwa mtazamo wake ni sahihi kisha akaashiria hadithi zinazopinga baadhi ya mambo na alijitahidi asiache hata hadithi moja. Kisha baada ya hapo akafanya uchambuzi wa hadithi hizo. Kwa hakika kitabu hiki ni cha aina yake na ni kitabu cha kwanza kukusaya hadithi ambazo pia ni zinapinga baadhi ya mambo.

 

Athari nyingine muhimu mashuhuri ya Sheikh Tusi anayejulikana pia kama Sheikh Taifah ni “al-Tibyan fi tafsir al-Qur’ani” kitabu ambacho kwa mukhtasari kinajulikana kwa jina la al-Tibyan. Kitabu hiki ni tafsiri ya kwanza kamili ya Kishia ya Qur’ani ambayo imefasiri Aya zote za Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kitabu hiki kinahesabiwa kuwa moja ya vyanzo vikongwe vya tafsiri ambapo wafasiri wengi wa Kishia wa Qur’ani wamepata muongozo hapo.

 

Katika kitabu chake hiki cha Tibyan, Sheikh Tusi akiwa na lengo la kufasiri Aya za Qur’ani mbali na kunukuu riwaya na hadithi kutoka kwa Bwana Mtume (saw) na Ahlul-Baiti (as) alitegemea pia akili na elimu mbalimbali sambamba na kuchambua na kutathmini rai na mitazamo ya wafasiri wa zamani na wa zama zake.

Tafsiri za Qur’ani zilizokuwa zimeandikwa na Mashia au Masuni kabla ya Sheikh Tusi hazikuwa zimejumuisha Qur’ani nzima mbali bali zilikuwa ni za baadhi ya Sura za kitabu hiki kitakatifu. Lakini tafsiri ya Sheikh Tusi ya “At-Tibyan Fi Tafsir al-Qur’ani” ilijihusisha na Aya zoteza Qur’ani na kubainisha Aya hizo katika mitazamo yote ya elimu mbalimbali za Qur’ani kama usomaji, maana, sarf, nahw na kadhalika. Aidha kutokana na kuwa, Sheikh Tusi alikuwa amebobea katika elimu ya teolojia, tafsiri yake hiyo inatoa majibu ya shubha na utata wa masuala mbalimbali yanayozungumziwa na makafiri na makundi ya batili.

Kutokana na umuhimu mkubwa ulionazo riwaya na hadithi katika kufahamu dini na maarifa yake, suala la uaminifu na kusema ukweli kwa mtu anayenukuu hadithi ni jambo muhimu na lenye thamani kubwa. Adabu na hukumu nyingi za dini zinafahamika kupitia maneno ya Bwana Mtume (saw). Hivyo basi kuna haja ya kuchambua kwa umakini mkubwa hadithi na kufahamu ni hadithi gani ni sahihi na ambayo kweli ni maneno ya Bwana Mtume (saw) au Maimamu watoharifu (as), na ni hadithi gani ambayo ni ya uongo na imenasibishwa tu na watukufu hao lakini kiasili si maneno ya Mtume (saw) wala Maimamu watoharifu (as), au hadithi ambayo kimsingi imenasabishwa na watukufu hao kimakosa bila ya kukusudia.

 

Kuanzia karne ya 4 Hijria kulishuhudiwa wimbi kubwa la upandikizaji hadithi. Sheikh Tusi alidiriki hatari hiyo na hivyo akachukua jukumu la kuandika kitabu alichokipa jina la al-Abwab au “Rijaal Tusi” kama ambavyo aliandika pia kitabu cha jina la al-Fihrist. Kitabu hiki kinahesabiwa kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya vitabu vinavyozungumzia wapokezi wa hadithi ambacho kinaaminiwa na wanazuoni wa Kishia.

Sheikh Tusi alikuwa na mtoto aliyefahamika kwa jina la Hassan ambaye baada ya kuaga dunia baba yake alibakia katika mji wa Najaf na kufanikiwa kufikia hatua ya Umarjaa. Aidha mjukuu wa Sheikh Tusi pia yaani Muhammad aliyekuwa na kuniya ya Abul Hassan naye alifanikiwa kukwea daraja za elimu na kufikia hatua ya kuwa Marjaa.

Sheikh Tusi amezikwa katika mji wa Najaf. Mwanazuoni huyu alizikwa katika nyumba yake na kwa mujibu wa wosia wake nyumba hiyo ilibadilishwa na kuwa msikiti.  Masjid Tusi ambao unajulikana pia kwa jina la Msikiti wa Jamia, hii leo ni moja ya misikiti mashuhuri mjini Najaf Iraq.

 

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa maneno ya Ustadh Shahidi Murtadha Mutahhari, mwanafikra mkubwa na mtajika wa Kiislamu wa Kiirani ambaye amesema kuhusiana na Sheikh Tusi kwamba: Katika ulimwengu wote wa Kiislamu kunahisika uwepo wa Sheikh Tusi wa imani ya Kiislamu, shauku na vuguvugu la Kiislamu na hamu ya kuuhudumia Uislamu.  Sheikh Tusi aliufahamu Uislamu kama unavyopaswa kufahamika, hivyo ni haki ya akili kumheshimu mwanazuoni huyo.

Kwa leo tunakomea hapa tukutane tena juma lijalo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags