Aug 24, 2020 06:14 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Agosti 24

Hujambo mpenzi mwanaspoti na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa......Karibu.....

Soka Iran; IPL yafikia tamati kwa vicheko na vilio

Ligi Kuu ya Soka ya Iran imefunga pazia lake msimu huu kwa vicheko na vilio. Siku ya Alkhamisi, klabu ya Foolad ilikamilisha jedwali lake kwa vicheko, baada ya kuichakaza Teractor bao moja la uchungu bila jibu. Bao hilo la ushindi na la kipekee la Foolad lilitiwa wavuni na Aref Aghasi katika kipindi cha kwanza. Kwa ushindi huo japo hafifu, lakini klabu hiyo imejikatia tiketi ya kushiriki Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia msimu ujao. Hapa mjini Tehran, mabingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Soka ya Iran, klabu ya Persepolis walishuka dimbani kuvaana na Saipa. Mchezo huo ulimalizika kwa Saipa kunyolewa kwa chupa kwa kuzabwa mabao 3-0. Mabao hao ya Wekundu wa Tehran yalifungwa na Vahid Amiri, Christian Osaguona na Ali Alipour.

Wachezaji wa klabu ya Esteqlal katika picha ya pamoja

 

Esteqlal nayo iliibamiza Shahin mabao 4-1 na kumaliza msimu katika nafasi ya pili. Mabao ya The Blues wa Tehran yalifungwa na Vouria Ghafouri, Cheick Diabate (2) and Mehdi Ghaedi.

Wakati huo huo, klabu ya Pars Jonoubi ambayo ilipaswa kuishinda Naft Majed Soleyman ili isalie katika Ligi ya IPL imejikuta ikiungana na Shahin katika kushushwa daraja, baada ya kuchabangwa bao 1 bila jibu. Sepahan imeambulia nafasi ya tano baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Paykan, wakati ambapo Zob Ahan ilikuwa inaishwa mabao 3-2 na Gol Gohar mjini Isfahan. Nao watengenezaji magari Machine Sazi wamefunga msimu kwa ushindi dhaifu wa bao 1-0 walipovaa na wanamafuta wa Sanat Naft.

Taekwondo Poomsae: Wairani wazoa medali

Wanafunzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa medali sita katika Mashindano ya Kimataifa ya Mabingwa wa Taekwondo aina ya Poomsae yaliofanyika Nepal. Hii ni mara ya kwanza kwa wanataekwondo hao wa Kiirani kushiriki mashindano hayo kwa njia ya intaneti kutokana na janga la Covid-19. Wanafunzi zaidi ya 290 wa kiume na 260 wa kike walishiriki mashindano hayo yaliyoratibiwa na Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Shule.

Mmoja wa wanataekwondo chipukizi wa Iran

 

Katika kategoria ya wanamichezo wenye umri baina ya miaka 12 na 14, Sanaz Taqipour wa mji mkuu Tehran aliibuka wa pili, huku Narges Bolqand na Amir Hossein Esmaeili wakiibuka katika nafasi ya tatu kila mmoja katika safu ya wasichana na wavulana kwa usanjari huo. Zeinab Toghyani na ahtab Taji Rostammabadi wa mkoa wa Esfahan katikati mwa Iran waliibuka wa pili na wa tatu kwa utaratibu huo, katika safu ya wanataekwondo wenye umri wa miaka 15 na 17 kwenye mashindano hayo ya wanafunzi yanayofahamika kwa Kiingereza kama World School Taekwondo Poomsae Championship.

Michezo Afrika

Shirikisho la soka Afrika (CAF) limetangaza rasmi ratiba ya mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) na Kombe la Dunia, ambayo yanarejea baada ya kusimama kwa muda mrefu kutokana na tatizo la virusi vya Corona. Ratiba iliyotolewa juzi na Caf, imeonyesha kuwa mechi za kuwania kufuzu fainali za Afcon mwaka 2021 zitakazofanyika Cameroon na zile za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar mwaka 2022 zitachezwa kuanzia Novemba 9 mwaka huu na zitahitimishwa rasmi Novemba 16 mwaka huu. Baada ya kuchezwa kwa raundi mbili ambazo ni ya kwanza na ya pili, mechi za raundi ya nne na ile ya tano ya mashindano ya kuwania kufuzu Afcon 2021, zimepangwa kuchezwa kati ya Novemba 9 hadi 15 mwaka huu kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa na Caf.

Huku hayo yakijiri, Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), limefungua dirisha la usajili na uhamisho wa wachezaji kwa msimu wa 2020/21 likitarajiwa kufungwa Septemba 19, mwaka huu. Dirisha hilo la usajili limefunguliwa kwa timu za Ligi Kuu ya Zanzibar kwa upande wa wanaume, Ligi Kuu ya Wanawake, Ligi ya Mikoa pamoja na Ligi za Wilaya. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Mashindano wa ZFF, Ali Mohmmed Ameir, imesema msimu huu klabu zitasajili kwa njia ya kielektroniki badala ya kujaza fomu kwa mkono kama ilivyozoeleka kwa misimu ya iliyopita.Alisema ingawa kwa sasa njia hiyo italeta changamoto kwa baadhi ya klabu, lakini shirikisho hilo litazidi kutoa elimu ili kila klabu iweze kufanya usajili kwa wakati kwa kutumia njia ya kielektroniki. 

Na mwanariadha bingwa wa Kenya, Timothy Cheruiyot aliibuka kidedea katika Mashindano ya Ligi ya Almasi jijini Stockholm na kutwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 upande wa wanaume siku ya Jumapili.  Cheruiyot alikata utepe kwa kutumia dakika 3:30.25. Mkenya mwingine, Ferguson Rotich ambaye ni mshindi wa medali ya shaba katika mbio za mita 800 aliambulia nafasi ya nne katika mashindano hayo ya Jumapili ya mita 1,500. Nafasi ya pili ilitwaliwa na raia wa Norway, Jakob Ingebrigtsen huku orodha ya tatu bora katika mbio hizo zilizofanyika nchini Sweden ikifungwa na Muaustralia, Stewart Mcsweyn.

Finali za Ligi ya Champions na Uropa

Kombe la Klabu Bingwa Ulaya lilifika tamati Jumapili hii kwa mechi ya kukata na shoka kati ya klabu ya Paris Saint Germain PSG ya Ufaransa na Bayern Munich ya Ujerumani. Bayern Munich imenyakua ubingwa wa Champions League kwa mara ya sita baada ya kuifunga PSG bao moja kwa nunge katika fainali iliyochezwa usiku wa kuamkia Jumatatu mjini Lisbon, Ureno. Bao la ushindi lilipachikwa wavuni katika dakika ya 59 na mshambuliaji Kingsley Coman aliyewastaajabisha mahasimu wao klabu ya PSG ya Ufaransa iliyokuwa ikimezea taji hilo la klabu bingwa barani Ulaya.

Wachezaji wa Bayern wakifurahia kombe walilolitwaa

 

Bayern ambayo ilinyakua pia ubingwa wa ligi ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga, imeondoka na kikombe cha Champions League kwa fahari baada ya kutopoteza mchezo hata moja kwenye mashindano hayo. Mamia ya wafuasi wa klabu hiyo katika mji wa nyumbani wa Munich walisherehekea ushindi wa timu yao kwa kumiminika barabarani wakipuliza firimbi na honi za magari. Wakati huo huo polisi mjini Paris ililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya mashabiki wa klabu ya PSG waliozusha vurugu baada ya timu hiyo kupoteza mchezo na Bayern na kulikosa kombe la Champions League.

Kwengineko, miamba ya soka nchini Uhispania, Sevilla waliweka rekodi ya kutawazwa mabingwa wa Europa League kwa mara ya sita baada ya kupepeta Inter Milan ya Italia 3-2 kwenye fainali iliyowakutanisha mjini Cologne, Ujerumani mnamo Ijumaa. Mechi hiyo ilianza kwa Romelu Lukaku kutikisa nyavu kabla ya nyota huyo wa zamani wa Everton na Manchester United kujifunga mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kushindwa kudhibiti mpira uliopigwa na beki Diego Carlos aliyesababisha penalti iliyofungwa na Lukaku. Ina maana kwamba Inter ya kocha Antonio Conte itasubiri zaidi kabla ya kujinyanyulia taji la kwanza ambalo wamekuwa wakilisaka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita. Bao la Lukaku lilikuwa lake la 34 msimu huu. Ni ufanisi uliomfanya kuwa mwanasoka wa kwanza kuwahi kufunga katika jumla ya mechi 11 mfululizo za Europa League. Mabao mengine ya Sevilla yalifungwa na Luuk de Jong kupitia krosi za Jesus Navas na Ever Banega kabla ya beki Diego Godin kufungia Inter katika dakika ya 35.

Ubingwa huo unakuwa ni wa sita kwa Sevilla na ndio inakuwa klabu pekee ambayo imechukua mara nyingi zaidi katika historia ya michuano hiyo. Kwa kocha Julen Lopetegui wa Sevilla, hilo lilikuwa taji lake la kwanza kutwaa tangu apokezwe mikoba ya kikosi hicho ambacho kwa sasa hakijapoteza mechi yoyote kati ya 21 zilizopita tangu Februari mwaka huu.

Na kwa kutamatisha, Ronald Koeman amepokezwa mikoba ya Barcelona siku mbili baada ya miamba hao wa soka ya Uhispania kumtimua mkufunzi Quique Setien. Koeman, 57, amesajiliwa na Barcelona kwa miaka miwili baada ya kushawishiwa kuagana na timu ya taifa ya Uholanzi wakati akisalia na miaka miwili kwenye mkataba wake na kikosi hicho. Koeman aliwahi kuchezea Barcelona kati ya 1989 na 1995 na akawasaidia kunyanyua mataji manne ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Katika kampeni za msimu huu, Barcelona walikamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya pili na kukosa kutwaa taji kwa mara ya kwanza tangu 2007-08. Pengo la alama tano lililodumu kati ya Barcelona na Real Madrid na kichapo kikali cha 8-2 ambacho kikosi hicho kilipokezwa na Bayern Munich kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, ni kiini cha Barcelona kukatiza uhusiano wao na Setien. Kutokana na kichapo hicho cha mbwa kuingia msikitini, Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi ameiambia klabu hiyo kuwa anataka kuondoka kutafuta maisha mengine, huku Manchester City ikiwa ni timu pekee inayoonyesha shauku ya kutaka kumsajili. Kwa mujibu wa mtandao wa ‘Esporte Interativo’ wa Hispania Messi 33, anashinikiza kuondoka kutokana na matokeo mabaya yanayoikumbu timu.

………………….TAMATI…..………..

 

 

 

Tags