Sep 07, 2020 08:06 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Sep 7

Hujambo mpenzi mwanaspoti wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.

Iran Soka: Teractor waondoka na Kombe la Hazfi

Klabu ya soka ya Teractor Sazi ya Iran imetwaa Kombe la Mtoano (Hazfi) baada ya kupata ushindi hafifu wa mabao 3-2 dhidi ya Esteqlal katika mechi ya fainali iliyochezwa Alkhamisi. Katika mchuano huo wa aina yake uliopigwa katika Uwanja wa Imam Ridha AS mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran, Watengeneza Matrekta wa Iran walitumia vizuri fursa zilizotokana na makossa ya kizembe ya vijana wa Tehran, na hivyo kuishia kupata ushindi, japo kwa mbinde na kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili. Teractor ilitamalaki kipindi cha kwanza kwa mabao 3 kwenye mchuano huo, kiasi cha kuifanya Esteqlal isione lango lao. Mabao hayo ya kipindi cha kwanza ya Teractor yalifungwa na Mohammadreza Khanzadeh (17), Ashkan Dejagah (34), na Akbar Imani (41). Katika kipindi cha pili, Esteqlal walirejea kwa ari na kasi mpya ungedhani wataibuka kidedea katika fainali hii.

Hata hivyo walifanikiwa kucheka na nyavu za Teractor mara mbili tu kupitia mabao ya mtoka benchi, Mehdi Ghaedi dakika ya sita baada ya kuanza kipindi cha pili, na Arsalan Motahari dakika ya 79 ya mchezo.

Awali Esteqlal iliwabanjua mahasimu wao wa jadi, klabu ya Persepolis katika mechi ya nusu fainali na kujikatia tiketi ya fainali. Licha ya kichapo hicho cha wastani cha Alkhamisi, lakini Esteqlal inasalia kuwa klabu iliyotwaa Kombe la Hazfi mara nyingi zaidi katika historia ya taji hilo la muondoana lililoasisiwa mwaka 1975 na Shirikisho la Soka Iran. Vijana wa The Blues ya Tehran wametwaa taji hilo mara saba.

Uogeleaji: Mwanamke Muirani aweka rekodi mpya 'Guiness Book'

Mwanamke muogoleaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameweka rekodi mpya katika Daftari la Kumbukumbu la 'Guiness Book of World Records', baada ya kuogelea umbali wa kilomita 10 katika Bahari ya Oman huku akiwa amevalia vazi la staha la hijabu. Elham Sadat Asghari ameweka rekodi mpya kwa kuogelea umbali huo kwa mkono mmoja na kwa kutumia masaa manne na dakika 59. Hii sio mara ya kwanza kwa bingwa huyo wa mashindano ya kuogelea wa Iran kuingia katika daftari hilo la kihistoria. Mwaka 2019, mwanamke huyo wa Kiirani alipigiwa saluti na Daftari la Kumbukumbu la Guiness, baada ya kuogelea umbali wa mita 5,488 katika Bahari ya Caspian na kidimbwi cha kuogelea hapa mjini Tehran, huku akiwa na pingu mikononi.

Elham Sadat Asghari

 

Aidha mwaka 2017, Elham Sadat Asghari mwenye umri wa miaka 37 aliiweka Jamhuri ya Kiislamu katika ramani ya dunia kwa kuogelea akiwa na pingu mikononi kwa zaidi ya masaa matatu mfululizo, katika mji bandari wa Bushehr, kusini magharibi mwa Ghuba ya Uajemi, yapata kilomita 1,050 kusini mwa mji mkuu Tehran.

Kuanza Ligi Kuu ya Soka Tanzania

Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ilianza kitifua vumbi Jumapili hii ya Septemba 6. Mechi sita zimepigwa wikendi, lakini mchuano uliokuwa na msisimko zaidi ni ule kati ya Simba na Ihefu FC ambapo kama ilivyotarajiwa, Simba ilinguruma. Magoli ya John Bocco na Mzamiru Yassin yaliwapa ushindi mabingwa hao watetezi huku Ifehu FC ikipata moja la kufutia machozi. Wageni wa Ligi Kuu msimu huu, Dodoma Jiji FC ambao wamepanda daraja wamepata ushindi wa kwanza baada ya kuiadhibu Mwadui FC bao 1 bila jibu. Katika timu tatu zilizopanda ligi kuu msimu huu, mbili zimepoteza mechi zake. Gwambina wakiwa ugenini dhidi ya Biashara United wamefungwa goli 1-0. Klabu ya Yanga imeanza vibaya msimu kwa kukubali kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Tanzania Prisons. Kocha mkuu wa Yanga, Zlatko Krmpotic amesema wachezaji wake hawakuwa sawa kimwili kuweza kucheza dakika zote na ndiyo sababu iliyopelekea kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Wanagereza hao. Shaban Kazumba, Kocha Msaizidi wa Prisons ameonekana kuridhishwa na sare hiyo kwa kuwa kikosi chake kilicheza na miamba ya kabumbu Tanzania Bara. Katika matokeo ya mechi zingine za ufunguzi zilizopigwa, Mtibwa Sugar iliambulia sare ya 0-0 dhidi ya Ruvu Shooting, wakati ambapo Namungo walikuwa wakiiadhibu Coastal bao 1-0.

Riadha: Mkenya aweka rekodi mpya

Mwanariadha wa Kenya Peres Jepchirchir ameweka rekodi ya dunia katika mashindano ya mbio za nusu marathon kwa wanawake kwa kutumia saa 1, dakika 5 na sekunde 34.  Jepchirchir mwenye umri wa miaka 26 ameibuka na ushindi huo katika mbio zilizofanyika katika uwanja wa Letna Park katika mji mkuu wa Jamhuri ya Czech, Prague. Rekodi ya awali ambayo ilikuwa ya saa 1, dakika 6 na sekunde 11, iliwekwa mwaka 2018 na Netsanet Gudet wa Ethiopia. Rekodi hiyo iliwekwa katika mashindano ya kutafuta bingwa wa nusu marathoni yaliyifanyika Valencia, Uhispania.

Dondoo za Hapa na Pale

Habari ifuatayo, inasikitisha na inachekesha kwa wakati mmoja, lakini pia inashangaza. Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Misri, EFA, Ahmed Shobir amesema kombe la AFCON limepotea katika makao makuu ya Shirikisho hilo. Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON lilikuwa limehifadhiwa Misri baada ya timu ya Mafarao kushinda kwa mara tatu mfululizo tangu mwaka 2006 hadi 2010. Watendaji wa Shirikisho hilo wamedai ya kuwa kombe hilo lilikuwa limehifadhiwa kwa nahodha wa timu ya taifa, Ahmed Hassan. Hassan ambaye naye amekanusha hilo na kusema alikaa nalo kwa siku moja baada ya kushinda na alilikabidhi tangu mwaka 2011. Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Misri, EFA, Ahmed Shobir amesema kombe la AFCON limepotea katika mazingira ya kutatansisha katika makao makuu ya shirikisho hilo nchini Misri.

Lionel Messi

 

Kwengineko, nguli wa soka, Lionel Messi hakuonekana katika kambi ya mazowezi  ya klabu yake ya Barcelona Jumamosi hii ya Septemba 5, licha ya uamuzi wa kubakia katika  klabu hiyo kwa makubaliano maalumu.  Nyota huyo wa Argentina alitangaza  siku  ya Ijumaa  kuwa  amelazimika  kubakia Barcelona, akidai  ni  baada  ya  rais wa klabu  hiyo Josep Maria Bartomeu  kukiuka  kauli yake  ya kumwachia  aondoke. Jumapili iliyopita Messi kwa makusudi mazima  aliepa kufanyiwa  vipimo vya lazima vya virusi  vya  corona ambavyo  wachezaji  wote  wa  Barcelona  wanalazimika  kufanyiwa.

Na klabu ya soka ya Ufaransa PSG imethibitisha kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa wachezaji wake watatu wana ugonjwa wa Covid-19. Wachezaji hao ni Ángel Di María, Leandro Paredes na Neymar Jnr. Ili kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona miongoni mwa wachezaji, klabu hiyo imechukua hatua za kuwaweka karantini wachezaji hao.

……………………..TAMATI….…………..

 

 

Tags