Sep 18, 2020 02:40 UTC
  • Ijumaa, tarehe 18 Septemba, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria inayosadifiana na Septemba 18 mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo, miaka 539 iliyopita alifariki dunia Muhammad Heravi, mwanahistoria wa Kiislamu huko Herat, magharibi mwa Afghanistan ya leo. Heravi alizaliwa katika familia maarufu huko Balkh kaskazini mwa nchi hiyo lakini aliishi zaidi katika mji wa Herat. Kutokana na elimu yake kubwa, alipewa heshima na mazingatio makubwa na Ali-Shir Nava'i, waziri mwanasayansi wa silsila ya watawala wa Gurkhani, ambaye alikuwa akiwaheshimu sana wasomi na wanazuoni. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Tarikh Raudhati Safaa kinachochunguza historia ya dunia tangu kuumbwa kwake hadi zama za msomi huyo. 

Katika siku kama ya leo miaka 311 iliyopita, alizaliwa Samuel Johnson mwandishi wa drama, malenga na mwandishi wa visa wa Kiingereza. Alianza shughuli zake za fasihi sambamba na ukosoaji wake katika taaluma hiyo. Baada ya muda mwanatamthilia huyo aliingia katika uga wa utunzi wa mashairi. Samuel Johnson aliaga dunia mwaka 1784.

Samuel Johnson

Katika siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, nchi ya Chile ilipata uhuru. Mwaka 1536 Chile ilidhibitiwa na Hispania. Sehemu kubwa ya kukoloniwa Chile, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Naibu Mfalme wa Uhispania nchini Peru.

Bendera ya Chile

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita yaani tarehe 18 Septemba mwaka 1961 aliaga dunia Dag Hammarskjold mwanasiasa na Katibu Mkuu wa Pili wa Umoja wa Mataifa. Mwanasiasa huyo wa nchini Sweden alifariki dunia baada ya ndege iliyokuwa imembeba wakati wa safari yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanguka. Hammarskjold alikuwa Congo kwa lengo la kufanya mazungumzo na pande husika ili kumaliza vita vya ndani nchini humo. Mwanasiasa huyo alizaliwa mwaka 1905 na alihesabiwa katika zama zake kuwa mmoja kati ya waandishi stadi nchini Sweden. Mwaka 1952, Dag Hammarskjold alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobeli kutokana na harakati zake za kuimarisha amani duniani.

Dag Hammarskjold

Na miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Susangerd moja kati ya miji ya magharibi mwa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Iran na hivyo kuondoka katika uvamizi wa vikosi vya utawala wa Kibaathi wa Iraq. Ushindi huo mkubwa ilikuwa matokeo ya ushirikiano na uratibu wa karibu baina ya vikosi vya jeshi na makundi ya wananchi.

Ramani ya eneo la Susangerd

 

Tags

Maoni