Sep 26, 2020 06:38 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (15)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

Kipindi chetu kilichopita kilimazilia kumzungumzia  Abu Ja’far Muhammad bin Hassan Tusi mashuhuri kwa jina la Sheikh at-Taifah au Sheikh Tusi fakihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mahiri na mashuhuri wa Kishia. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali za elimu za Kiislamu. Hii leo kuna athari takribani 50 zilizobakia. Athari za mwanazuoni huyo hivi sasa zimeratibiwa na kuchapishwa katika sura ya Dairatul-Maarif yaani Ensaiklopidia ambayo ni seti ya vitabu vinavyotoa taarifa kuhusu mambo mengi. Vitabu viwili kati ya vitabu vinne muhimu vya hadithi kwa Waislamu wa Kishia vinavyojulikana kwa jina la Kutub al-Ar’baa ambavyo ni Tahdhib al-Ahkam na Al-Istibsar vimeandikwa na Sheikh Tusi. Aidha tulieleza kwamba, Sheikh Tusi amezikwa katika mji wa Najaf, Iraq. Sehemu ya 15 ya kipindi chetu juma hili itamzungumzia Sheikh Fadhlu bin Hassan Tabarsi mwandishi wa tafsiri ya Qur’ani ya Majmaa al-Bayan. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Fadhl bin Hassan Tabarsi

 

Fadhl bin Hassan Tabarsi aliyelaziwa mwaka 468 Hijria na kufariki dunia mwaka 548 ni mmiongoni mwa maulamaa wakubwa wa Kishia na mfasiri wa Qur’ani Tukufu katika karne ya tano na ya sita Hijria. Sheikh Tabarsi ana vitabu kadhaa vya tafsiri ya Qur’ani. Hata hivyo tafsiri ya Majmaa al-Bayan ndicho kitabu chake kilichompatia umashuhuri zaidi na anajulikana zaidi kwa kitabu hicho. Allama Majlsi alikuwa akiamini kwamba, neno Tabarsi ni la Kiarabu na limetoholewa ambapo neno la Kifarsi ni Tafresh na ndio maana alikuwa akimhesabu Sheikh Tabarsi kwamba, ni mkazi asili wa Tafresh moja ya viungwa vya mji wa Qum.

Familia ya Tabarsi ilikuwa moja ya familia mashuhuri baina ya Waislamu wa Kishia. Baba yake Fadhl yaani mzee Hassan alikuwa mmoja wa Maulama mahiri katika zama zake. Wtoto wake pia yaani Radhiuddin na Hassan bin Fadhl Tabarsi nao waliondokea kung’ara kama nyota za mbinguni kielimu, uchaji-Mungu na kuipa mgongo dunia. Alikuwa miongoni mwa wanafunzi hodari wa baba yake na alimu huyu ameandika vitabu vingi kikiwemo cha Makarim al-Akhlaq. Fadhl bin Hassan Tabarsi alikipindi kipindi chake cha masomo wakati wa utoto na ujana wake jirani na Harama ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) katika mji wa Mash’had.

Moja ya vitabu vyya Sheikh Fadhl bin Hassan Tabarsi

 

Baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi alianza kusoma kwa bidii na juhudi kubwa maarifa ya Kiislamu na kushiriki darsa na vikao vya elimu vya waalimu na wasomi mahiri wa zama hizo. Alifanya hima na idili kubwa kujifunza elimu mbalimbali kama fasihi ya kugha ya Kiarabu, tafsiri, hadithi, fikihi, itikadi na Usul al-Fikih kiasi kwamba, akaondokea kuwa mahiri katika elimu zote hizo. Licha ya kuwa katika zama hizo, elimu kama vile, hisabati hazikuwa zimeenea sana lakini Tabarsi alifanya hima ya kujifunza hisabati na kuondokea kuwa mmoja wa wasomi wenye nadharia katika elimu hiyo.

 

Maulama wakubwa na wataalamu wa kuelezea habari na historia zawatu, wanamtaja Sheikh Tabarsi kama alimu, mujitahidi na fakihi mkubwa. Sheikh Tabarsi alibaibnisha kwa mara ya kwanza nadharia na mitazamo ya makundi mbalimbali ya Kiislamu na baada ya kubainisha mtzamo wa Mashia na alibainisha nadharia yake kwa nuania ya fatwa. Akthari ya mafakihi wakubwa wa Kishia walikuwa wakiuheshimu mtazamo wake.

Sheikh Tusi aliishi katika mji wa Mash’had kwa muda wa takribani miaka 54 na kisha mwaka 523 alielekea katika mji wa Sabzawar akiitikia mwito wa shakhsia wakubwa wa mji huo. Sheikh Tusi alifanya hivyo kutokana na kuwa katika mji huo kulikuwa na suhula nyingi zilizokuwa zikimuandalia mazingira mazuri ya kufundisha, kualifu na kueneza mafundisho ya Kiislamu.

Tafsiri ya Maj'maul Bayan ya Sheikh Fadhl bin Hassan Tabarsi ni miongoni mwa tafsiri mashuhuri za Qur'ani Tukufu

 

Hatua ya kwanza aliyoichukua baada ya kuwasili katika mji wa Sabzawar ni kukubali kuchukua jukumu kusimamia Chuo cha Kidini mjini humo kilichojulikana kwa jina la Chuo cha Mlango wa Iraq. Kwa hima, bidii na miongozo yake, chuo hicho kiliondokea kuwa chuo kikubwa cha kidini na kilichokuwa na umuhimu mkubwa. Utajiri wa utamaduni na elimu wa eneo hilo, uliwavutia wengi hasa vijana waliokuwa na kiu cha elimu ambao waliokuwawakitokea katika maeneo mbalimbali ya Iran na kwenda kusoma katika mji huo. Katika kipindi cha mudawa miaka 25 alioishi mjini Sabzawar, Sheikh Tabarsi alifanikiwa kuwalea wanafunzi wengi.

 

Athari na kumbukumbu muhimu zaidi ya Sheikh Tabarsi ni kitabu cha tafsiri ya Qur’ani ya Majmaa al-Bayan. Allama Amini ameandika hivi kuhusiana an daraja ya kielimu ya Sheikh Tabarsi: Amin al-Islam, mashuhuri kwa jina la Sheikh Tabarsi alikuwa mbeba bendera ya elimu na uongofu. Alikuwa mmoja wa viongozi mahiri wa kidini na madhehebu ya Shia. Tafsiri yake ya Majmaa al-Bayan, ilikuwa inatosha kabisa kubainisha bahari ya elimu na ubobezi mkubwa aliokuwa nao katika uga wa elimu. Tafsiri ambayo inatoa nuru ya ukweli, kitabu ambacho hakuna mtu ambaye anaweza kudaia kwamba, hakihitajii.” Mwisho wa kunuu.

Sheikh Tabarsi alitumia muda wa miaka 7 kuaindika tafsiri ya Majmaa al-Bayan akipata muongozo wa tafsiri ya Tibyan ya Sheikh Tusi. Tafsiri ya Majmaa al-Bayan imewavutia Maulamaa wengi hata wa madhehebu ya Kisuni.

Kitabu cha Tafsiri ya Majmaa al-Bayan kina mijalada kumi na imechapishwa katika mijalada mitano.

Sheikh Tabarsi ambaye anafahamika pia kwa lakabu ya Imam wa wafasiri aliaga dunia tarehe 9 Mfunguo Tatu Dhul-Hijaa mwaka 548 Hijria na kurejea kwa Mola wake baada ya kuishi kwa miaka 80, umri ambao ulijaa baraka na fadhila. Baadhi ya waandishi wanamtaja Sheikh Tabarsi kama shahidi kwani wanasema kuwa, aliuawa kwa kupewa sumu.

Mahala lililo, kaburi la Sheikh Fadhl bin Hassan Tabarsi, Mash'had jirani na haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as).

 

Mwili wa Sheikh Tabarsi ulihamishwa kutoka Sabzawar na kwenda kuzikwa jirani na haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as).

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa, nikitaraji kuwa mtajiunga nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Tags