Sep 28, 2020 08:25 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Septemba 28

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Persepolis yatamba Ligi ya Mabingwa ya AFC

Klabu ya Persepolis ya Iran siku ya Jumapili ilishuka dimbani kuvaana na al-Sadd ya Qatar katika Uwanja wa Mji wa Elimu mjini Doha na kuibuka na ushindi mwembamba katika dakika za lala salama, katika mchuano wa Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia (AFC Champions League). Wekundu wa Tehran walipata bao la kipekee na la ushindi katika dakika ya 88 ya mchezo, kupitia goli la kichwa la Issa Alekasir. Persepolis ilitinga hatua hii baada ya kuinyoa kwa chupa klabu ya Sharjah ya Umoja wa Falme za Kiarabu mabao 4-0 siku ya Alkhamisi. Klabu hiyo ya Qatar inayonolewa na mchezaji wa zamani wa Bercelona, Xavier Harnades (Xavi) iliiweka Persepolis chini ya mashinikizo makubwa katika dakika za lala salama, lakini ilishindwa kucheka na nyavu za klabu hiyo ya Iran. Kwa ushindi huo, Persepolis ya Iran imesonga mbele hadi hatua ya robofainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Iran, Mahdi Mohammad Nabi ameipongeza Persepolis kwa kutinga robo fainali ya ligi hiyo ya kikanda.

Mchezaji wa Persepolis akimpiga chenga hasimu

 

Wakati huohuo, klabu ya Esteqlal ya Jamhuri ya Kiislamu ya ilishindwa kufurukuta mbele ya klabu ya Pakhtakor ya Uzbekistan katika mechi ya Mzunguko wa 16 ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia (AFC Champions League). Pakhtakor ilitoka nyuma na kuizaba Esteqlal mabao 2-1 katika mchezo wa Jumamosi uliopigwa katika Uwanja wa Al Janoub nchini Qatar. Esteqlal ilikuwa ya kwanza kuona langu la mahasimu kupitia bao la dakika ya 32 ya Ali Karimi. Na kwa kuwa kutangulia si kufika, Pakhtakor walikaza mikanda na kufanya mambo kuwa sawa bin sawa dakika mbili kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza. Timu hiyo ya Uzbekistan ilipata la ushindi dakika chache baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza kipindi cha pili, kupitia bao la Erin Deriyok. Kwa ushindi huo Pakhtakor imejikatia tiketi ya kusonga mbele, huku Esteqlal wakibanduliwa. The Blues ya Tehran ilifikia hatua hii baada ya kuichabanga mabao 3-0 al-Ahli ya Saudia katika kitimutimu cha Jumatano. Sepahan na Shahr Khodro ni timu zingine mbili za Iran zilizoondolewa kwenye dimba hilo la kieneo.

Riadha: Ligi ya Almasi

Mwanariadha bingwa mara tatu wa dunia Mkenya Hellen Obiri, aliandikisha muda bora zaidi duniani katika kampeni za Wanda Diamond League kwa mara ya pili mwaka huu 2020 siku ya Ijumaa. Malkia huyo wa mbio za mita 5,000 duniani alikamilisha mbio za mita 3,000 katika mbio za Ligi ya Almasi (Doha Diamond League) jijini Doha nchini Qatar kwa dakika 8:22.54 na kukaribia dakika 8:20.68 ambao ndio muda bora zaidi anaojivunia katika fani hiyo. Obiri aliwahi kutamalaki duru ya kwanza ya Diamond League msimu huu alipokamilisha mbio za mita 5,000 kwa muda bora wa dunia (dakika 14:22.12) huko Monaco mnamo Agosti 14.

 

Alisalia katika nafasi ya pili kwa muda mrefu jijini Doha huku akisoma mgongo wa Mkenya mwenzake Winny Chebet aliyefikia hatua ya mita 1,000 kwa muda bora wa dakika 2:48.46 kabla ya kupitwa na Obiri. Zikisalia mita 500 pekee, Beatrice Chepkoech alichukua usukani kutoka kwa Obiri ila bingwa huyo wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji hakuongoza kwa kipindi kirefu kabla ya kuzidiwa maarifa na Obiri katika mita 300 za mwisho. Licha ya ushindani mkali kutoka kwa Wycliffe Kinyamal, Erik Sowinski wa Marekani na Muingereza Giles Elliot, Mkenya Ferguson Rotich aliibuka mshindi wa mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume jijini Doha. Aliandikisha muda wa dakika 1:44.17 na kumpiku bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot.

Simba Hoyee!

Klabu ya Simba inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania ndiyo yenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa kijamii wa Instagram. Klabu hiyo imezifunika timu nyingi Afrika ikiwa ni pamoja na Klabu ya Al Ahly ya Misri kutokana na kushika namba moja kwenye mtandao wa IG. Hayo ni kwa mujibu wa wavuti wa Deporfinanzas ambao umetoa ripoti ya mwezi Agosti mwaka huu, na kuiweka Simba namba moja kwa umaarufu kutokana na kutembelewa sana na watu. Takwimu zinaonyesha kwamba kwa mwezi huo watu milioni 536 waliitembelea akaunti ya Simba huku ile ya Al Ahly ikitembelewa na watu milioni 517 na Raja Casablanca watu milioni 511. Hii ni mara ya Kwanza kwa timu kutoka Tanzania kung'ara kiasi hiki.

Wachezaji wa Simba uwanjani

 

Dondoo za Hapa na Pale

Mabingwa wa UEFA Champions League FC Bayern Munich ya Ujerumani wamewaonesha Ubabe Mabingwa wa Europa League klabu ya Sevilla FC kutokea Hispania katika mchezo wa fainali wa UEFA Super Cup. Mchezo huo uliochezwa Budapest Hungary umemalizika kwa FC Bayern Munich kuwa Bingwa wa Kombe hilo kwa kuifunga Sevilla magoli 2-1 mchezo ambao ulilazimika dakika 90 na kwenda dakika 120 ili kupata mbabe. Ushindi huo unaifanya FC Bayern Munich ndani ya mwaka 2020 kuwa imepata ushindi katika mchezo wa 23 mfululizo lakini ni mchezo wao wa 32 wakicheza bila kupoteza na hilo ndio taji lao la nne ndani ya mwaka huu.

Huku hayo yakijiri, usimamizi wa UEFA umetoa orodha ya majina matatu ya wachezaji ambayo ndiyo yameingia kwenye tatu bora kuwania tuzo hiyo na kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya Mwongo mmoja kupita majina maarufu na yaliyozoeleka katika kuzichukua tuzo hizi, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wamekosekana. Majina ya wachezaji Robert Lewandowski na Manuel Neuer kutokea Bayern Munich, na la tatu likiwa ni la kijana wa Manchester City, Kevin De Bruyne ndiyo yaliobahatika kuingia tatu bora na hatmaye kupatikana mchezaji bora wa mwaka kwenye tuzo zitakazotolewa siku ya Alhamisi ya tarehe 1 Oktoba. Nyota huyo wa Barcelona, Messi ametwaa tuzo hiyo katika mwaka 2010-11 na 2014-15 na jina lake limeingia kwenye kinyang'anyiro hicho zaidi ya mara sita ndani ya misimu 10.

Mbwana Samatta

 

Na mshambuliaji wa timu ya soka nchini Tanzania Mbwana Samatta amejiunga na klabu ya Uturuki Fenerbahce kwa mkataba wa miaka minne kutoka Aston Villa. Klabu hiyo imeandika katika mtandao wake kwamba imemuongeza nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania katika kikosi chake kwa mkataba wa miaka minne.Mchezaji huyo aliyeshinda taji la mfungaji bora mara kadhaa nchini Ubelgiji kabla ya kujiunga na Aston Villa nchini Uingereza atahudumu katika klabu hiyo kwa mkopo wa mwaka mmoja kabla ya kuandikisha kandarasi ya kudumu ya miaka minne. Samatta alianza kibarua kwa kushiriki debi la Uturuki linayozikutanisha Galatasary na Fenerbahce na mchezo huo kumalizika kwa sare ya kutokufungana. Samatta aliingia dakika ya 66 akichukua nafasi ya Mame Thiam akiwa na jezi namba 10 mgongoni alionekana kusumbua mabeki wa timu pinzani licha ya kupata mpira mara chache. Straika huyo amejiunga na timu Fenerbahce kwa mkopo wa mwaka wa mmoja akitokea Aston Villa ya Ligi Kuu ya Uingereza. Samatta katika dakika alizocheza ameokoa mpira wa adhabu kwa kichwa uliokuwa ukienda langoni kwao na kutoa pasi ya shambulizi ambayo haikuzaa matunda. Kuondoka Samatta Uingereza na kutua Uturuki kumepokea na hisia mseto na mashabiki zake.

.............................TAMATI....................

 

Tags