Oct 12, 2020 08:05 UTC
  • Biashara ya kidijitali yastawi wakati wa janga la Corona

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matikio muhimu ya sayansi na teknolojia duniani. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa nami hadi mwisho. @@@

Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo UNCTAD linasema utafiti umebaini kuwa janga la corona au COVID-19 limebadili mtazamo wa watu kuhusu kuelekea zaidi kwenye ulimwengu wa kidijitali.

Utafiti huo uliofanyika kwa njia ya mtandao umeonesha kwamba mabadiliko ya tabia ya manunuzi mtandaoni huenda yakawa na athari za muda mrefu.

Kwa mujibu wa UNCTAD utafiti huo “COVID-19 na biashara mtandaoni” uliohusisha wateja 3,700 katika nchi 9 zinazoendelea na zilizoendelea umedhihirisha kwamba janga la COVID-19 limebadili tabia ya manunuzi ya mtandaoni daima.

Utafiti huo umetathimini jinsi gani janga hili lilivyobadili njia za wanunuzi kutumia biashara ya mtandaoni na suhula za kidijitali na umejumuisha nchi za Brazil, China, Ujerumani, Italia, Jamhuri ya Korea, Urusi, Afrika Kusini, Uswisi na Uturuki.

Kwa mujibu wa utafiti huo kufuatia janga la COVID-19 zaidi ya nusu ya watu waliofanyiwa utafiti wamesema sasa wananunua vitu mtandaoni mara nyingi na wanategemea intaneti zaidi kwa kupata habari, taarifa kuhusu masuala ya afya na burudani.

Utafiti huo unasema, wanunuzi kutoka nchi zinazoendelea ndio waliofanya mabadiliko makubwa ya kuingia mtandaoni kununua bidhaa.

Janga la COVID-19 limeongeza kasi ya hulka ya kuingia kwenye ulimwengu wa kidijitali. Mabadiliko tunayofanya sasa yatakuwa na athari za muda mrefu wakati uchumi wa dunia ukianza kuchipuka tena.” Amesema Mukhisa Kituyi Katibu Mkuu wa UNCTAD.

Ameongeza kuwa ongezeko la kasi la manunuzi mtandaoni duniani kote linadhihirisha uharaka wa kuhakikisha kwamba nchi zote zinaweza kunufaika na fursa hizo zinatoletwa na ulimwengu wa kidijitali wakati dunia ikiondokana na janga la COVID-19.

Utafiti huo uliofanywa kwa pamoja na UNCTAD na jumuiya ya biashara mtandaoni ya Uswisi Netcom zikishirikiana na kituo cha mtandao wa Habari cha Brazil NIC.Br na Inveno umeonyesha kwamba manunuzi mtandaoni yameongezeka kwa asilimia 6 hadi 10 katika bidhaa mbalimbali. 

Na walionufaika zaidi na biashara hizo ni makampuni ya teknolojia ICT, bidhaa za kielektroniki, bidhaa za bustani, vitu vya kujitengenezea, makampuni ya madawa, elimu, samani, bidhaa za nyumbani na vipodozi na vifaa vya usafi binafsi na kujilinda. 

Ripoti hiyo pia imebaini kwamba sekta za utalii na usafiri zimeathirika sana kwa kupoteza pato kubwa ambapo kwa wastani manunuzi ya mteja yameshuka kwa asilimia 75 kwa bidhaa hizo za utalii na safari. 

Utafiti huo umebaini pia kwamba wanawake na watu wenye elimu ya juu wameongeza manunuzi yao mtandaoni kuliko watu wengine.  

Pia watu wenye umri wa kati ya miaka 25 na 44 ndio kundi lililoongeza zaidi manunuzi mtandaoni ikilinganishwa na makundi yenye umri mdogo. 

Kwa mujibu wa utafiti huo majukwaa ya kidijitali yanayotumika zaidi kwa mawasiliano ni Whatsapp, Instagram na Facebook Messenger, yote yakimilikiwa na Facebook. 

Hata hivyo Zoom na Microsoft Teams ni majukwaa yaliyofaidika sana kutokana na ongezeko la matumizi ya upigaji simu kwa njia ya video katika maeneo ya kazi. 

Nchini China majukwaa ya mawasiliano yanayoshika nafasi ya juu ni WeChat, DingTalk na Tencent Conference, umesema utafiti huo. 

Matokeo ya utafiti huo yanapendekeza kwamba mabadiliko haya katika shughuli mtandaoni yana uwezekano wa kuendelea hata baada ya janga la COVID-19. 

Ufugaji wanyama unaweza kuibua janga jipya mithili ya corona

Ripoti mpya ya Shirika la kulinda maslahi ya wanyama la Uingereza la World Animal Protection, inatahadharisha kuwa mifumo ya ufugaji wanyama ya kisasa inaweza kuchangia kusababisha baa jipya la afya mithili ya COVID-19.

Hii ni kwa sababu ya matumizi ya dawa za kuua bakteria ambazo hutumika kwa wingi kwa wanyama wanaofugwa kwa sababu ya mayai, maziwa na nyama. Kulingana na ripoti ya shirika hilo la ulinzi wa wanyama, matumizi ya muda mrefu ya dawa za kuua wadudu huenda yakazifanya zisiwe na taathira, kwa sababu ya utegemezi mkubwa wa dawa hizo katika ufugaji wa wanyama.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2020 imebaini kuwa mbinu za kisasa za kilimo na ufugaji zinazofanana na mifumo ya viwandani, zina mchango mkubwa kwenye kusambaza magonjwa ya kuambukiza kati ya wanyama na binadamu kama vile homa ya nguruwe, homa ya mafua ya ndege na virusi vya Nipah.

Dokta Victor Yamo, meneja wa kampeni za kilimo katika shirika la World Animal Protection linalolinda maslahi ya wanyama anasema kwa mantiki hii ipo haja ya kutathmini upya mifumo ya kisasa ya kilimo na ufugaji wa wanyama. Utafiti wa mifumo ya kilimo na kufuga wanyama wa chakula umebaini kuwa vijidudu na bakteria vinaendelea kuwa sugu na dawa zinashindwa kuviua.

Hayo yamekuwa dhahiri Brazil, Uhispania, Thailand, Marekani na barani Afrika. Vijidudu hivyo ambavyo havisikii dawa vinawatatiza matabibu wanapowahudumia wagonjwa wanaohitaji dawa za kuua bakteria. Hilo linaweza kuchangia na kusababisha janga la kiafya kote ulimwenguni. Utafiti uliofanyika Wuhan umebaini kuwa kilichochangia kutokea kwa karibu nusu ya vifo vyote vilivyotokana na COVID-19 ni maambukizi ya pili ya bakteria na wagonjwa walipewa dawa kuyaziua.

Kwa upande wake Shirika la Afya Uliwenguni, WHO linatahadharisha kuwa huenda ukafika wakati baadhi ya vijidudu vikawa sugu kwa dawa zote kwa sababu ya matumizi ya kupindukia. Hivyo itakuwa vigumu kwa magonjwa ya kawaida kutibiwa.

Profesa Sam Kariuki ni mkurugenzi wa kitengo cha Utafiti na Maendeleo kwenye taasisi ya utafiti wa tiba Kenya, KEMRI ambaye amehusika na utafiti wa bakteria kwa muda mrefu anasema wakulima na wafugaji wa wanyama wa chakula wanakumbana na changamoto nyingi kutokana na hilo.

WHO kupima dawa za mitishamba Afrika

Shirika la Afya Duniani (WHO) limekubali kanuni za kupima dawa za mitishamba za Afrika kwa ajili ya mapambano dhidi ya Covid-19.

Sayansi itakuwa ndio msingi wa vipimo hivyo kwa ajili ya usalama na ufanisi wa dawa ambazo zitaidhinishwa, imesema WHO katika taarifa iliyotolewa mwezi Septemba.

Madawa yoyote ya kienyeji ambayo yanaaminika kuwa yana ufanisi yanaweza kuharakishwa kutengenezwa kwa kiwango kikubwa.

Rais wa Madagascar amekuwa akinadi dawa ya asili ambayo haijafanyiwa vipimo ambayo anasema inaweza kutibu virusi vya corona, licha ya onyo la WHO dhidi ya matumizi ya dawa hizo za mitishamba.

WHO ilisema kuwa kanuni mpya zinalenga kusaidia na kuwawezesha wanasayansi wa Afrika kufanya majaribio yanayofaa ya kimatibabu.

Sambamba na juhudi hizi, kliniki za majaribio ya awamu ya tatu zimepewa ruhusa ya kuendelea kutumia dawa za kiasili za Afrika.

Rais wa Madagascar Andrey Rajoelina akizundua dawa ya mitishamba ya kutibu corona

Jopo la wataalamu, linalojumuisha WHO, Kituo ch kudhibiti na kuzuia magonjwa cha Muungano wa Afrika na tume ya Muungano wa Afrika ya masuala ya kijamii, wamekubaliana juu ya mpangilio wa shughuli hiyo.

Awamu ya tatu ya majaribio kwa kawaida hupima usalama na ufanisi wa dawa kwa kundi kubwa la watu wanaoshiriki.

"Kuidhinishwa kwa nyaraka za kiufundi kutahakikisha kwamba ushahidi wa pamoja wa kimatibabu wa ufanisi wa dawa hizo asili kwa ajili ya tiba ya Covid-19 unapatikana bila kukiuka usalama wake," amesema Profesa Motlalepula Gilbert Matsabisa, mwenyekiti wa jopo hilo la wataalamu.

 

Tags