Oct 19, 2020 09:36 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Oktoba 19

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Fainali ya AFC 2020 kufanyika Doha, Qatar

Ni rasmi sasa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia (AFC Champions League) mwaka huu 2020 itapigwa Disemba 19 katika mji mkuu wa Qatar, Doha. Hayo yamethibitishwa Ijumaa hii na Shirikisho la Soka Asia (AFC) pamoja na Shirikisho la Soka la Qatar (QFA). Mashabiki wa soka hapa Iran walitazamia kuwa mchuano huo wa fainali ungelipigwa hapa nchini kwa kutilia maanani kuwa, moja ya klabu zilizotinga fainali ni Persepolis ya Tehran. Katibu Mkuu wa AFC, Dato’ Windsor John amesema: Janga la Covid-19 bila shaka limefanya uamuzi wa kuamua pahala pa kuchezewa fainali uwe mgumu sana mwaka huu kutokana na vikwazo na vingiti vya kusafiri na nyakati zisizotabirika.

Klabu ya Persepolis iliyovaa jezi jekundu

 

Klabu hiyo ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitinga fainali ya ligi ya kieneo kwa kuigaragaza klabu ya al-Nassr ya Saudi Arabia mabao 5-3. Katika mchuano wa nusufainali wa Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia (AFC Champions League) uliopigwa katika Uwanja wa Jasim Bin Hamad nchini Qatar, timu mbili hizo zilikabana koo, ambapo dakika 90 za ada na 30 za nyongeza hazikutosha kumtoa mshindi. Timu hizo mbili zililazimika kuingia katika mikwaju ya penati baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Persepolis ambayo italiwakilisha eneo la magharibi mwa Asia, itakutana katika fainali na mshindi wa timu ya mashariki mwa bara hili. Robofainali ya eneo la mashariki mwa Asia ya Ligi ya Klabu Bingwa Barani Asia itasakatwa Disemba 10, kabla ya nusufainali Disemba 13.

Corona yavuruga mechi za Iran

Kwengineko, mchuano wa kirafiki baina ya timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mali umeakshirishwa. Mechi hiyo ilitazamiwa kupigwa mjini Antalya nchini Uturuki Oktoba 13, lakini imeakhirishwa kutokana na janga la corona. Hii ni baada ya wachezaji kadhaa wa timu hiyo ya magharibi mwa Afrika kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19. Iran ilishuka dimbani kuvaana na Uzbekistan siku ya Jumanne ya Oktoba 8 mjini Tashkent na kupata ushindi mnono wa mabao 2-1.

Kocha Dragan Skocic wa Timu ya Taifa ya Iran

 

Machui wa Persian wanatazamiwa kuchuana na Senegal mwezi ujao wa Novemba, kabla ya kutoana udhia na Bosnia au Panama katika mchuano mwingine wa kirafiki. Mkufunzi wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dragan Skocic anaandaa kikosi cha kukichezesha katika mechi za kufunzu Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar. Mechi za kufunzu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar ziliztazamiwa kuchezwa mwaka huu lakini zikaakhirishwa hadi mwakani kutokana na janga la corona. 

Soka; Tanzania tayari kwa CHAN

Timu ya Taifa Tanzania 'Taifa Stars' itaanza kutupa karata yake ya kwanza katika fainali za wachezaji wanaocheza soka ya ndani (CHAN) Januari 19, 2021 dhidi ya Zambia mchezo utakaopigwa katika mji wa Buea, Cameroon. Fainali hizo zinaanza rasmi mwakani, huku Tanzania wakiwa wamefuzu baada ya kuifunga Sudan 1-0. Stars watakuwa na kibarua kingine dhidi ya Namibia, Januari 23 mchezo utakaopigwa katika mji wa Buea huku mchezo wa mwisho ukipigwa dhidi ya Guinea katika mji wa Douala. Tanzania inasisitiza kuwa imejiandaa vya kutosha kwa ajili ya michuano hiyo ya kikanda.

Fainali za kombe hilo zenye makundi manne zinatarajia kumalizika Februari 7 mchezo utakaopigwa katika jiji la Younde kwenye mji wa Ahmadou Ahidjo, Cameroon. Timu zilizofuzu ni Cameroon, Zimbabwe, Mali, Burkina Faso, Libya, Niger, Dr Congo, Congo, Morocco, Togo, Rwanda, Uganda, Zambia, Tanzania, Guinea na Namibia.

Riadha; Pufya Kenya

Mwanariadha nyota wa Kenya, Peres Jepchirchir wa Kenya siku ya Jumamosi aliweka rekodi mpya baada ya kushinda mbio za nusu marathon za wanawake nchini Poland. Jepchirchir mwenye umri wa miaka 27 alikata utepe wa ushindi katika mbio hizo za kimataifa kwa kutumia saa moja, dakika tano na sekunde 16. Mwanariadha huyo wa kike wa Kenya amevunja rekodi yake mweyewe kwa sekunde 18. Jepchirchir aliwaonyesha kivumbi wanariadha bingwa Melat Yisak Kejeta wa Uingereza aliyemaliza katika nafasi ya pili, akifuatiwa na Muethiopia, Yalemzerf Yehualaw.

Mashindano haya ya mabingwa wa riadha wa kike yalitamiwa kufanyika Machi mwaka huu lakini yakaakhirishwa hadi mwezi huu wa Oktoba kutokana na janga la corona. Wakati huohuo, Mkenya Daniel Wanjiru, ambaye ni mshindi wa mbio za Marathon za London mwaka 2017, amepigwa marufuku kwa miaka minne kutokana na ukiukaji kanuni za hati maalum za kibayolojia za riadha. Mshindi wa zamani wa mbio za London marathon Daniel Wanjiru amefungiwa kushiriki mbio hizo kwa kipindi cha miaka minne. Kulingana na kitengo huru cha uadilifu wa mchezo wa riadha (AIU), mwanariadha huyo wa Kenya mshindi wa mbio za London marathon mnamo mwaka 2017 amefungiwa kwa kipindi hicho cha miaka minne kutokana na ukiukwaji wa hati ya kibaiologia ya kusafiria. Wanjiru ambaye amekanusha kutenda kosa lolote, alisimamishwa kwa muda kujihusisha na masuala ya riadha mnamo mwezi April. Marufuku yake iliungwa mkono Desemba 9 mwaka 2019 na matokeo yote ya miaka 28 tangu Machi 9 mwaka uliopita yamefutwa, AIU ilisema katika taarifa yake. Ana siku 30 za kukata rufaa juu ya hukumu hiyo kwenye mahakama ya usuluhishi ya michezo. ABP hutumiwa kufuatilia vigezo vya kibaiologia kwa muda ambao huweka wazi madhara ya madawa ya kulevya badala ya kujaribu kuchunguza kemikali au mbinu yenyewe.

Dondoo za Hapa na Pale

Mchezaji nyota wa klabu ya Manchester United Juan Mata anaripotiwa kukataa ofa kubwa ya pauni milioni 18 kuhamia katika klabu moja ya Saudi Arabia. Hii ni licha ya mchezaji huyo kwa miaka kadhaa sasa amekuwa akipigwa benchi na hajashirikishwa katika mechi ya Man United. Hata hivyo, alishirikishwa katika mechi mbili ya United ikiwemo Kombe la Carabao ambapo alichangia pakubwa katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Brighton na kufuzu kwa robo fainali ya mashindano hayo. Na katika kujaribu kumnasua kwenye masaibu yanayomkumba ugani Old Trafford, MailSport inaripoti kuwa Muhispania huyo alikabidhiwa ofa ya pauni milioni 11.5 kuhamia katika timu ya Saudia. Kulingana na gazeti hilo likinukuu shirika la Uhispania la AS, ofa hiyo iliongezwa hadi pauni milioni 18 lakini Mata alikataa kuhama. Inaaminika kuwa mkali huyo wa zamani wa Chelsea hana hamu ya kuhama na ana matumaini kuwa huenda United itashinda taji msimu huu. Hii ni licha ya Manchester United kuendelea kujikokota tangu kuanza kwa kampeni mpya na kusajili ushindi mmoja pekee dhidi ya The Seagulls. Wanamichezo mbalimbali wamekuwa wakikataa ofa za kwenda kuchezea klabu au timu za michezo za Saudia, kutokana na faili jeusi la ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na watala wa Riyadh.

Ronaldo aliyekumbwa na corona

 

Na wachezaji wote wa klabu ya Juventus wamejiweka karantini kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona. Wachezaji hao wamelazimika kujitenga kwa ridhaa yao baada ya kiungo wa timu hiyo Weston McKennie kuthibitika kuwa na ugonjwa wa Covid-19. McKennie ambaye amejiunga na Juventus katika dirisha hili la usajili akitokea Schalke ya Ujerumani, ndio mchezaji pekee wa Juventus kuthibitika kuwa na maambukizi hayo kati ya wachezaji wote hivyo wanajitenga kwa tahadhari. Taarifa hizo zinakuja ikiwa ni saa 24 zimepita toka Cristiano Ronaldo wa Juventus athibitike pia kuwa na maambukizi ya Corona akiwa kwao Ureno na sasa amejitenga.

……………………….TAMATI………….……

Tags