Oct 23, 2020 03:03 UTC
  • Ijumaa tarehe 23 Oktoba 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 6 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 23 Oktoba mwaka 2020.

Miaka 838 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulavi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Balkh ambao ni moja kati ya miji ya Iran ya wakati huo. Molavi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya muda Maolavi alihamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maanavi, Fihi Ma Fihi, Maktubat Maulana na Rabaiyyat. Malenga huyo mkubwa wa Kiirani alifariki dunia mwaka 672 Hijria Shamsia.

Maulawi

Miaka 148 iliyopita, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa. Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.

Theophile Gautier

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita sawa na tarehe Pili mwezi Aban mwaka 1307 Hijria Shamsia, Ayatullah Dakta Sayyid Muhammad Husseini Beheshti mwanafikra na mwanamapinduzi wa Iran alizaliwa huko Isfahan, moja kati ya miji ya katikati mwa Iran. Ayatullah Beheshti alilelewa katika familia ya kidini na alianza kujifunza masomo ya kidini akiwa kijana mdogo. Akiwa na umri wa miaka 18, alielekea katika mji wa kidini wa Qum nchini Iran na kusoma kwa maulamaa wakubwa wa mji huo akiwemo Imam Khomeini (RA). Wakati huo huo, Dakta Beheshti alitumia kipawa chake kikubwa na kuamua kuendelea pia na masomo ya Chuo Kikuu na kufanikiwa kupata shahada ya udaktari katika falsafa. Dakta Beheshti aliuawa shahidi akiwa na viongozi na shakhsiya wengine 72 wa Iran katika mkutano mwezi Tiir mwaka 1360 Hijria Shamsia baada kundi la kigaidi la Munafiqin kuripua bomu katika mkutano huo.

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani. Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika. Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Vita vya kihistoria vya al-Alamein 

 

Tags

Maoni