Oct 26, 2020 08:24 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 26

Ufuatao ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita kitaifa na kimataifa....

Iran yampa mkono wa kheri Pele

Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limemnyooshea mkono wa kheri, fanaka na baraka tele aliyekuwa mchezaji nguli wa soka wa Brazil, Edson Arantes do Nascimento maarufu kama "Pele" wakati huu anapoadhimisha sikuzawa yake. Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Brazil, Mehdi Mohammad Nabi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amempongeza Pele katika maadhimisho ya miaka 80 tangu kuzaliwa kwake. Barua hiyo imeashiria safari za Pele hapa nchini Iran miaka ya huko nyuma, na kukutana timu za mataifa haya mawili katika mechi mbalimbali, na vile vile jitihada za pande mbili za kuimarisha ushirikiano wa kisoka wa Iran na Brazil. Pele ambaye alizaliwa Oktoba 23 mwaka 1940, alikuwa mmoja wa wanamichezo mashuhuri na waliofanikiwa zaidi katika karne ya 20. Katika enzi zake, mwanasoka huyo nyota alikuwa mmoja wa wanamichezo wanaolipwa donge nono zaidi duniani. Mbali na kuwa bingwa wa kucheka na nyavu, mashambuliaji huyo mahiri wa zamani wa Brazil anatambulika katika madaftari ya historia kama mchezaji pekee aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu (1958, 1962, and 1970).

Licha ya magonjwa ya hapa na pale yanayomnyemelea mfalme huyo wa mpira wa miguu kutokana na umri wake mkubwa, lakini angali mcheshi na mwingi wa bashasha na hilo lilidhihirika wazi siku chache zilizopita katika siku yake ya kuzaliwa, aliposema kwa utani kumwabia Rais wa Shirikisho la Soka la Brazil: Mie nipo ngangari, siwezi tu kucheza lakini sina neno. Pele ambaye anasihi viungani mwa mji wa Sao Paulo, ameweka rekodi ya kuifunga timu ya taifa ya Brazil mabao mengi zaidi, ambapo alifanikiwa kuchek ana nyavu mara 77, rekodi ambayo Neymar Jnr anaikaribia kwa kufunga mabao 64.

Corona yavuruga tena soka Iran

Kwa mara nyingine tena, Idara ya Afya ya Shirikisho la Soka la Iran imesimamisha michuano ya Ligi Kuu ya Soka ya Iran kutokana na wimbi jipya la virusi vya corona. Mohammad Asad Masjedi, Kaimu Rais wa kitengo hicho cha tiba cha Shirikisho la Soka la Iran amesema ligi hiyo ambayo inafahamika hapa nchini kama Ligi ya Wataalamu (IPL) imeakhirishwa kutokana na msambao wa ugonjwa wa Covid-19. Kadhalika Shirika la Kuratibu Ligi za Iran limetangaza kuwa mechi za ligi kuu ya IPL humu nchini zimesimamishwa kwa sasa kutokana na kasi ya msambao wa corona, na kwamba zitarejelewa Novemba 6 iwapo hali itakuwa imeboreka. Huku hayo yakiarifiwa, Rais wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Iran, Reza Salehi Amiri ameambukizwa maradhi ya Covid-19. Katibu Mkuu wa kamati hiyo, Keykavous Saeidi amesema Amiri yuko katika hali nzuri, lakini atasalia kwenye karantini kwa muda wa siku 14. Jumatatu ya wiki iliyopita, watu 337 waliaga dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Iran, kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa hapa nchini tangu maradhi hayo yaripotiwe hapa nchini mapema mwaka huu.

Michezo Afrika

Klabu ya Reneissance Berkane ya Morocco imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika la CAF, baada ya kuibamiza Pyramids ya Misri bao moja bila jibu katika fainali iliyopigwa Jumapili katika Uwanja wa Mwanamfalme Abdullah jijini Rabat. Berkane ilitumia vizuri msemo wa mcheza kwao hutuzwa, na kuhakikisha kuwa wanaibuka washindi na kutwaa taji hilo la kieneo. Bao hilo la ushindi la kipekee katika mchuano huo lilitiwa kimyani na Issouffou Dayo kunako dakika ya 15 ya mchezo.

Pyramids walishindwa kucheka na nyavu za wenyeji, licha ya kutawala mchezo na kumiliki mpira kwa asilimia 61. Mchezo huo ulishuhudia kiungo Bakr al-Hilali wa Berkane akilishwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi. Kabla ya hapo, klabu hiyo ililishwa kadi 3 za njano, na wenzao wa Pyramids 4. Pyramids ya Misri ambayo inaonekana kama timu kinda katika soka barani Afrika ilifanikiwa kutinga fainali baada ya kuibwaga Horoya ya Guinea kwa mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF. Nusu fainali nyingine mkondo wa pili ilizikutanisha al-Ahly ya Misri na Wydad Casablanca ya Morocco, ambapo mafao walipa ushindi wa mabao 3-1.

Nembo ya Shirikisho la Soka Afrika

 

Kwengineko, Wizara ya Afya nchini Morocco imeitaka klabu ya Raja Casablanca kujiweka karantini kutokana na wachezaji wake 9 kukutwa na Corona baada ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya Zamalek ya Misri. Kwenye mchezo huo Raja Casablanca walipoteza kwa goli 1-0 na walitakiwa kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Zamalek Jumamosi hii nchini Misri. Hata hivyo CAF wametangaza kuwa mchezo wa marudiano uliyokuwa uchezwe wikendi hii umeakhirishwa kutokana na Raja Casablanca kutakiwa kuingia karantini.

Mikakati ya Kocha mpya wa Harambee Stars ya Kenya

Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) Nick Mwendwa amemtangaza Jacob 'Ghost' Mulee kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars kwa mkataba wa miaka mitatu. Maamuzi hayo yanakuja ikiwa ni siku moja toka FKF itangaze kuachana na aliyekuwa mkufunzi wao mkuu Francis Kimanzi na benchi lote la ufundi. Kocha huyo mpya wa Harambee Stars, tayariametaja kikosi cha wanasoka atakaowategemea katika mechi mbili zijazo dhidi ya Comoros katika vita vya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021. Stars wameratibiwa kuwa wenyeji wa Comoros mnamo Novemba 11 jijini Nairobi kabla ya kurudiana na Wanavisiwa hao mjini Moron siku nne baadaye.  

Wachezaji wa Harambee Stars wakishangilia bao

 

Wachezaji wanaosakata soka katika klabu mbalimbali za ligi ya humu nchini humo wanatarajiwa kuripoti kambini mnamo Oktoba 28 huku wale wanaotandaza kabumbu ya kulipwa ughaibuni wakitazamiwa kuingia kambini kufikia Novemba 2. Ni wachezaji 20 pekee ambao watajumuishwa kwenye orodha ya mwisho ya masogora watakaotegemewa na Mulee dhidi ya Comoros. Chini ya Kimanzi, Stars walianza kampeni zao za Kundi G kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14 mwaka jana 2019 ugenini, kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18 jijini Nairobi.

Dondoo za Hapa na Pale

Lewis Hamilton ameweka historia kwa kuibuka mshindi bora wa muda wote wa mashindano ya mbio za magari ya Langalanga (Formula One). Hii ni baada ya kusajili ushindi wa 92 katika mashindano ya Grand Prix ya Ureno Jumapili ya Oktoba 25 na kumpiku nguli Michael Schumacher. Kwa kuzitawala mbio hizo, Hamilton aliivunja rekodi ya miaka 14 ya Schumacher. Hamilton (35) alijitahidi maradufu baada ya kuonekana kulemewa awali alipotupwa hadi nafasi ya tatu gari lake lilipopata tatizo la gurudumu kutokana na mvua. Ushindi alioupata nchini Ureno mnamo Oktoba 24 ulikuwa wake wa nane katika jumla ya mashindano 12 ambayo ameyashiriki mwaka huu. Hamilton ambaye ni bingwa mara sita wa dunia, alikamilisha mbio hizo kwa sekunde 25.5 mbele ya mwenzake wa Team Mercedes, Valtteri Bottas. Max Verstappen wa Red Max aliridhika na nafasi ya 3. Hamilton kwa sasa anajivunia rekodi ya kuibuka wa kwanza mara 97.

Khabib, Mwandondi nyota wa Russia aliyetangaza kustaafu masumbwi

 

Huku hayo yakiarifiwa, mwanamasumbwi nyota wa kimataifa raia wa Russia, Khabib Abdulmanapovich Nur-magomedov ametangaza kustaafu ndondi. Khabib (32) ametangaza hayo baada ya pambano lake la mwisho dhidi ya Justin Gaethje katika taji la UFC 254, ambapo alimsagasaga hasimu wake huyo kwa alama 29-0. Khabib "The Eagle" ambaye ameshinda mataji 13 ya UFC amesema aliingia katika taaluma ya ngumi miaka 20 iliyopita kutokana na ushawishi wa babake mzazi, na sasa anastaafu kwa kuwa alimuahidi mamake mzazi kuwa pambano lilipoita la UFC litakuwa lake la mwisho.

Mbali na hayo, ripoti kutoka jijini London zinaarifu kuwa kiungo mshabuliaji wa Arsenal, Mesut Ozil, ameondolewa kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha timu hiyo kinachoshiriki  Ligi Kuu ya Uingereza. Orodha rasmi imewasilishwa FA ikimaanisha kuwa Ozil hataweza kuichezea timu hiyo kwenye mechi za ligi hiyo mpaka mwezi Februari 2021.  Pia, hivi karibuni alitemwa kwenye kikosi kitachoshiriki michuano ya Europa. Ozil ndiye mchezaji anayelipwa mshara mkubwa zaidi ndani ya The Gunners na kocha Mikael Arteta ameonyesha kutomhitaji fundi huyo wa Kijerumani ambaye mkataba wake unamfikia tamati mwakani. Ozil, 32, alijiunga na Arsenal mnamo 2013 kwa kima cha Sh5.9 bilioni kutoka Real Madrid ya Uhispania. Nyota huyo aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia Ujerumani ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2014 nchini Brazil, hajawahi kuwajibishwa na Arsenal kwenye mechi yoyote tangu Machi 7, 2020. Mzawa huyo wa Uturuki na raia wa Ujerumani tangu ajiunge na Emirates, ameifungia Gunners mabao 44 kutokana na mechi 254 katika mapambano yote.

Ozil

 

Na kwa kutamatisha, nguli wa soka, Cristiano Ronaldo amepimwa tena na kukutwa na ugonjwa wa corona wakati Juventus ikijiandaa kwa pambano la Ligi ya Mabingwa Ulaya wiki ijayo dhidi ya Barcelona, kwa mujibu wa ripoti kutoka Italia, kwa sasa Ronaldo amejitenga nyumbani kwake Torino baada ya kupimwa na Covid-19 mnamo Oktoba 13 wakati akiwa na timu ya taifa ya Ureno kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mataifa. Jumatano iliyopita, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alipimwa tena na kugunduliwa kuwa bado ana virusi hivyo. Fowadi huyo wa Ureno anaweza kuwa tayari kwa ajili ya mchezo dhidi ya Barcelona mnamo Oktoba 28. Chini ya sheria za UEFA Ronaldo atahitaji kuwa na vipimo hasi saa 24 kabla ya mchezo wa Barcelona huko Torino.

..................................TAMATI........................

 

 

Tags