Oct 28, 2020 14:38 UTC
  • Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020

Leo ni Jumatano tarehe 11 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na Oktoba 28 mwaka 2020.

Siku kama ya miaka 149 iliyopita, alizaliwa mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allama Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia. 

Allama Agha Bozorge Tehrani (katikati)

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatullah Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa. Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza. Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo katika jaribio hilo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah.

Ayatullah Sayyid Hassan Modarres

Katika siku kama ya leo miaka 88 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sayyid Hassan Sadr mmoja wa maulama mahiri wa Kiislamu. Alikuwa mmoja wa mafakihi ambao walipata daraja ya Ij’tihad katika kipindi cha ujana. Sayyid Hassan Sadr alikuwa katika orodha ya walimu mashuhuri katika Chuo KIkuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Aliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sadruddin katika elimu ya fikihi, Usul, Itikadi, falsafa na hadithi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Sayyid Hassan Sadr ni Tahsil al-Furu’u al-Diniyyah fi Fikih al-Imamkiyah na Taasis al-Shiyah.

Sayyid Hassan Sadr

Tarehe 28 Oktoba miaka 72 iliyopita wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakisali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho. Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote.

Tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 yaani siku kama hii ya leo miaka 58 iliyopita, ulihitimishwa mgogoro wa makombora wa Cuba baada ya kiongozi wa wakati huo wa Urusi, Nikita Khrushchev kuamuru kurejeshwa nyumbani meli zilizokuwa na makombora ya nyuklia. Hatua ya Urusi ya kujenga vituo kadhaa vya makombora ya nyuklia nchini Cuba katika umbali wa kilomita 90 kutoka Marekani ilizusha mgogoro mkubwa wa makombora uliokaribia kuitumbukiza dunia katika vita vya nyuklia. Wakati huo Marekani na Russia zilitishia kushambuliana kwa makombora ya nyuklia na kuzusha hofu kubwa hususan kwa watu wa Marekani, Russia na nchi za Ulaya. Hatimaye tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 Nikita Khrushchev alitoa amri ya kurejea nchini meli zote zilizokuwa na makombora ya nyuklia na kufungwa vituo vya makombora vya Urusi nchini Cuba.  

Nikita Khrushchev

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Taha Hussein mwandishi mahiri na stadi wa Kimisri. Alizaliwa mwaka 1889 katika moja ya vijiji vya Misri. Taha Hussein ambaye alikuwa mtoto wa saba katika familia yake, alipofuka na kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka mitatu. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimjaalia kipaji cha hali ya juu. Taha Hussein alifanikiwa kuihafidhi Qur’ani yote katika kipindi kifupi. Akiwa na umri wa miaka 14 alifanikiwa kufaulu mtihani wa watahaniwa wa kuingia Chuo Kikuu cha al-Azhar na akiwa pamoja na kaka yake alijishughulisha na kusoma masomo ya dini pamoja na lugha ya kigeni. Mwaka 1914 Taha Hussein alihitimu kwa alama nzuri na kutunukiwa shahada ya uzamivu yaani PhD. Wakati huo Chuo Kikuu cha Taifa cha Misri kilichukua uamuzi wa kuipeleka timu ya wahadhiri nchini Ufaransa kwa ajili ya kwenda kufundisha historia ya Mashariki. Akiwa ahuko alifunza lugha ya Kifaransa pamoja na histotia ya Ugiriki na Roma ya Kale pamoja na lugha ya Kigiriki. Mwaka 1959 mwandishi huyo mahiri wa Kimsri alinutukiwa tuzo ya Nobel kutokana na mchango wake katika uga wa fasihi ya lugha. Taha Husserin ameandika vitabu vingi katika taaluma za fasihi, sayansi ya siasa na historia.

Taha Hussein

 

Tags