Nov 01, 2020 02:30 UTC
  • Jumapili, Mosi Novemba, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 15 Mfunguo Sita Rabiul-Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Novemba, 2020 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, Muhammad Ghazvini, mwanafasihi, mhakiki na mwanahistoria wa Kiirani alizaliwa mjini Tehran. Alifanikiwa kuwa na ufahamu wa misingi ya fasihi na teolojia akiwa katika rika la ubarobaro na kuinukia. Akitumia kipaji chake alistafidi na elimu ya baba yake. Kipindi fulani Muhammad Ghazvini alielekea barani Ulaya na kufanikiwa kupata kopi ya vitabu vya hati ya Kifarsi katika majumba ya makumbusho barani humo. Msomi huyu hakuwa nyuma pia katika fani ya uandishi wa vitabu. Hatimaye Muhammad Ghazvini aliaga dunia mwaka 1360 Hijria na amezikwa katika mji wa Rey uliopo kusini mwa Tehran. ***

Muhammad Ghazvini,

 

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo, ufalme wa Austria na Hungary uligawanyika baada ya kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Ufalme huo ambao uliundwa katika nusu ya pili ya karne ya 19 iladia, kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia ulikuwa umepelekea kutokea ufalme mkubwa na wenye nguvu barani Ulaya na ambao ulipanuka sana. Hata hivyo, baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia, madola yaliyoibuka na ushindi katika vita hivyo, yaliugawa ufalme huo katika nchi tatu za Austria, Hungary na Czechoslovakia kama gharama ya kushindwa katika vita hivyo. ***

Austria

 

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Kemal Ataturk. Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wa utawala wa Othmania, Atatürk aliamua kuvunja utawala huo wa kifalme na kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa na misingi ya kidini. Hivyo mwanzoni alitenganisha baina ya utawala wa kisultani na cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikibakia kama cheo cha heshima tu. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600. Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri na wa kisekulari hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923. ***

Kemal Atarturk

 

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella. Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ulipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi. ***

Ahmed ben Bella

 

N miaka 57 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Aban 1342 Hijria Shamsia Tayib Haj-Rezaei mmoja wa wapinzani mashuhuri wa utawala wa kidhalimu wa Kipahlavi hapa Iran alinyongwa. Alizaliwa mwaka 1280 Hijria Shamsia katika mji wa Tehran na kwa kipindi fulani alikuwa akihesabiwa kuwa mfuasi wa utawala wa kifalme wa Kipahlavi. Hata hivyo imani ya Tayib Haj-Rezaei kwa Uislamu hususan mapenzi yake makubwa kwa Imam Hussein AS ni mambo yaliyomfanya ajitenge na utawala huo wa Kifalme wa Shah na kujiunga na harakati ya mapinduzi ya Imam Ruhullah Khomeini (MA). Hatimaye baada ya mateso mengi, alivyongwa katika siku kama ya leo. ***

Tayib Haj-Rezaei

 

Tags