Nov 16, 2020 08:27 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Nov 16

Hujambo mpenzi mwanaspoti wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.

Soka: Iran yaizaba Bosnia katika mchuano wa kirafiki

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeichabanga Bosnia Herzegovina mabao 2-0 katika mchuano wa kirafiki uliopigwa Alkhamisi katika Uwanja wa Asim Ferhatović-Hase mjini Sarajevo nchini Bosnia. Machui hao wa Uajemi waliutandaza mpira barabara licha ya kuchezea ugenini. Kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu hizo kuona lango la hasimu. Hata hivyo katika kipindi cha pili, Iran iliongeza kasi na sekunde chache baada ya kupulizwa kipengya cha kuanza ngoma, Kaveh Rezaei alitikisa nyavu za wenyeji.

Kikosi cha Iran kilichovaana na Wabosnia

 

Mtoka benchi, Mehdi Ghaedi alifanya mambo kuwa 2-0 kupitia goli la kiufundi la dakika za majeruhi. Kabla ya hapo, Iran ilishuka dimbani kuvaana na Uzbekistan Jumanne ya Oktoba 8 mjini Tashkent na kupata ushindi mnono wa mabao 2-1. Mkufunzi Mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dragan Skocic anaandaa kikosi cha kukichezesha katika mechi za kufunzu Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar. Mechi za kufunzu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar ziliztazamiwa kuchezwa mwaka huu lakini zikaakhirishwa hadi mwakani kutokana na janga la corona. 

Taekwondo: Wairani wazoa medali 17

Wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamezoa jumla ya medali 17 katika Duru ya Kwanza ya Mashindano ya Mabingwa wa Taekwondo Mtindo wa Poomsae ya Asia mwaka huu 2020. Wanataekwondo hao wa Iran walitia kibindoni medali moja ya dhahabu, fedha tano na shaba 11 katika mashindano hayo ya kibara yaliyoanza baina ya Novemba 12 na 14. Mashindano hayo yalifanyika kwa njia ya intaneti. Mwanadada wa Kiirani Sakineh Maher ndiye aliyelipa fahari taifa hili kwa kunyakua medali ya dhahabu.

Mwanataekwondo wa kike wa Iran

 

Binti mwingine Muirani, Narjes Sharifi ametawazwa katika nafasi ya tatu ya mashindano hayo yanayofahamika kwa Kiingereza kama Asia Taekwondo Poomsae Championships. Kwa mujibu wa Shirikisho la Taekwondo Asia, mashindano hayo hayakuorodhesha matokeo ya timu, lakini yaliwapiga darubini tu wachezaji binafsi. Hata hivyo kwa mujibu wa wingi wa medali, mwenyeji Korea Kusini imeibuka ya kwanza, huku timu 2 za Iran zikitwaa nafasi ya pili na tatu, na Ufilipino ikafunga orodha ya nne bora.

Mbio za AFCON: Kenya na Tanzania wabanwa ugenini

Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars ilibanwa mbavu na kikosi cha Tunisia kwenye mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon mwaka 2022 nchini Cameroon. Bao la pekee na la ushindi kwa Tunisia kwenye mchezo huo wa kundi J uliochezwa Ijumaa ya Novemba 13 lilifungwa na Youssef Msakni dakika ya 18 kupitia mkwaju wa penalti. Jitihada za Stras kusawazisha ziliambulia patupu kwa kubanwa mbavu mpaka dakika 90 zinamalizika. Mchezo wa marudio baina ya timu mbili hizo unatarajiwa kuchezwa Novemba 17, katika Uwanja wa Mkapa nchini Tanzania. Mashabiki wa Taifa Stars wanasisitiza kuwa, kuvunjika kwa mwiko si mwisho wa kusonga sima.

Siku ya Jumapili, timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars nayo ilijizoa zoa dimbani kuvaana na vijana wa Kingazija. Katika mchuano huo, Kenya ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutokana kwa Wacomoro na hivyo matumaini ya kutia mguu katika michuano ya Afcon yakizidi kufifia. Comoro ilikuwa ya kwanza kucheka na nyavu kupitia goli la El Fardou Ben Nabouhane katika dakika ya 21 ya mchezo, lakini Cliff Nyakeya akafanya mambo kuwa sawa bina sawa dakika 14 baadaye. Baada ya wenyeji kufunga la pili, waliamua kuweka uzio usiovukika katika safau ya nyuma hadi kipenga cha mwisho kinalia. Harambee Stars ambao walitoa sare ya kufungana bao 1-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Nairobi wiki iliyopita, sasa wana kibarua kigumu cha kutakiwa kuzifunga Togo na Misri katika karata zao za mwisho za kutinga Afcon, mwezi Machi mwaka huu.

 

Huku hayo yakiarifiwa, mshambuliaji Halid Lwaliwa alitoka benchi na kufunga bao lake la kwanza la kimataifa kwenye uwanja wa nyumbani wa klabu yake, wakati Uganda ilipopambana na Sudan Kusini kwenye mechi iliyochezwa Jumatano jioni. Wageni kwa ujumla walilingana nguvu na wenyeji, lakini hawakuwa na bahati na kulazimika kukubaki kichapo hicho. Lakini Lwaliwa, mmoja kati ya wachezaji wawili wenyeji, na mwingine akiwa mbadala wa kipindi cha pili Karim Wantambala, walihakikisha Uganda inadumisha ushindi huo. Uganda inaonekana kuwa timu iliyofanya vizuri kati ya timu za Afrika Mashariki, baada ya Kenya kubanwa mbavu na Comoro, na Tanzania kuelemewa na Waarabu wa Tunisia. Sierra Leone nao walitoka nyuma kwa mabao manne bila jibu na kulazimisha Super Eagles ya Nigeria sare ya 4-4 katika mechi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Novemba13 jijini Benin City, jimbo la Edo, Nigeria. Katika michuano mingine ya Novemba 13, sajili mpya wa Chelsea, Hakim Ziyech alifungia Morocco mabao mawili na kuhakisha kwamba wanasajili ushindi wa nyumbani sawa na Mali, Niger na Afrika Kusini. Licha ya sare hiyo ya 4-4, Nigeria wanasalia kileleni mwa kundi lao kwa alama saba, alama mbili zaidi ya Sierra Leone wanaoshikilia nafasi ya tatu. Mabao mawili kutoka kwa Ziyech yalisaidia Morocco kuipepeta Jamhuri ya Afrika ya Kati mabao 4-1 na kupaa hadi kileleni mwa Kundi E. Magoli mengine ya Morocco yalifumwa wavuni na Achraf Hakimi na Zakaria Aboukhlal aliyekuwa wakiwajibishwa katika timu ya taifa kwa mara ya kwanza. CAR walifutiwa machozi Louis Mafouta. Morocco kwa sasa wanaselelea kileleni mwa kundi lao kwa alama saba, mbili zaidi kuliko Mauritania ambao ni wa pili. Afrika Kusini walihitaji penalti ili kusajili ushindi wa 2-0 uliowaepushia aibu ya kuangushwa na Sao Tome Principe, taifa dogo lililo na raia 200,000 pekee ambalo linashikilia nafasi ya 182 kwenye orodha ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Percy Tau aliwafungulia Afrika Kusini ukurasa wa mabao kunako dakika ya 55 kabla ya Bongani Zungu kuongeza la pili jijini Durban. Afrika Kusini kwa sasa ni ya pili kwenye Kundi C kwa alama sita, tatu nyuma ya viongozi Ghana. Mali waliungana na Guinea kileleni mwa Kundi A baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Namibia jijini Bamako. Mfungaji wa bao hilo la pekee alikuwa tineja El Bilal Toure katika dakika ya 38. Kwingineko, Niger waliwapokeza Ethiopia kichapo cha 1-0 katika mechi ya Kundi K jijini Niamey. Niger na Ethiopia kwa sasa wanajivunia alama tatu kila mmoja, tatu nyuma ya viongozi Ivory Coast na Madagascar.

Masumbwi: Mwakinyo hoyee!

Na bondia wa Tanzania Hassan Mwakinyo ameshinda tena kwa gumi zito la Technical Knock Out (KO) dhidi ya bondia Muargentina Jose Carlos Paz na kuendelea kutetea Mkanda wake wa WBF na kumfanya awe na jumla ya KO’s 12 katika mara 18 alizoshinda ndani ya mapambano 20 ambayo ameyafanya hadi sasa.

Bondia Muargentina alisalimu amri katika Round ya 4 katika Pambano la Round 12 la uzito wa Intercontinental Super Walter Weight siku ya Ijumaa, pambano lililofanyika katika ukumbi wa Next Door Arena kuwania Ubingwa wa WBF.

……………………..TAMATI……………..

 

Tags