Nov 26, 2020 00:50 UTC
  • Alkhamisi tarehe 26 Novemba 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Rabiuthani 1442 Hijria sawa na tarehe 26 Novemba 2020.

Siku kama ya leo miaka 1241 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani  mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Jaafar A.S mmoja wa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu. Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha AS kuwasili Khorassan nchini Iran, Bibi Maasuma alichukua uamuzi wa kuondoka Madina na kumfuata kaka yake huko Khorassan, lakini akiwa njiani aliamua kusimama katika mji wa Qum. Baada ya kupumzika katika mji mtakatifu wa Qum kwa muda wa siku 17 hatimaye bibi huyo mtukufu aliaga dunia kutokana na maradhi, au kama wanavyosema baadhi ya wanahistoria, kutokana na sumu aliyopewa. Bibi Maasuma A.S amezikwa katika mji huo mtukufu.

Siku kama ya leo miaka miaka 165 iliyopita, Adam Bernard Mickiewicz mshairi na mwandishi mkubwa wa Kipoland aliaga dunia huko Istanbul uliokuwa mji mkuu wa utawala wa Othmania. Alizaliwa mwaka 1798. Kama alivyokuwa baba yake, Mickiewicz naye alikuwa mtu aliyekuwa akipigania uhuru. Aliishi katika zama ambazo nchi yake ya Poland ilikuwa imegawanywa na madola ya Prussia, Russia na Austria na alikuwa akifanya jitihada ili nchi yake iungane tena na kuwa kitu kimoja. Ni kutokana na sababu hiyo ndiyo maana mwaka 1823 alibaidishiwa nchini Russia. Baada ya miaka 6, Adam Mickiewicz alikimbilia nchini Ufaransa na kuanza kufundisha fasihi ya lugha.

Adam Bernard Mickiewicz

Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo. Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani. Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti. 

Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchill na Joseph Stalin 

Miaka 7 iliyopita katika siku kama ya leo, watu 200 waliuawa na wengine 300 kujeruhiwa katika mji wa Mumbai nchini India kufuatia mashambulio kadhaa ya kigaidi na mapigano ya siku tatu baina ya vikosi vya usalama na magaidi. Hoteli kubwa mbili na kituo kikuu cha treni katika mji huo wa kibiashara wa Mumbai ni miongoni mwa maeneo yaliyolengwa katika mashambulio hayo ya kigaidi. Serikali ya India iliibebesha lawama Pakistan na kuituhumu kwamba, ilihusika katika mashambulio hayo kwa madai kuwa, magaidi waliofanya mashambulizi hayo walipata mafunzo nchini Pakistan. Hata hivyo Pakistan ilikanusha madai hayo na kutangaza kuwa iko tayari kushiriki katika uchunguzi wa pamoja na India ili kuwasaka wahusika wakuu wa mashambulio hayo ya kigaidi.

Tags